Baadhi ya Wanawake wanapofikisha umri wa zaidi ya miaka 50, huonekana ‘kuchoka’, hawana uwezo wa kufanya kazi za nguvu nyingi, lakini dhana hiyo ni tofauti kwa Anna Mwaole.
Mama huyu ni mwanamuziki mkongwe, aliyetimiza miaka 54 mwaka huu 2019.
Yawezekana baadhi ya watu hawamfahamu mwanamuziki huyo ambaye amepanda na kushuka milima na mabonde hadi kukubalikana na wapenzi wa muziki wa dansi na taarabu hapa nchini.
Anna Mwaole amefanikiwa kutimiza malengo yake baada ya kyakwepa majaribu lukuki aliyokumbana nayo hususan katika tasnia hiyo ya muziki.
Ni mama aliyejaaliwa vipaji vingi vikiwemo vya uigizaji, uimbaji wa nyimbo za dansi na taarabu.
Mwaole ukimwangalia kwa wasiwasi hauwezi kuamini kama anaweza kulishambulia jukwaa kwa kucheza hasa ukizingatia umbo lake la mwili lilojaa minofu kila maeneo.
Uzoefu na vipaji vyake aliviendeleza baada ya kupitia katika bendi mbalimbali za muziki wa dansi alizopitia na vikundi vya taarab.
Anna Mwaole alizungumza na mwandishi wa makala hii alisema kuwa yeye ameimba nyimbo nyingi za muziki wa dansi na taarabu, katika bendi zaidi ya nane hapa nchini akitafuta maisha na harakati za kujiedeleza kimuziki.
Historia ya maisha ya Mwaole mwenye asili ya mkoa wa Iringa, inaanzia katika mji wa Mpwapwa mkoani Dodoma, ambako mama huyo ndiko alikozaliwa mwaka 1965.
Anna akiwa yu ngali kigori, alikuwa akihusudu sana sauti na uimbaji wa mwanamuziki wa kike toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Marikirala Mboyo ‘M’bilia Bel’.
Alisema kila mara alikuwa akinunua kanda za M’bilia, akanza kujifunza kuimba nyimbo zake.Mwaole alijiunga katika kwaya ya Kanisa mjini Mpwapwa 1989, akiwa na Rahma Shaari.
Anasimulia kuwa yeye na Rahma Shaari walikuwa waimbaji wakutegemewa katika kwaya ya Kanisa hilo.Anna Mwaole alifafanua kwamba kabla ya hapo yeye na Ramha Shaari walikuwa waumini wa dini wa Kikristo.
Alimuelezea Rahma kwamba alikuwa akiitwa Grace, lakini baada ya kuolewa na mwislamu, akalazimika kusilimishwa akapewa jina hilo la Rahma.Halikadharika yeye Anna naye aliolewa na mwanamume mwislamu aliyemtaja kwa jina la Rashidi Nyambya.
Huyo ndiye aliyesababisha kusilimu na kuingia dini ya kiislamu, akachagua jina la Sauda.Sauda Mwaole anamtaja Rahma Shaari kuwa ndiye aliyechangia kwa kiasi kikubwa kwa yeye kuingia katika tasnia ya muziki wa dansi, muda mfupi baada ya kufika jijini Dar es Salaam mwaka 1988.
Alisema wakati huo alimkuta Rahma akiimba katika bendi ya Maquis du Zaire, ambapo alimuombea nafasi ya kuimba katika bendi hiyo mwaka 1989.
Sauda alifafanua kwamba ushawishi wa Rahma kwa uongozi wa Maquis ulifankiwa, akaitwa na kufanyiwa usaili kwa kuimba wimbo wa ‘Nakei Nairobi’ wa M’bilia Bel na ule wa ‘Kama umenichoka mpenzi’ ulioimbwa na Issa Nundu wa bendi hiyo.
