Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii.
MAHAKAMA ya Tanzania imeingia mkataba wa sh. Bilioni 4.2 na shirika la mawasiliano Tanzania TTCL kwa ajili ya kuunganisha mahakama zote nchini katika mkongo Wa Taifa ili kuziwezesha kupatikana haki kwa urahisi na haraka zaidi.
Imeelezwa kuwa, kuunganishwa kwa Ofisi za Mahakama nchi nzima katika Mtandao Mpana (WAN) kwa kutumia mkongo wa Taifa kutapunguza gharama za uendeshaji wa shughuli na kusaidia shahidi kuwasilisha ushahidi wake bila kulazimika kufika mahakamani.
Mkurugenzi wa Tehama wa Mahakama ya Tanzania Kelege Enock, ameeleza hayo leo Julai 29,2019 jijini Dar es Salaam, wakati wa utilianaji saini wa mkataba huo kati ya Mahakamani na TTCL.
Akizungumza kabla ya kutiliana saini, Enock amesema, huduma hiyo ya mtandao Itasaidia kurahisisha upatikanaji wa huduma za mahakama kwa kupitia mifumo, electroniki, kuwa na mazingira wezeshi ya kubadilishana taarifa kati ya Mahakama na taasisi wadau katika mfumo mzima wa utoaji haki nchini.
"aasisi wadau ni pamoja na Magereza, Polisi, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Chama Cha Mawakili (TLS),” alisema.
Aidha Kelege amesema, mkataba huo wenye lengo la kuunganisha majengo ya mahakama kuanzia Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya na baadhi ya Mahakama za Mwanzo zenye majengo ya kisasa kwa kuanzia jumla ya majengo 157 yatapata Huduma hiyo.
"Mahakama zitakazo ingizwa kwenye mtandao ni, Mahakama ya Rufani moja, Mahakama Kuu 16, Mahakama Kuu Maalumu (Specialized Divisions) nne, Mahakama za Mkoa 29, Mahakama za Wilaya 112, Mahakama za Mwanzo 10 hivyo kufanya jumla ya majengo ya Mahakama 157 kwa kuanzia,” amesema Enock.
Ameongeza kuwa, katika mkongo huo wa Taifa huduma za aina mbili zitapatikana ambazo ni mtandao wa ndani yaani ‘data’ pamoja na ‘Internet’ katika maeneo yote tajwa.
“Kwa kuzingatia unyeti na usalama wa shughuli za Mahakama huduma hii ya mtandao itawezeshwa na teknolojia ya “Virtual Private Network (VPN)” kupitia ‘‘Multiprotocol Labelling Switch (MPLS) ambapo jitihada za kuunganisha mahakama zilianza mwaka 2015 kwa kuwahusisha kikamilifu TTCL mpaka leo mafanikio yamepatikana" amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba amesema shirika lao limekuwa likiuza data katika kampuni zingine za mawasiliano kutokana na hilo wanawahakikishia mahakama kuwa wataifanya kazi hiyo na kuimaliza kwa wakati.
“Tunajivunia kuwa sehemu ya watu watakaowasaidia watanzania kupata haki kwa haraka hivyo tunaishukuru mahakama kwa kutuchagua kwani kutokana na miradi hii ndio inayowezesha kuwepo kwa gawio linalorudi serikalini,” alisema.
Aidha alisema watanzania wanapaswa kutumia vitu vya nyumbani kwani kwa kufanya hivyo faidi inabaki nchini na kwenda kutumika katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Hussein Kattanga na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Waziri Waziri Kindamba wakikabidhiana Mkataba huo mara baada ya kuusaini.
Picha ya pili Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Hussein Kattanga na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Waziri Waziri Kindamba wakikabidhiana Mkataba huo mara baada ya kuusaini.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Hussein Kattanga (katikati) na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Waziri Kindamba (wa pili kulia) wakionesha kwa furaha Mkataba huo mara baada ya kuusaini. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Bw. Mohamed Mtonga.
Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Mahakama ya Tanzania Bw. Kalege Enock akielezea kuhusu Mahakama kuingia kwenye Mkongo wa Taifa wakati wa Hafla ya kusainiwa kwa Mkataba kati ya Mahakama ya Tanzania na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) leo jijini Dar es salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...