Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Ofisi ya Zanzibar imezitaka Kampuni za
utembezaji Watalii Zanzibar kusajili Kampuni zao na kulipa Kodi kwa
wakati ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.
Kwa kufanya hivyo kutawarahisishia kufanya kazi zao na kuwaondoshea
usumbufu ikiwemo kulipa faini ya kuchelewesha Kodi hizo.
Wito huo umetolewa na Afisa mwandamizi Elimu ya mlipa kodi TRA
Shuweikha S. Khalfan wakati akiwasilisha mada katika Semina ya utozaji
wa Kodi na uwasilishaji wa Taarifa za Mapato kwa Kampuni za utembezaji
Watalii Zanzibar iliyofanyika Raha leo mjini Zanzibar.
Amesema Sheria ya Kodi ya mapato ya mwaka 2004 ibara 4(1) inamtaka
kila mtu ambaye anapata kipato kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.
Amesema lengo la Semina hiyo ni kuendelea kutoa elimu kwa kila kundi
ambalo lina wajibu wa kulipa Kodi ili kuziba mianya ya upoteaji wa
mapato nchini.
Shuweikha amesema TRA inategemea sana wafanyabiashara katika
kufanikisha malengo yaliyowekwa ili kuindeleza miradi mbali mbali ya
maendeleo na huduma za kijamii nchini.
Wakichangia katika Semina hiyo Wawakilishi wa Kampuni hizo waliiomba
TRA kufanya utafiti wa kina kubaini mapato wanayoingiza kabla ya
maamuzi ya kutakiwa kulipa Kodi.
“Hakuna ambaye anakataa kulipa Kodi lakini lazima TRA wafanye Research
ya kina hasa maeneo tunayofanyia kazi ili wabaini kipato chetu maana
ukweli biashara ya kutembeza watalii imekuwa ngumu sana” Alisema
Mwakilishi wa Kampuni ya Coral Tour Khamis Makame
Khamis amesema Kampuni za kuendesha utalii zinapitia wakati mgumu
hivyo ni vyema kuwe na mikutano ya kuelimishana mara kwa mara kwa
lengo la kuongeza uelewa kwa wadau.
“Tunahitaji pia kila mtu kujua Kampuni yake inanufaika vipi na Kodi
inayoitoa hasa ikizingatiwa kuwa Kampuni inaweza kupita hata miezi
sita bila hata kupata mgeni wa kufanya naye kazi” Alisema Khamis.
Kwa upande wake Salim Salim amesema biashara hiyo imekuwa ngumu
kutokana na kuwepo kwa Tozo nyingi zinazotolewa bila kuangalia kipato
halisi wanachoingiza kwa mwaka.
Hivyo alishauri Semina zinazofuata TRA wawashirikishe Wadau wengine wa
Kodi kama vile ZRB na Halmashauri ili kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu
ulipaji wa Kodi.
Kwa upande wake Afisa Elimu ya Mlipa Kodi kutoka TRA Abd Seif amesema
maoni yaliyotolewa yatafanyiwa kazi ili kuhakikisha Makampuni hayo ya
kiutalii yanashirikiana vyema kulipa kodi bila tatizo.
Amesema wataendelea kutoa elimu kwa makundi yote ili kuziba mianya ya
ulipaji Kodi nchini.
Afisa Elimu ya mlipa kodi TRA Ofisi ya Zanzibar Abdallah Seif akionesha Kitabu cha Makadirio ya Bajet ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mwaka 2019-20 kwa washiriki wa Semina iliyohusu utozaji wa Kodi na uwasilishaji waTaarifa za Mapato kwa Kampuni za utembezaji Watalii Zanzibar iliyofanyika Raha leo mjini Zanzibar. Kulia ni Afisa mwandamizi Elimu ya mlipa kodi TRA Shuweikha S. Khalfan.
Mmoja wa wawakilishi wa Kampuni za utembezaji Watalii Zanzibar Salim Salim akihangia katika Semina iliyoendeshwa na TRA Ofisi ya Zanzibar huko Raha leo mjini Zanzibar kuhusu utozaji wa Kodi na uwasilishaji waTaarifa za Mapato kwa Kampuni za utembezaji Watalii Zanzibar.
Mwakilishi wa Kampuni ya Coral Tour Khamis Makame akichangia katika
Semina ya utozaji wa Kodi na uwasilishaji wa Taarifa za Mapato kwa
Kampuni za utembezaji Watalii Zanzibar iliyofanyika Raha leo mjini
Zanzibar.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...