Wimbo wa ‘Nakei Nairobi’ kwake ilikuwa kama ‘kumsukuma mlevi’ kwani tayari alikuwa amezifanyia mazoezi nyimbo zote za M’bilia Bell toka wakati akiwa Mpwapwa.
Kwa majigambo Sauda Mwaole alisema aliuimba wimbo huo kwa kujiamini hadi baadhi ya viongozi wa bendi hiyo wakiwemo akina Chibangu Katayi ‘mzee Paul’, Chinyama Chiyaza, Nguza Mbangu ‘Vicking’ na Tshimanga Kalala Assosa, hawakuamini masikio yao, walimkubali papo hapo akapata ajira.
Siku ya kwanza kupanda stejini akiwa na Maquis du Zaire, Mwaole anaeleza kwamba alitetemeka mno mara alipoambiwa kuimba mbele ya wapenzi na mashabiki katika ukumbi wa Wapi wapi’s Bar iliyokuwa Chang’ombe Maduka mawili.
“Nilitamani ardhi ipasuke, nitumbukie humo. Nilihofu hasa baada ya kuona jinsi wapenzi na mashabiki wa Maquis waliokuwa wamefurika ukumbini humo wakiniangalia mimi ” alitamka Mwaole.
Lakini anamshukuru mungu alimpa ujasiri akaimba kwa umahiri mkubwa wimbo wa ‘Kama umenichoka mpenzi’ akishirikiana na Issa Nundu.Sauda Mwaole alisema alipoimba wimbo wa ‘Nakei Nairobi’, watu waliinuka kwenye viti vyao wakishangilia na kumtuza pesa, huku wakitamka kwamba wamepata M’bilia Bell wa Tanzania.
Walitamka hayo kwa vile sauti na uimbaji wake haukutofatiana na wa Bell.
Mwaole alisema hatoweza kuisahau siku hiyo katika maisha yake, kwa kuwa ndiyo ilikuwa imemfungulia ukurasa mpya wa maisha yake katika fani ya muziki.
Mwezi Septemba 1989, alichukuliwa katika bendi ya Polisi Jazz, ambako alilazimika kwenda ‘depo’ za kijeshi kwa miezi mitatu, Kilwa road jijini Dar es Salaam.Akiwa katika bendi hiyo alikutana na wanamuziki wengine anawataja kwa majina ya akina Mobari Jumbe, Maimuna Ramadhani, Hamza Mwanamasingi, Ali Moshi na wengine wengi.
Akiwa na Polisi Jazz alitoka na wimbo wa ‘Sitaki sitaki visa vyako’ wimbo uliotungwa na Mobari Jumbe.
Mwaole alipenda kujiendeleza zaidi katika fani hiyo ya muziki, hivyo akaondoka kwenda kujiunga na bendi ya Bantu Group, iliyokuwa ikiongozwa na ‘mzee wa madongo’ Komandoo Hamza Kalala.
Akiwa Bantu Group alikutana na vijana wengine chipukizi akina Muumini Mwinjuma, Musemba wa Minyungu, Rogers na wapiga gitaa Magele Sange na Ali Adinani.
Alisema hakutarajia kwamba ipo siku angelikuja kuingia katika studio kurekodi nyimbo. Lakini kwa mara ya kwanza aliweza kuingia studio kurekodi wimbo wa ‘Emma tupunguze matumizi yasiyo ya lazima’
Safari ya Mwaole haikuishia hapo, kwani mwishoni mwa 1991, alijiunga katika bendi ya Orchestra Makssy iliyokuwa ikiongozwa na Mzee Kitenzogu Makassy.
Baada ya mwaka mmoja kupita ‘alichupa’ na kwenda kujiunga na bendi ya Lego Stars, iliyokuwa na wakali akina Joseph Bartholomew Mulenga ‘King Spoiler’(solo), Anania Ngorika, Kapaya Vivi na Chibanda Sonny (waimbaji)
Bendi ya Legho iliposambaratika, Mwaole akaenda kujiunga na Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ na bendi yake ya La Capitale.
