Na: Moshy Kiyungi

Jina la Ally Choki siyo geni masikioni mwa washabiki na wapenzi wa muziki, anayetamba kwa kipindi kirefu Afrika Mashariki kupitia tungo nauimbaji wake.

Baada ya kuonesha vituko vingi kwenye kumbi mbalimbali,  baadhi ya washabiki wake walimpachika walimuita “Mzee wa Farasi” au “Mzee wa Kijiko”. Choki kila bendi aliyopita kupiga muziki, aondokapo huacha simanzi kubwa kwa wanamuziki wenziwe, washabiki na wapenzi wa muziki wa dansi.

Ni mwenye vipaji vingi vilivyojengeka kichwani mwake vikiwemo vya kutunga, kuimba pamoja na uongozi.

Historia yake katika muziki Choki iliieleza kwamba alianza muziki rasmi mwaka 1988, alipojiunga katika bendi ya Lola Africa. Baadaye akajiunga na bendi ya Mwenge Jazz iliyokuwa chini ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Hakudumu kwa kipindi  kwani baada ya miezi sita alihamia katika bendi ya Bantu Group iliyokuwa ikiongozwa na ‘Komandoo’ Hamza Kalala.

“Mwaka 1990 nikiwa Bantu na Hamza Kalala akiwa kiongozi tulitoa albamu ya Baba Jane. Mwaka 1991 nilitoka Bantu, nikajiunga na Legho Stars chini ya uongozi wa Tshimanga Kalala Assosa...” alisema Ally Choki

Safari ya kusaka mafanikio ilikuwa ikisababisha kwenda huku na kule ambapo huko Legho Stars, nako hakudumu sana akaamua kurudi katika bendi ya Bantu Group.

Choki alikuwa mithiri ya Kunguru kwani  huko nako hakukaa sana, akaenda kujiunga na  bendi ya Bendi ya MK Beat ‘Tukunyema’ iliyokuwa ikiongozwa na Shem Ibrahim Kalenga.

Mwaka 1992 alihamia katika bendi ya Washirika Stars ‘Watunjatanjata’ ambako walitoa albamu iliyopewa jina la Gubu la Wifi. Pale walikuwa na mwimbaji mahiri Adam Bakari ‘Sauti ya Zege’, mpapasaji Kinanda Abdul Salvado ‘Father kidevu’ na wengine wengi.


Katika harakati za kusaka maisha Ally Choki aliamua kuvuka mpaka wa nchi nakuingia  katika jiji la Nairobi, nchini Kenya mwaka 1994, ambako aliungana na wanamuziki wengine akiwemo Muumini Mwinjuma, wakaanzisha bendi yao ikiitwa Extra Kimwa mwaka 1998.

Ilipotimu mwaka  mwaka 1999, aliamua kurejea nchini  baada ya kupata taarifa kuwa mama yake mzazi kuwa alikuwa mgonjwa.

Ally akiwa hapa nchini aliamua kujiunga katika bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’  chini ya uongozi wa mkurugenzi Asha Baraka. Choki alikubali kujiunga na bendi  hiyo baada ya kupokea ushauri kwa mwanamuziki mwenzake Robert Hegga ‘Caterpillar’ ambaye walikuwa wote Nairobi.

Mwaka 2000 walitoa albamu iitwayo Jirani ilikuwa na nyimbo nyingi lakini Jirani ulikuwa utunzi wake yeye Choki.

Kama kuna kitu ambacho hawezi kukisahau wakati akiwa Twanga, ni pale wanamuziki wengi walihama bendi hiyo na kwenda kujiunga na bendi nyingine ya Chuchu Sound. Wengine wakatimkia katika bendi ya Mchinga Sound, akiwemo Adolf Mbinga mpiga solo.

Busara zake akazitumia kwa kumfuata mpiga solo mwingine Miraji Shakashia ‘Shaka Zulu’.

Shakashia naye hakudumu kwa kipindi kirefu akatimka, ndipo nafasi yake ilishikwa na Kassim Rashid ‘Kizunga’ aliyekuja kupiga gitaa la rhythm.

Baadae alipewa cheo kuwa kiongozi wa bendi na ndipo walipotengeneza albamu ya Fainali Uzeeni. Albamu hiyo ilifuatiwa na ile ya ‘Ukubwa Jiwe’ hatimae ‘Chuki Binafsi’.

Ally Choki alikuwa na kila sababu  za kujivunia akiwa hapo Twanga, kwa kuwa alikuwa akiongoza kwa kutunga nyimbo nyingi zilizovuma.

