Na Moshy Kiyungi,Dar es Salaam.

Kosmas Tobias Chidumule alikuwa mwanamuziki wa muziki wa dansi, akitumia sauti yake nyororo kufikisha ujumbe mwanana kwa wapenzi wa muziki huo.

Baada ya kuutumikia muziki wa kidunia kwa kipindi kirefu, Chidumule aliamua Kuokoka, na hivi sasa ni Mchungaji akihubiri injili .

Licha ya kufanyakazi ya kumtumika Mungu, nguli huyo bado anafanya muziki lakini ni wa injili.Sauti wakati wa kuimba, hadi leo bado haijabadilika licha ya umri kumtupa mkono.

Kosmas popote ukutanapo naye huoneka ni mwenye furaha, afya njema, utanashati wake, ucheshi, utani kwa wingi.Kila bendi aliyopita aliacha simulizi kwa wapenzi na mashabiki wake kufuatia tungo na uimbaji wake usiobadilika Abadan.

Msomaji wa makala hii, nikukumbushe wimbo mmoja wa Neema, ambao mpaka leo unaporindima watu hawakosi kutikisa vichwa vyao, ni kati ya tungo nzuri za Kosmas.

Chidumule ni mwanamuziki mwenye vipaji vya kutunga na kuimba kwa umahiri mkubwa nyimbo za muziki wa dansi na sasa za injili.Gwiji huyu kabla ya kuokoka alipitia bendi nyingi za muziki wa dansi hapa nchini.

Alisimulia kwamba alianza kupenyeza katika tasnia ya muziki wa dnsi miaka ya 1970, akiwa katika bendi ya Butiama Jazz.Butiama Jazz ilikuwa na makao yake jijini Dar es Salaam, kukienzi kijiji alichozaliwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kosmas akielezea safari yake katika muziki wa dansi, alibainisha kuwa alipiga muziki katika bendi hiyo kabla ya kuhamia bendi ya Urafiki Jazz, iliyokuwa ikiongozwa na Juma Mrisho ‘Ngulimba wa Ngulimba.

Hata hivyo huko nako hakudumu kwa kipindi kirefu, aliondoka akaenda kujiunga na wanamuziki wengine miaka hiyohiyo ya 1970, wakaanzisha bendi ya Dar International, ambako aliungana na mtunzi na mwimbaji Marijani Rajabu. 

Katika harakati zake za muziki Chidumule alichomoka akaenda kungana na wanamuziki wengine wakaanzisha bendi ya Orchestra Mlimani Park, iliyompatia umaarufu mkubwa.

Akizungumzia kilichopelekea kuhama kwake mara kwa mara toka bendi moja hadi nyingine Chidumule alisema kwamba hizo zilikuwa ni harakati zake binafsi za kutaka kujiinua kimuziki na kimaslahi zaidi.

Katika harakati hizo za kusaka maslahi, aliwahi kupiga muziki katika bendi za Vijana Jazz wakati huo ilikuwa ikiongozwa na Hemed Maneti na Orchestra Mlimani Park, inayotumia mtindo wa ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’

Baadhi ya wanamuziki aliokuwa nao wakati huo ni Abel Balthazar, ambaye ndiye aliyekuwa kinara wa waanzilishi wa bendi ya Orchestra Mlimani Park.Wengine ni pamoja na yule aliyekuwa mtaalamu wa kupiga ala zote Michael Enoch ‘Teacher’, Joseph Bernard, Joseph Mulenga ‘King Spoiler’ Abdalah Gama, Machaku Salum na Habib Jeff.

Bendi hiyo ilikuwa imeweka maskani yao katika Klabu ya Mlimani, maeneo ya Mwenge jijini Dar es Salaam.Mlimani Park ‘iliwanyakua’ watunzi na waimbaji mahiri akina Muhidin Maalim Gurumo na Hassan Rehani Bitchuka.Kwa pamoja walishirikiana vyema kutunga na kuimba vibao motomoto wakitumia mtindo wa ‘Sikinde ngoma ya Ukae’.

Chidumule aliweza kutunga na kuimba nyimbo nyingi zilizompatia umaarufu mkubwa kufuatia ujumbe uliokuwamo kwenye nyimbo zake zikiwa na mafundisho mazuri kwa jamii.Baadhi ya nyimbo hizo ni 'Barua kutoka kwa mama', 'Neema', 'Telegramu', pia alitunga na kuimba nyimbo za Ubaya, Nalala kwa taabu, Usitumia pesa, Ugomvi wa Baba na Mama, Epuka na maeneo.

Mwishoni mwa miaka ya 1980 Chidumule alijiunga katik bendi ya Orchestra Super Matimila, iliyokuwa ikiongozwa na Ramadhan Mtoro Ongala ‘Dk. Remy’.Akiwa na bendi hiyo alitunga nyimbo nyingi ukiwemo wa “Dodoma makao Makuu”, uliompa sifa lukuki kila pembe humu nchini.

Katika wimbo huo alijizolea sifa lukuki kwa kuongeza maneno machache ya lugha ya Kiingereza.Chidumule alibainisha kwamba kujiunga kwake na bendi ya Orchestra Super Matimila, ilikuwa ni mapenzi yake makubwa kwa Ramadhan Mtoro Ongala ‘Dk. Remy’, zaidi ya bendi yenyewe."Nilimpenda Dk. Remy tangu alipokuja katika bendi ya Ochestra Makassy na yeye pia akinikubali sana nilipokuwa Urafiki…" alisema.
Alifafanua kuwa mara baada ya kujiunga na bendi hiyo kuna wakati Dk. Remy alimwachia bendi kwa miezi sita, alipokwenda Ulaya.