Nyota yake ikamuangazia zaidi kwani Januari 1993, alijiunga katika bendi ya Washirika ‘Watunjatanjata’ Bendi hiyo ilikuwa na wanamuziki wakubwa ambao waliweza kumsaidia kuinua kipaji chake cha kuimba.
Aliwataja wanamuziki hao kuwa ni pamoja na Madaraka Morris, Adam Bakari ‘Sauti ya zege’, Eddy Sheggy na Christian Sheggy na Mhina Panduka’ Toto tundu’
Hapo napo akaona hapatoshi, akajiengua kati ya mwaka 1993 hadi 1995, akaenda katika bendi ya Tanza Muzika iliyokuwa ikimilikiwa na Elvis Musiba. Elvis Musiba kwa vijana wa zamani watamkumbuka kwa utunzi wake wa kitabu chake cha ‘Simu ya Kifo’
Anna alifafanua kuwa katika bendi hiyo aliwakuta wanamuziki wenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, François Makassy ‘Makassy Junior’, Kasongo Ilunga, na Chibanda Sonny.
François Makassy ni mtoto wa Mzee Kitenzogu Makassy.
Msemo usemao kwamba ‘Wazee dawa’ Sauda Mwaole alioufanyia kazi pale alipoamua kwenda kuchota mawazo, fikra na ujuzi toka kwa wazee wa bendi ya Shikamoo Jazz ya jijini Dar es Salaam.
Wanamuziki wazee aliowakuta katika bendi hiyo anawataja baadhi yao kwamba ni akina Salimu Zahoro, John Simon, Juma Mrisho ‘Ngulimba wa Ngulimba’ na Majengo Selemani.
Akiwa na Shikamoo Jazz, alibahatika kusafiri akiambatana na bendi hiyo iliyofanya ziara na kupiga muziki katika mji wa Kampala nchini Uganda.
Miezi sita ilitosha kuyapata aliyoyadhamiria, hivyo aliondoka kwa wazee wa Shikamoo Jazz na kutimkia bendi ya Matimila ya Dokta Remy Ongalla kwa kipindi kifupi kabla ya kujiunga na bendi ya Super Volcano, iliyokuwa ikiongozwa na Binti ya Mbaraka Mwinshehe Mwaruka, Taji Mbaraka.
Sifa zake za kupitia Jeshi la Polisi zilipelekea yeye apate kazi kiulaini katika bendi ya Magereza Februari 1998.Akiwa Magereza Jazz alitoka na wimbo wake wa ‘Samahani Baba watoto’ akishirikiana kuimba na akina Makoye Kwirukwira, Sharifa Bernard na wengine.
Sauda katika juhudi za kuhangaika kutafuta kujiendeleza zaidi katika tasnia ya muziki, alikwenda kujiunga na bendi ya Vijana Jazz anayomilikiwa na Jumuiya ya Vijana Tanzania. Huko alikutana na waimbaji ambao alisema walimuongezea chachu katika kipaji chake cha kuimba.
Aliwataja wanamuziki hao kuwa ni Suleiman Mbwembwe, Freddy Benjamin, Abdallah Mgonahanzelu, na mwana dada wakati huo Nuru Muhina’ Baby White’ Kwa upande wa ala za muziki, walikuwepo Miraji Shakashia ‘Shakazulu’ Kulwa wa Milonge, Mawazo Hunja na Rashid Pembe. Wote hao anawashukuru kwa kumuongezea ujuzi katika muziki.
Ilikuwa mwaka 2001 ambapo msanii maarufu wa kucheza na Nyoka, Norbert Chenga, alipomchukua mwanamama huyo kwenda kujiunga katika kikudi cha Muungano dancing Troupe.
Alipofika hapo akaambiwa azifanyie mazoezi nyimbo za taarabu za alizokuwa akiziimba Nasma Hamis ambaye alikuwa tayari katimkia kundi lingine.Nyimbo hizo alizitaja kuwa ni za ‘Mtu mzima ovyo’, ‘Hata mkisema’, ‘Sanamu ya mMichelini’ na nyingine nyingi.
