Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv.
WALIMU wa Shule za Sekondari nchini wameshauri wadhibiti wa ubora wa elimu kupokea nyaraka zilizoandaliwa kwa njia ya teknolojia badala ya zile zilizomo kwenye vitabu kwani ni rahisi kuchakaa.
Pia walimu hao, wameiomba serikali iwaruhusu wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi kutumia simu na vikokotoo wanapokuwa wanafundishwa na kwenye mitihani ili waweze kutunza kumbukumbu kwa muda mrefu bila ya kuchakaa.
Wakizungumza kwenye warsha iliyoandaliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Watu (HDIF) kupitia Taasisi ya Shule Direct katika maonesho ya Wanasayansi Chipukizi, iliyofanyika leo Julai 31, 2019, walisema sababu inayochangia wanafunzi wengi kutopenda masomo ya sayansi ni sera zilizopo ambazo zinakataza mwanafunzi kutumia kikokotoo awapo shuleni.
Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Azania, Thelesphory Sylvester amesema wanauwezo wa kupata huduma za teknolojia shuleni na pia huandaa nyaraka mbalimbali lakini wadhibiti ubora wa elimu wanapofanya mapitio huko mashuleni hutaka nyaraka zilizo kwenye makaratasi.
"Uwepo wa teknolojia lengo lake ni kurahisisha utendaji wa kazi hivyo wanapaswa kupewa elimu ya kutumia teknolojia ipasavyo na kuachana na matumizi ya makaratasi ambayo huweza kuharibika haraka.
Ameongeza kuwa, ili kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi ni lazima kuwepo mazingira mazuri ya masomo iiwemo upatikanaji wa teknolojia na kuruhusu matumizi ya simu na vikokotoo.
"Kwanini tuhamasishe matumizi ya teknolojia ya kompyuta wakati bado nyaraka zinazotakiwa ni za makaratasi..tunaomba muendelee kuwaelimisha wadhibiti kutumia teknolojia pia katika mapitio yao," amesema Mwalimu Sylvester.
Kwa upande wake, mwalimu, aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Mathias amesema teknolojia ni nzuri kutumika mashuleni kwani huwasaidia wanafunzi kujikumbushia masomo mbalimbali ikizingatiwa kuwa, kuna changamoto mbali mbali hasa katika masomo ya sayansi ambayo yana maneno magumu ambayo ili mwanafunzi aweze kuelewa anapaswa kueleweshwa kwa lugha rahisi.
"Tumekuwa tukiwakaririsha wanafunzi katika masomo ya sayansi lakini kama teknolojia ikitumika hadi mashuleni inaweza kuleta mapinduzi kwa mwanafunzi kupata picha halisi ya kile anachojifunza", amesema.
Naye, Mtengeneza Tovuti kutoka Shule Direct , Rajabu Mgeni amewaeleza walimu kuwa wanayo fursa ya kuwasaidia wanafunzi wao kwa kuandaa masomo kwa kuyatuma kwenye mtandao ambapo wao kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) wamekuwa wakipitia masomo mbalimbali yanayoandaliwa na walimu nchini kwa ajili ya kutumika na wanafunzi.
Amesema, taasisi yao inatoa mafunzo kidigitali kwa kufuata kanuni za maendeleo ya kidijiti na kwamba mwalimu anahitaji kusaidia idadi kubwa ya wanafunzi hivyo wanapaswa watumie mfumo huo kwani una uwezo wa kufikia walimu na wanafunzi zaidi ya M 1.5
Aidha amezitaja kanuni za maendeleo ya kidijiti kuwa ni kuelewa mfumo wa ekolojia uliopo, kuandaa pamoja na mtumiaji, kushirikiana, ubunifu unaolenga ukuaji, kusukumwa na takwimu, usiri na usalama.
Kamati ya Maandalizi ya Wanasayansi Chipukizi wakijiandaa kufanya maonesho ya bunifu mbalimbali zilizofanywa na wanafunzi katika warsha iliyoandaliwa na Mfuko wa maendeleo ya Watu (HDIF) kupitia Taasisi ya Shule Direct jijini Dar es Salaa
Wanafunzi kutoka mikoa mbalimbali wa shule za sekondari nchini wakiwa kwenye maonesho ya Wanasayansi Chipukizi yaliyofanyika leo Julai 31,2019 jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko wa Maendeleo ya Watu (HDIF) Joseph Manirakiza akipiga picha moja ya machapisho yaliyowasilishwa na Wanasayansi Chipukizi leo katika warsha iliyoandaliwa na Mfuko wa maendeleo ya Watu (HDIF) kupitia Taasisi ya Shule Direct jijini Dar es Salaam.
Wanafunzi walioshiriki maonesho ya Wanasayansi Chipukizi wakitoa maelekezo juu ya bunifu zao kwa mkurugenzi wa HDIF Joseph Manirakiza na pembeni yao ni Mtaalamu wa Mawasiliano wa HDIF Hannah Mwandoloma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...