Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Madaktari na Wauguzi mara baada ya kutembelea chumba cha upasuaji cha hospitali ya Arusha Lutherani Medical Centre (ALMC) alipokwenda katika hospitali hiyo kuwashukuru kwa huduma na matibabu waliyoyatoa kwake alipopata ajali ya gari mwaka jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akiwa katika picha ya pamoja na Madaktari,Wauguzi na wafanyakazi wa Arusha Lutherani Medical Centre (ALMC) mara baada ya kutembelea hospitali hiyo kuwashukuru kwa huduma ya matibabu waliyoitoa kwake na kwa wasidizi wake alipopata ajali ya gari mwaka jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla (kushoto) akikaribishwa na Mkuu wa Idara ya magonjwa ya dharura cha Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) Dk. Peter Mabula mara baada ya ya kuwasili katika hospitali hiyo jijini Arusha leo (16 Juni, 2019) kuwashukuru Madaktari,Wauguzi na wafanyakazi wa hospitali hiyo kwa huduma na matibabu waliyoyatoa kwake na kwa wasaidizi wake alipopata ajali ya gari mwaka jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Madaktari,Wauguzi na wafanyakazi wa Arusha Lutherani Medical Centre (ALMC) alipokwenda katika hospitali hiyo kuwashukuru kwa huduma ya matibabu waliyoitoa kwake na kwa wasaidizi wake alipopata ajali ya gari mwaka jana.
………………….

WMU – Arusha.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla amewashukuru Madaktari, wauguzi na wafanyakazi wa hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ya jijini Arusha kwa huduma na matibabu waliyoyatoa kwake na kwa wasaidizi wake alipopata ajali mbaya ya gari Agosti 4, 2018 katika eneo la Magugu mkoani Manyara.

Dk. Kigwangalla ametoa shukrani hizo wakati akizungumza na Madaktari, Wauguzi na wafanyakazi wa hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre, jijini Arusha.

Akiwa ameambatana na mkewe Dk. Bayoum Awadh, amewashukuru na kuwapongeza madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kwa matibabu waliyompatia kwa kipindi chote alichokuwa hospitalini hapo na kuwaomba waendelee kuwahudumia wananchi wenye shida.Amesema kazi ya udaktari, uuguzi na fani zote zilizo katika sekta ya afya ni za wito na kila anayezifanya inampasa azifanye kwa wito kutoka ndani ya moyo wake.

“Kazi ya udaktari, uuguzi na fani zote zilizo katika sekta ya afya kwa kiasi kikubwa ni kazi ambazo mtu anazifanya kutoka ndani ya moyo wake kuwahudumia wengine ambao wako katika madhira mbalimbali ya kiafya” Amesema Dkt. Kigwangalla.

Amesisitiza kuwa hakuna namna ambayo Daktari au Muuguzi anayetoa huduma ya kumtibu mtu, kumwondolea maumivu, au kumpa faraja mgonjwa anaweza kulipwa na malipo hayo yakalingana na kazi aliyoifanya.
Amesema kazi ya Udaktari na Uuguzi inafanywa na watu wachache ambao kwa kiasi kikubwa wanakua wameitika wito ama wametumwa na Mungu na kwamba mtu yeyote hawezi kusema kuna kipato au kitu utakachoweza kumlipwa kikamtosheleza au kukidhi umuhimu na ugumu wa kazi anayoifanya.

“Kwa dhati ya moyo wangu ninatoa shukrani zangu za dhati lakini pia kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ambaye kwa muda wote toka tulipopata ajali alikua akifuatilia afya zetu, ninaomba nifikishe kwenu shukrani za Serikali anayoiongoza ya kwamba tunatambua mchango wenu mkubwa” Amesisitiza Dkt. Kigwangalla

Ameeleza kuwa yeye na wasaidizi wake waliopata ajali Agosti 4, 2018 walipita katika hospitali hiyo wakiwa na hali ngumu kiafya lakini kutokana na juhudi na upendo uliooneshwa na madaktari wa hospitali hiyo wakishirikiana na madaktari wa hospitali ya mkoa wa Arusha na KCMC waliweza kushughulika afya zao na kuokoa maisha yao.

“Tunawashukuru sana kwa yote mliyotenda, tunawaombea dua madaktari, wauguzi na watumishi wa kada zote zilizo katika sekta hii ya tiba hatuna cha kuwalipa zaidi ya kusema Mungu awabariki katika maisha yenu, awape mafanikio makubwa na ujuzi zaidi ili muendelee kuwasaidia wengine” Amesisitiza Dkt. Kigwangalla.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya magonjwa ya dharura cha Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC), Dk. Peter Mabula akizungumza kwa niaba ya uongozi wa hospitali hiyo amesema kuwa kitendo cha Dkt. Kigwangalla kupanga muda wa kwenda kuwashukuru kimewapa nguvu na moyo wa kuendelea kufanya kazi vizuri zaidi.

Dk. Mabula amemwomba Mhe. Kigwangalla atenge muda mwingine wa kuitembelea hospitali hiyo pia afikishe salam zao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwamba wataendelea kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...