Ninaimani kwamba baadhi ya wapenzi wa muziki wa dansi humu nchini, hawamfahamu au hawamkumbuki mwanamuziki Omari Kungubaya.

Lakini kwa wale waliokuwa umri mkubwa miaka ya miaka ya 1970 hadi 1990, watakumbuka kulikuwa na kipindi cha Ugua pole, kilichokuwa kikirushwa kila Jumapili toka hospitali mbalimbali hapa nchini na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD).

Madhumuni makubwa ya kipindi hicho yalikuwa ni kuwapa faraja wangonjwa katika hospitali zilizopo mikoani nchini kote.

Kama alivyokuwa Mzee Moris Nyunyusa, aliyekuwa akipiga ngoma kumi kwa wakati mmoja, mirindimo ya ngoma hizo zikatumika kama kiashiria cha taarifa ya habari ya RTD.

Omari Kungubaya alitunga wimbo wa Salamu za Wagonjwa, ambao ulikuwa ndio kiashiria cha kufungua ama kifunga (Sign tune) ya kipindi cha Ugua pole.Haijambo Morris Nyunyusa, alifaidi ‘trip’ ya kwenda Japan kwenye maonesho wa biashara yaliyofanyika katika mji wa Osaka nchini humo mwaka 1970.

Kungubaya akajipatia umaarufu mkubwa, sehemu mbalimbali nchini kupitia wimbo huo.Ilikuwa mtangazaji katika eneo husika alipita katika hospitali akiwajulia hali wagonjwa, huku akiwapa nafasi ya kutuma salamu kwa ndugu, jamaa na rafiki zao kuwaeleza hali yake ilivyo.

Aidha mtangazaji alitoa fursa kwa mgonjwa kuchagua kibao akipendacho kuchezewa.Msikilizaji wa RTD iliyokuwa pekee humu nchini wakati huo, alijongea karibu mara baada ya kusikia kiashiria cha kipindi hicho ambayo ilikuwa ni wimbo wa ‘salamu za wagonjwa’.

Wimbo huo ulikuwa mfupi uliojaa faraja tele kwa mgonjwa, hata ndugu na jamaa za wagojwa hao.Wakati akipiga wimbo huo alikuwa akitumia gitaa la aina ya galatoni, lililokuwa na nyuzi sita.

Vijana wa kizazi hiki licha ya kutolijuwa gitaa hilo, pia hawakupata kusikia tungo zake kutokana na kutokupigwa tena katika redio hiyo, licha ya kuwa na Maktaba kubwa.Hapana shaka wakazi wa mikoa yote hapa nchini watakumbuka jinsi kipindi hicho kilivyokuwa kikiwakuna.

Mathalani wakazi wa Kanda ya Magharibi hususan mkoa wa Kigoma, hawawezi kumsahau mtangazaji wa RTD wakati huo, Chisunga Steven.

Alikuwa mwakilishi wa redio hiyo mkoani Kigoma, ambapo aliprndwa na watu kuatia mtindo wa aina ya mahojiano kwa wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika hospitali ya Maweni mkoani Kigoma.

Takriban kila mgonjwa alitamani kufikiwa na Chisunga, ili apate fursa ya kuhojiwa huku akiwafanyia ‘utani’ wa kurudishia kila neno alilokuwa likitamkwa na mgonjwa husika.

Kwa faida yako wewe kijana ambaye hakupata kuusikia wimbo huo au kwa yule aliyeusahau, kwa ridhaa yako nakuomba nikupe maneno yaliyomo katika beti hizi:

“Wakati umewadiwa wa salamu za wagonjwa hospitalini.

Leo tunawapa pole x2

Ajuaye Bwana Mungu kwa mzima kuwa mfu mgonjwa kuwa salama

Leo tunawapa pole x2

Kipindi chenu kinawapa pole

Wote tunawapa pole

Mungu awajalieni pole x2

Tunawapa pole x2.

Mashairi haya yalisikika kwenye kipindi cha Ugua Pole, kila siku ya Jumapili kuanzia saa 4.02 asubuhi hadi saa 5.00.

Ujumbe uliomo katika shairi hilo, unaweza kubaini ni kwa kiasi gani Kungubaya alikuwa na Weledi katika utunzi na uimbaji.