Kipaji cha Sauda Mwaole kilijoinnesha mapema hapo Muungano, baada ya kuzitendea haki nyimbo hizo. Aliweza kuziimba huku wapenzi wakisema kumbe pengo laweza kuzibika.
Aliimba nyimbo zote za Nasma pasipo mtu kubaini kuwa anayeimba hakuwa Nasma.Mashabiki papo hapo walimpachika jina la Nasma Junior.Akiwa Muungano dancing troupe, Mwaole licha ya kuimba taarabu pia aliweza kucheza sarakasi na ngoma za asili zalizokuwa zikichezwa na kikundi hicho.
Mwaole alikuwa mtafutaji ikizingatia msemo usemao ‘atafutae hachoki, na akichoka kaisha pata’ Ndivyo ilivyokuwa kwa mama huyo ambaye mwaka 2004 aliachana na Muungano baada ya kutokuelewana katika mpango mzima wa maslahi.
Mwaka 2006 aliomba kurudi kwa King Kiki ‘Bwana Mkubwa’ katika bendi ya La Capitale. Sauda alikubaliwa japo alikaa na bendi hiyo kwa muda mfupi sana, akaamua kwenda kupiga muziki katika hoteli mbalimbali mjini Zanzibar mwaka 2007.
Mkataba ulipomalizika huko Zanzibar, alikwenda katika bendi ya Bana Maquis inayoongozwa na Thsimanga Kalala Assosa ambako aliungana na mwimbaji mkongwe Abubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’
Kama nilivyo kujuza kuwa historia ya Mwaole katika mzuziki haichoshi kuisikia au kuisoma, aliitwa kujiunga na bendi ya Super Kamanyola ya jijini Mwanza ‘Rocky City’.Huko nako alikutana na wakali wengine katika uimbaji akina Mukumbule Lolembo ‘Parash’ na Benno Villa Anthony.
Alipiga muziki na bendi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili baadae akarejea katika bendi yake ya Bana Maquis.Sauda Mwaole tayari amekwisha tengeneza album ambayo anasema bado ipo jikoni ikikolezwa viungo kabla ya kupakuliwa hivi karibuni.
Anazitaja nyimbo zilizo katika album hiyo kuwa ni ‘Penye penzi pana mengi’, ‘Penzi la ukweli’, ‘Shoka la bucha’, ‘Siyo kama nina wivu’, ‘Huyu ni chaguo langu’ na ‘Sitaki visa vyako’Mwaole alibahatika kupata watoto watatu, mmoja kati yao alitangulia mbeleza haki. Anawataja watoto walio hai kuwa ni Mariam Rashid na Kassim Farid.
,Kassim alimuelezea kuwa amefuata nyayo zake za kuimba nyimbo za muziki wa dansi, akitumia jina la kisanii la ‘Farid Lokuwa’
Kama mzazi, alitoa wito kwa vijana kufuata maadili mema na kutoiga utamaduni wa nje wa kuvaa nguo nusu uchi hadharani, kuvaa hereni na vipini kwa vijana wa kiume na mengine mengi ya kuudhi.
“Ni kujivunjia heshima mbele ya kadamnasi, aibu kubwa kwa jamii kwa kuwa ni kujidharirisha pasipo sababu” kwa masikitiko anatamka Sauda Mwaole.
Kwa upande wa muziki wa kizazi kipya Mwaole alisema muziki wao ungelikuwa mzuri zaidi kama baadhi yao wasingelikuwa wanatamka maneno ya matusi katika nyimbo zao.
Aliwasihi maproduza wenye studio za kurekodi miziki, kuzichuja nyimbo za wasanii hao pindi wanapobaini kwamba lugha iliyotumika katika nyimbo hizo haziendani na utamaduni wa Mtanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...