Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Issac Kamwelwe leo akifungua Jukwaa la Pili la Kitaifa la Usafiri wa Anga linalofanyika kwa siku mbili kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam. 


SERIKALI imesema imeweka mipango kabambe ya kuboresha viwanja vidogo vya ndege (Airstrips), ili viweze kutumika kirahisi na ndege ndogo zinazosafirisha Watalii kutembelea mbuga mbalimbali za wanyama na vivutio vilivyopo nchini. 

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Issac Kamwelwe katika Jukwaa la Pili la Kitaifa la Usafiri wa Anga linaloendelea kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), ambapo tayari imeundwa kamati kutembelea viwanja hivyo, ambavyo amesema vipo zaidi ya 600 vikiwemo vya makampuni binafsi. 

“Hivi viwanja ndivyo vinavyoingiza Watalii ndani ya mbuga na vivutio vingine baada ya kushuka pale KIA (Kilimanjaro International Airport) na hapa Dar es Salaam Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), sasa hivi vinatakiwa viwe katika ubora mzuri utakaofanya Watalii kujiona wapo sehemu nzuri na salama,” amesisitiza Mhandisi Kamwelwe. 

Hata hivyo, Mhandisi Kamwelwe amesema Idara ya Uhandisi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), itaimarishwa zaidi ili iweze kufanya marekebisho kwenye viwanja hivi, ikiwezekana kununuliwa vifaa ili kufanya kazi kwa ufanisi. 

Pia amesema tayari Serikali imeweza kusimamia vyema mradi wa ujenzi wa Jengo la Tatu la abiria la JNIA, ambao umekamilika na limeongeza uwezo wa kuhudumia abiria, ambapo itahudumia abiria milioni sita kwa mwaka. 

“Ninawataka wafanyabiashara na wadau wengine wote kuchangamkia fursa za
kibiashara zilizopo kwenye jengo letu hili la kisasa, ambapo sasa nimetaarifiwa wapo katika hatua za kuwapata watoa huduma ndio maana ninasema mjitokeze kwa wingi kuomba,” amesema Mhandisi Kamwelwe. 

Akizungumzia viwanja vingine amesema baada ya kukamilika kwa upanuzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Songwe na Mwanza vitawekwa katika daraja la Kimataifa, kutokana na kuwa na miundombinu ya kisasa, ambapo kwa upande wa Mwanza ujenzi wa jengo la mizigo upo katika hatua ya mwisho kukamilika. 

Kwa sasa kiwanja cha ndege cha Songwe kipo daraja 3C na yakikamilika maboresho ya miundombinu kitakuwa daraja la 4D na Mwanza ni daraja 4C.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...