*Yaelezwa Jiji la Dar, Tanga vinara kwa utumiaji wa dawa hizo
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
WANANCHI wa Jiji la Tanga wameendelea kupewa elimu kuhusu madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya nchini yakiwemo ya magonjwa ya maambukizi kwa walioathirika na utumiaji wa dawa hizo.
Elimu hiyo imetolewa kwenye maeneo mbalimbali yakiwamo ya vijiwe ambavyo kuna vijana ambao wamekuwa wakijihusisha na utumiaji wa dawa za kulevya au waliokuwa wanatmia na kuacha, pia elimu hiyo imetolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari pamoja na rika za makundi mbalimbali yaliyopo katika Jiji la Tanga.
Utolewaji wa elimu inayohusu madhara ya dawa za kulevya ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Dawa za Kulevya Duniani ambayo kilele chake itakuwa ni kesho Juni 26 mwaka huu.
Hivyo Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini imepiga kambi katika Jiji la Tanga kwa ajili ya kuhakikisha wanatoa elimu hiyo ambayo itasaidia kuifanya jamii kuwa sehemu ya kushiriki katika kukomesha dawa za kulevya nchini.
Michuzi Blog na Michuzi TV ambayo imepiga kambi katika Jiji la Tanga ili kukuuza kila kinachoendelea imeshuhudia namna ambavyo wataalam mbalimbali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inavyotoa elimu hiyo kwa wananchi.
Kamishna wa Idara ya Kinga na Tiba wa mamlaka hiyo Dk.Peter Mfisi amefafanua kuwa lengo la kutolewa kwa elimu hiyo ni kuhakikisha kila mmoja wetu kwa nafasi yake anashiriki kwenye vita ya kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya kwa athari zake ni kwa jamii nzima na si mtu mmoja tu.
"Kwa wanaotumia dawa za kulevya na hasa ambao tayari wameathirika na dawa hizo madhara yake ni makubwa sana.Utafiti unaonesha asilimia 40 ya walioathirika na utumiaji wa dawa za kulevya wanaishi na virusi vya Ukimwi.
"Pia wapo wenye magonjwa ya Kifua Kikuu(TB) lakini wengine wanasumbulia na homa ya ini.Hivyo madhara yake ni makubwa na kibaya zaidi magonjwa ambayo wanayo ni ya kuambikiza, hivyo wanaweza kuambikiza na jamii nyingine,"amesema Dk.Mfisi.
Alipoulizwa kwanini maadhimisho hayo yanafanyika katika Jiji la Tanga, amefafanua kuna sababu nyingi kwanza Mamlaka imekuwa ikifanya maadhimisho hayo kwenye mikoa mbalimbali kwa kila mwaka.
Hata hivyo kwa Tanga kuna umuhimu wake kwasababu utafiti wa mwaka 2014 ulofanywa na iliyokuwa Tume ya Dawa za kulevya unaonesha Tanga inashika nafasi ya pili kwa kuwa na watu 7000 wanaomia dawa za kulevya na nafasi ya kwanza kwa mujibu wa utafiti huo inashikwa na Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuwa na watumiaji 30,000.
"Pia tupo Tanga tukiendelea na utoaji wa elimu kwasababu wafanyabiashara hii ya dawa za kulevya wanaitumia Pwani ya Tanga kupitisha dawa hizo.Hivyo jamii ikiwa na uelewa wa madhara ya dawa hizo hawatakuwa tayari kuwa sehemu ya kushiriki kufanya biashara au kutumia kabisa,"amesema Dk.Mfisi.
Mmoja wa wakazi wa Jiji la Tanga, Athuman Shekimweri amesema anatoa pongezi kwa Mamlaka hiyo kwa namna ambavyo imeamua kuzunguka maeneo mbalimbali na kutoa elimu kwani imewafanya kutambua madhara ya kutumia dawa za kulevya na hivyo watakuwa mabalozi kwa wengine.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...