Omari aliwahi kutunga na kuimba wimbo wa “Nina mpenzi wangu Kibamba”, ulichukua ‘chati’ kwa kupendwa na wapenzi na washabiki wa muziki wa dansi wakati huo.

Mzee huyo alisahaulika hata kutamkwa kuwa alikuwa miongoni wa nguli walioiletea sifa kubwa tasnia ya muziki hapa nchini.

Kwa bahati mbaya pamoja na kazi zake hizo nzuri, hakuweza kunufaika kwa lolote nyimbo zake zote zimehifadhiwa katika maktaba ya TBC Taifa bila kuchezwa.Kufuatia umri wake kuwa mkubwa uliokadiriwa kuwa ana miaka 74, hakuwa na vyanzo vyovyote vya kujipatia pesa za kujikimu kimaisha.

Mara mojamoja Kungubaya alikuwa akienda kujitafutia riziki kwa kupiga muziki katika baa ya Luguluni Park, iliyopo maeneo ya Makondeko, jijini Dar es Salaam.Hapana ubishi kwamba wanamuziki wa zamani wengi wameaga dunia wakiwa ni mafukara, hata walio hai hali zao kimaisha ni dhoofu.

Ikumbukwe kwamba marehemu Muhidin Maalim Gurumo aliweza kupatiwa misaada japo kidogo wakati akiwa taabani nyumbani kwake.Hiyo ilitokana na vyombo vya habari kumfikia na kumtangaza. Kungubaya huko alikokuwa, yawezekana hakutembelewa na chombo chochote cha habari.


Wasifu wa Kungubaya

Omari Kungubaya lilikuwa tunda jingine toka Morogoro, ambako kuna hazina isiyokwisha ya wanamuziki wenye vipaji vya kila aina.

Matunda mengine yaliyotokea mjkoani humo ni pamoja na Salumu Abdallah Yazidu ‘SAY’, Mbaraka Mwinshehe, Hemed Maneti, Abel Balthazar, Juma Kilaza na wengine wengi.Kungubaya alizaliwa mwaka 1939 katika Kijiji cha Mgaza Vigolegole, mkoani Morogoro.

Nguli huyo alipata elimu ya msingi hadi darasa la nane, Msamvu Middle School mwaka 1955 mjini humo.Kungubaya alishindwa kuendelea na masomo kutokana na wazazi wake kukosa kumlipia karo.

Historia yake kimuziki ilianzia mwaka huo wa 1955 akiwa shuleni Msamvu, wakati huo akiwa na umri wa miaka 16.Omari aliweza kuchaguliwa kuwa kiongozi wa bendi ya shule (Band Master).Mara baada ya kumaliza shule akajiunga rasmi na bendi ya Cuban Marimba iliyokuwa chini ya Salum Abdallah Yazidu 'Say'.

Itakumbukwe kwamba, Cuban Marimba ilikuwa na maskani yake Nunge Welfare (sasa eneo hilo linajulikana kama Mji Mpya), mjini Morogoro.
Cuban Marimba yaelezwa kwamba ndiyo iliyoibua vipaji vya wanamuziki wengi, akiwemo Hemedi Maneti Ulaya.

Bendi hiyo ilikuwa tishio kwa bendi ya Morogoro Jazz na nyingi za Dar es Salaam.Katika mahojiano mzee Kungubaya alimtaja Kibwana Katashingo, aliyekuwa dereva wa marehemu Salum Abdallah.

Kibwana pia alikuwa mpiga drums wa bendi hiyo, kwamba ndiye aliyekuwa mwalimu wake wa kwanza katika muziki wakati alipojiunga na Cuban Marimba.Wakati huo yeye Kungubaya alikuwa akipiga gitaa la galatone lenye nyuzi sita.

Mwaka 1960 Kungubaya alichanja mbuga na kuelekea Nairobi, Kenya kwa kile alichosema alikwenda kujiendeleza kimuziki.Huko alipokewa na wanamuziki wakongwe wakiwemo John Ondolo Chacha, John Mwale na David Amunga, ambao wote walikuwa wakikung'uta magitaa ya galatone kwenye vilabu mbalimbali jijini humo.