Baada ya kujipima uwezo wake, akanzisha bendi yake ya Extra Bongo mwaka 2003. Bendi hiyo ilikusanya wanamuziki wengi mahiri hapa nchini na kuweza kuwa tishio kwa bendi zingine hususan katika jiji la Dar es Salaam.

Choki aliweza kushirikiana kuima na baadhi ya wanamuziki akiwemo Muhidin Maali Gurumo, walipotoka na wimbo wa ‘Jirani’. Aidha alishirikiana na Ndanda Kossovo katika wimbo wa ‘Bea’.

Lakini kama wasemavyo waswahili “Penye riziki hapakosi fitina” ndivyo ilivyotokea kwa Ally Choki ambapo fitina ikatengenezwa  na wanamuziki wake wakanunuliwa akabaki  pasipo ‘mweupe’

Kutokana na hali hiyo, alilazimika kuiacha bendi yake na kwenda kujiunga katika bendi ya Mchinga. Huko nako hakudumu kwa kipindi kirefu, akarejea tena Twanga Pepeta.

Baadaye tena akajiunga na kundi zima la Tanzania One Theater lililokuwa likiongozwa na Kapteni mstaafu John Komba.

Akiwa ni mmoja wa viongozi wa TOT, Choki alifanikiwa kuipandisha chati bendi hiyo baada ya kuwaleta wanamuziki toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Alidumu na bendi hiyo ya TOT hadi mkataba wake ulipokwisha, akaamua kuifufua tena bendi yake ya Extra Bongo mwaka 2009.

 Ally Choki akizungumzia kisa cha sababu za kushuka kwa kiwango cha muziki wa dansi, Choki alikanusha kauli hiyo.

Alisema kwamba muziki wa dansi haujashuka kiwango isipokuwa vyombo vya habari vimeupa kisogo kwa kuangalia zaidi muziki wa Bongo Fleva, licha ya wao kuntoa nyimbo nzuri na hata video.

“Uongozi wa bendi za muziki ni mgumu ukilinganisha na mwanamuziki wa Bongo Fleva ambapo kiongozi hana wanamuziki wengi. Hata hivyo naamini kuna muda utafika muziki huu utakuwa juu…” alisema Ally Choki.

Choki akithamini mchango mkubwa wa wanamuziki waliomtangulia, alimuelezea marehemu Muhidin Maalim Gurumo, kuwa alikuwa mwalimu na mtu anayesikiliza ushauri.

Alisema kwamba yeye binafsi alifanya naye kazi nyingi zikiwapo zili walizotoa albamu yenye nyimbo zake tatu na za Gurumo tatu.

“Album hiyo ilifanya vizuri sana na tulipata fedha nyingi mpaka kila ninapokutana naye akawa anasema nakushukuru sana kijana….” Alisema Ally Choki.

Akielezea siri ya mafanikio yake , Choki alieleza kuwa yanatokana na yeye kufanya juhudi, kutokuvuta sigara wala kunywa pombe aliyoanchana nayo 1994.

Aidha amesema kwamba anamiliki nyumba, gari, mke na watoto sita.

Ikumbukwe kabla ya kuondoka African Star, alikwaruzana na mkurugenzi wake  Asha Baraka. Katika  purukushani hizo Choki alifika mbali kwa kutoa kiapo kibaya dhidi ya mkurugenizi wake  huyo.

Kwanza kitendo cha ASET kumpeleka mahakamani kumdai gari, pili ASET kukataa kurudisha pesa za Miraji Shakashia na tatu ni ASET kutothamini michango ya wasanii walioizalishia pesa nyingi.

Choki alisema kitendo cha ASET kumpeleka mahakamani kumdai gari ambalo walimpa mwenyewe kilimkera sana.

Kama Wahenga walivyonena kuwa “Wangombanao ndo hao wapatanao” Ally Choki baadaye alirejea tena bendi yake ya zamani ya African Star ‘Twanga Pepeta’.

Baadaye Ally Choki alikwenda jijini Mwanza akajiunga katika bendi ya Orchestra Kamanyola. Huko ameungana na watunzi na waimbaji wenzake mahiri akina Benno Villa Anthony na Mukumbule Lolembo ‘Parashi’.

Julai 2019, alisikika akiimba nyimbo katika bendi yake ya zamani iliyolea kwa kipindi kirefu ya African Stars  ‘Twanga Pepeta’

Mwandaaji wa makala anapatikana kwa namba: 0784331200 , 0736331200, 0713331200 na 0767331200

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...