Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv,
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi likiwemo shitaka la kuisababishia serikali hasara  inayowakabili vigogo wa Kampuni ya  Six Telecoms akiwemo Wakili Dk Ringo Tenga kukamilisha nyaraka wanazoziandaa katika kesi hiyo ili iweze kuanza kusikilizwa.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, amesema kwa sababu shauri hilo ni la uhujumu uchumi, mahakama hiyo haina meno ya kuisemea lakini ni vema upande wa mashitaka kukamilisha taratibu hizo mapema.

Hatua hiyo imekuja kufuatia upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa serikali Wankyo Simon kudai mahakamani hapo leo Julai 17, 2019 kuwa kwa sasa wanaandaa nyaraka muhimu katika kesi hiyo wakati kesi hiyo ilipokuja kwa kutajwa.

"Mheshimiwa hakimu, tupo katika hatua za kuandaa nyaraka mbalimbali ikiwemo vielelezo ambavyo ni muhimu katika kesi hii hivyo tunaomba mahakama iahirishe kesi hii kwa wiki mbili ili kukamilisha hatua hiyo.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 26, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Mbali na Tenga, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Peter Noni, Mkuu wa fedha wa kampuni hiyo na Noel Chacha.

Washtakiwa hao wanadai kuwa, kati ya Januari 1, 2014 na Januari 14,2016 maeneo ya Dar es Salaam, walitoza malipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa chini ya kiwango cha Dola za Marekani 0.25 kwa dakika kwa lengo la kujipatia faida.

Pia katika kipindi hicho, wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini(TCRA) kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa kiasi cha Dola za Marekani 3,282,741.12 kwa TCRA, kama malipo ya mapato.

Washtakiwa hao ,wanadaiwa katika kipindi hicho walishindwa kulipa ada za udhibiti za Dola za Marekani 466,010.07 kwa TCRA.

Katika shtaka la utakatishaji wa fedha, Hafidhi, Noni,Tenga na Chacha, wanadaiwa kuwa walitumia ama walisimamia Dola za Marekani 3,282,741.12 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu linalotokana na mashitaka yaliyotangulia.

Vile vile ,washitakiwa hao wanadaiwa kuwa waliisababishia TCRA hasara ya Dola za Marekani 3,748,751.22 (sawa na Sh bilioni nane.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...