Orchestra Super Matimila ilipata mwaliko wa kushiriki katika maonesho barani Ulaya mwaka 1988, baada ya shirika linalopandisha chati wanamuziki na wasanii mbalimbali kutoka katika nchi za dunia ya tatu, World of Music, Arts and Dance (WOMAD) kuvutiwa na nyimbo zao.

Chidumule akaunda kundi la Serengeti. Dk. Remy aliporudi akaendelea kutumia kundi la Serengeti maana wale aliokwenda nao Ulaya wengi ‘walizamia’ huko.Kosmas baada ya kuokoka alianza kutamba katika medani ya muziki wa injili mwaka 1999.

Akithibitisha hilo alisema, alitoka kwenye bendi ndogo sana na kuweza kupiga muziki kwenye bendi kubwa zenye wanamuziki wenye majina makubwa.Akizungumzia uamuzi wake wa kuachana na muziki wa dansi Chidumule alisema "Niliacha bendi ya Orchestra Matimila nipoamua kuokoka baada ya kupata maono tulipokuwa safarini kwenda Dodoma kupiga muziki. Sauti iliniijia ndotoni na iliniuliza nini hatma ya maisha yangu ya kimuziki…"

"Sauti hiyo ilinisimbua sana hata baada ya kufika Dodoma. Tulipofika ukumbini sikuwa na hamu ya kuimba.Kiongzi wangu Dk. Remmy alibaini jinsi nilivyokuwa nimenyong'onyea, akanipa glasi ya Konyagi ili nitoe ‘Nishai’, ikanidondoka na kuvunjika nikakimbia stejini maana kwenye glasi ile niliona umetoka upanga au mkuki.

Siku iliyofuatia nikarudi Dar es Salaam asubuhi nikatangaza redioni, Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na kwa uongozi na wanamuziki wa bendi yangu kwamba mimi nimeamua kumfuata Mungu, nimeokoka…" alisema Kosmas Chidumule.

Kosmas Chidumule alipiga na bendi Super Matimila hadi ilipotimu mwaka 1993, alipoamua kuokoka na kuamua kumtumikia Bwana.Hivi sasa ni mchungaji, mhubiri, mtunzi na mwimbaji wa nyimbo za ijili.

Alifanikiwa kutoa albamu yake ya kwanza ya injili iitwayo 'Yesu ni Bwana'. Baadaye alitoka na Hosanana, Nani Alaumiwe na Furaha yangu. 'Yesu ni Bwana', 'Kimbilia kwa Yesu' na 'Sioni pa Kwenda.

Kama mwanamuziki mzoefu, Chidumule hakusita kutoa ujumbe akisema “Ujumbe wangu kwa wapenzi wa muziki wa dansi wanakazi kubwa ya kuwahurumia wanamuziki kwa sababu wengi wao wanaishi maisha halisi ambayo ni tofauti kabisa na kile wanachokiimba.

Mazingira ya muziki wa dansi ni hatarishi sana, japo wanamuziki wanaimba vyema. Tunapiga kwenye vilabu, wengi wa wapenzi wa muziki ni walevi, hata kama hunywi unalazimika kuishi kama mlevi ili ukubalike kwa wapenzi wa kazi yako…"

"Nyimbo zangu za dansi zilikuwa na mafundisho kabla ya kuokoka kwani Mungu alishanichagua tayari, tatizo mimi mwenyewe nilikuwa sijajitambua. Nilikuwa nawakanya watu lakini mimi mwenyewe nikifanya kinyume na yale niliyoimba." alisema Chidumule.

Chidumule alienda mbali zaidi akasema

“Wokovu ni maisha ya Yesu ndani ya mwanadamu sio dini, ndo maana mimi sishughuliki na dini bali miili na nafsi za watu…”

Akizungumzia utunzi wa nyimbo zake, Chidumule alikuwa na haya ya kusema, "Utunzi wangu huongozwa na maono, nikisukumwa sana na wazo fulani ndipo ninapotengeneza nyimbo zangu. Naandika sana na kuhifadhi kwenye maktaba. Ziko nyimbo niliandika kama "Naifariji Nafsi Yangu", iliyo kwenye albamu yangu ya mwisho, mwaka 1996, iko kwenye albamu yangu ya tatu."

"Pamoja na kuhubiri kwa muziki naheshimu pia vyombo vya binadamu kama COSOTA. Vyombo hivi vinahitaji kushirikiana na Jeshi la Polisi au Mahakama ili kuweza kudhibiti vyema kazi za watunzi wa kazi za muziki..” alitamka Kosmas Chidumule.

Aidha aliiomba COSOTA ifike hadi ngazi ya chini kabisa kama Kanda, na ifanye kazi kwa mtazamo wa Kiafrika Mashariki.Chidumule alijinasibu kwa kuusifia muziki wake kwamba umempa umaarufu lakini bado hajafaidika kama muuzaji wa muziki wake anavyofaidika.

Alitolea mfano ukiuzalisha kwa gharama ya shilingi milioni 3, ukisharudisha fedha hiyo huingia mkataba mwingine mpya wa namna ya kugawana mapato hayo lakini hiyo ni tofauti.Chidumule alilalama akisema unaweza kumkuta mtu anauza kazi yake hata baada ya miaka mitano na bado hupati chochote, wakati yeye ananunua magari na kujenga majumba.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...