Na Zainab Nyamka, Michuzi Tv
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe amemtembelea na kumuona mchezaji wa zamani wa timu ya mpira wa miguu ya Yanga na Taifa Stars Jellah Mtagwa anayeumwa kwa kipindi kirefu.
Dkt Mwakyembe amesikitishwa sana na hali aliyomkuta nayo mchezaji huyo aliyeipa mafanikio timu ya Taifa.
Akizungumza nae, Dkt Mwakyembe amesema wamepata taarifa kupitia vyombo vya habari na kutambua kuwa wao kama serikali na Shirikisho wana wajibu wa kufanya jambo kwa ajili ya mchezaji huyo.
Amesema, hali ya Mtagwa si nzuri kwani anaumwa, ana changamoto anapokaa kwani mazingira ya nyumba sio rafiki kutokana na hali yake ambapo anatakiwa kupelekwa hospitali kwa ajili ya mazoezi ya viungo (physiotherapy).
Dkt Mwakyembe amesema, pia hali ya maisha sio nzuri kwani kwa sasa hafanyi kazi yotote na imefikia hatua mama(mkewe) aache kazi kwa ajili ya kumuuguza.
"Kuna kila sababu Jellah Mtagwa kusaidiwa, nitakaa na Shirika la Posta kumsaidia kwani aliweza kulibeba kwa kuuza stamp zake kwa muda mrefu pamoja na TFF ambao aliweza kuuhudumia mpira kwa ngazi mbalimbali ikiwemo Timu ya Taifa,"amesema Dkt Mwakyembe.
Aidha, Ameeleza kuwa atafikisha pia suala hilo kwa viongozi wengine wa nchi kwa ajili ya msaada na atarejea tena kwa ajili ya kuwaona pamoja na kuwapa mrejesho kwani kwa sasa Mtagwa anahitaji dawa, anahitaji gari kwa ajili ya kumpeleka hospitali na kurudi na mahali anapokaa si pazuri.
Mtagwa akiongea, amemshukuru Waziri Mwakyembe kwa kwenda kumtembelea kwani hakuna kiongozi yoyote aliyewahi kuja kumtembelea toka aanze kuumwa.
Ameongezea kuwa, ana changamoto mbalimbali ila kikubwa ni makazi na usafiri ambavyo angeweza kuvipata angeshukuru sana.
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe akizunguma na mchezaji wa zamani Jellah Mtagwa baada ya kumtembelea na kumjulia hali yake nyumbani kwake akiugua kwa muda mrefu.
Mchezaji wa zamani Jellah Mtagwa akizungumzia kutembelewa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe na kumshukuru na kumuelezea changamoto anazokutana nazo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...