WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Haruzale, Kata ya Nyamihyolo, Mwibara, Wilayani Bunda, leo. Lugola alisema tabia ya baadhi ya polisi nchini wanaoshirikiana na mafisadi kudhulumu ardhi ya wananchi maskini, dawa yao imeiva, hatamuonea mtu huruma. 
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akiwaelekeza wananchi wa Kijiji cha Kabainja Kata ya Kasuguti, Mwibara, Wilayani Bunda, jinsi ya kujenga darasa lililoimara katika shule ya msingi Kabainja kijijini hapo, leo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. 
……………………… 
Na Felix Mwagara, Mwibara (MOHA) 
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema baadhi ya polisi wasiokuwa waaminifu nchini wanaoshirikiana na mafisadi kudhulumu ardhi ya wananchi maskini, sasa dawa yao imeiva. 
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Haruzale, Kata ya Nyamihyolo, Jimbo la Mwibara, Bunda akiwa katika ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo jimboni mwake, Lugola amesema amepokea malalamiko mengi ya ardhi katika jimbo lake na sehemu mbalimbali nchini. 

Amesema mafisadi wa ardhi hukimbilia kufungua kesi vituoni wakilazimisha kwa kutumia fedha ardhi iwe mali yao wakiwatumia polisi wasiokuwa waaminifu ili kufanikisha matwaka yao. 

“Haiwezekani tabia hii ikachekewachekewa na kuonekana ni kawaida, nimekemea sana katika mikutano yangu hapa Mwibara na sehemu zinginezo hapa nchini, nitahakikisha napambana na mafisadi pamoja na polisi hao wasiokuwa waaminifu,” alisema Lugola. 

Waziri Lugola alisema kila kukicha anapata malalamiko mengi kutoka sehemu mbalimbali nchini kuwa mafisadi wanaendelea kuwaonea wananchi maskini kwa kupora ardhi wakidai wao ndio wamiliki halali. Aliongeza kuwa, utumia polisi wasiokua waaminifu kuwakandamiza wananchi ambao hawana nguvu ya kifedha na kufanikiwa kudhulumu ardhi zao. 

“Dawa yao ilikuwa jikoni, sasa imeiva, siwezi mwangusha Mheshimwa Rais Dkt. John Magufuli, Serikali hii haichezewi hata siku moja, sasa nitawashughulikia ipasavyo,” alisema Lugola. 

Aidha, Lugola aliwataka wananchi wa Mwibara kuhifadhi vyakula vizuri ili kuepusha janga la njaa kwa hapo baadaye na kusababisha wananchi kuja kuteseka kwa ukosefu wa vyakula na kusababisha mateso katika familia. 
“Tutunzeni vyakula vyetu, msitumie hovyo, kuweni makini na matumizi ya vyakula, sitaki nije kuona mnateseka na njaa, hakikisheni mnatunza vyakula kwa ajili ya matumizi ya baadaye, ogopeni njaa kama ukoma,” alisema Lugola. 
Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo, alifanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo akikagua madarasa ya shule ya msingi pamoja na zahanati.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...