Hata hivyo, mwaka uliofuatia, Kungubaya alirejea Morogoro na kujiungana na bendi ya Kilosa Jazz.Bendi hiyo ilikuwa ikiundwa na akina Yahya Abbas na Abel Balthazar, ambapo alidumu na bendi hiyo hadi mwaka 1963.

Omari Kungubaya baada ya kipindi kifupi aliamua kurejea tena Morogoro, ambapo viongozi wa bendi hiyo wakampeleka kwa Mzee Mwaipungu aliyekuwa akiongoza bendi nyingine iliyokuwa tawi la Cuban Marimba, lakini mwaka 1969 akaondoka.

Safari hii aliamua kuyaweka kando masuala ya muziki na kuwa 'Cashier' katika vituo vya kuuza mafuta vya Capital Esso Services, kilichopo mtaa wa India na baadaye kituo cha Agip Centre cha Mwembesongo mjini Morogoro mwaka 1970.

Omari alieleza kwamba, mwaka 1971 akaamua kurejea tena kwenye muziki, akiwa na mbinu mpya ya kujitegemea mwenyewe.Wakati huo alikuwa akipiga gitaa moja tu la galatone, ambapo alihamia Dar es Salaam na kuanza kutumbuiza katika baa moja iliyokuwa ikimilikiwa na Mama Hamm huko Tandale, Manzese.

Penzi, anasema, halina mipaka na halichagui fukara wala tajiri.Kwanini? Kungubaya alisema kwamba, bosi wake huyo Mama Hamm 'alimzimia' na kuanguka kwenye penzi zito.Hivyo akaamua kumuoa mama huyo, ambaye hadi anafariki mwaka 1995, hawakubahatika kupata mtoto.

Mzee Kungubaya alisema kwamba, kabla mkewe huyo hajafariki alimpa ruksa ya kuoa mwanamke mwingine, ili aweze kupata watoto.Kwa kuwa dini ya Kiislamu inaruhusu kuoa wake si zaidi ya wanne, Omari Kungubaya alioa mke mwingine wakabahatika kupata watoto watatu, ingawa mmoja alifariki.

Mwaka 1974 walinunua shamba kijijini Kwembe, ndiko alikuwa akiishi.
Kungubaya akawa mwanakijiji, shughuli zake zikawa ni kilimo japokuwa hakuwa na mtaji wa kutosha, mara nyingi atumia jembe la mkono kulima.
Nguli huyo aliwahi kusema kuwa ingawa yuko kijijini, lakini kwa vile muziki uko kwenye damu yake hawezi kuuacha.

Kila siku ya Ijumaa hadi Jumapili jioni, alikuwa akionekana katika baa mbalimbali huko Kibaha Maili moja, akiwatumbuiza watu kwa kutumia gitaa lake la galatone alilolinunua miaka ya 1970.Mara nyingi Kungubaya alikutwa akiimba nyimbo nyingi zilizopata kutamba miaka ya 1960 hadi 1970, hususan nyimbo kama Mtoto si Nguo na Ndugu sikilizeni navunja vunja vikombe zilizoimbwa na Heorge Mukabi wa Kenya.

Zingine ni za Wanawake wa Tanzania na Maneno madogo madogo kwa mabibi na mabwana zilizoimbwa na marehemu Salum Abdallah wa Cuban Marimba.Wakati wa uhai wake Omari Kungubaya alitunga nyimbo nyingi sana, lakini alisema kwamba, katika miaka 47 akiwa kwenye jukwaa la muziki, hakunufaika na chochote zaidi ya kuishia kutumbuiza vilabuni!

Aliiomba serikali kuweka utaratibu mzuri wa kuwajali Wanamuziki wa zamani kwa kuwaenzi na ikibidi iwekwe siku maalum ya kuwakumbuka wakongwe wa zamani na kazi zao.

Aidha, Kungubaya alisema kwa kuwa Sheria ya Haki Miliki imekwisha pitishwa na serikali, basi ni vyema hata wasanii wa zamani wafikiriwe kupewa japo chochote na Radio Tanzania kutokana na kazi zao zilizohifadhiwa huko, ambazo sasa RTD (TBC Taifa) imekuwa ikiziuza.

Mzee Omari Kungubaya aliaga dunia mwaka 2006 akiwa fukara.
Mungu aipumzishe roho yake pahala pema peponi, Amina.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...