Na Moshy Kiyungi
Nyboma Mwan'dido ni nguli katika muziki alianza kufaidi matunda ya jasho lake akiwa na umri wa miaka 18, kupitia tungo na sauti yake nyororo katika uimbaji.
Amepiga muziki katika bendi nyingi akishirikiana na wanamuziki wakubwa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Tungo na sauti ya mwanamuziki huyo, haijachuja tangu akiwa kinda. Sauti yake inayoweza kulinganishwa na ya ndege aitwaye Churiku.
Mfano mdogo sauti yake imesikika akiimbisha wimbo wa Abisina, wakati akiwa katika bendi ya Orchestra Kamale, huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mwan’dido anazo talanta nyingi za utengenezaji muziki, utunzi na uimbaji wa nyimbo za muziki wa Soukous.
Alizaliwa nchini humo, na kujifunza kuiimba akiwa bado mdogo wakati huo akiwa kijiji cha Nioki, kilicho umbali wa kilometa 200, Kaskazini Mashariki mwa jiji la Kinshasa, DRC.
Alipokuwa mwanafunzi wa shule, alijiunga na kwaya ya shule pamoja na ya Kanisa.
Baada ya wazazi wake kuhamia katika jiji la Kinshasa, wakati yeye akiwa bado mwanafunzi ya shule ya msingi, alijiunga katika bendi yake ya kwanza ya Baby National, kama mwimbaji wa kulipwa mwaka 1969, wakati huo akiwa na umri wa miaka 18.
Baadaye Nyiboma alikwenda kujiunga katika bendi ya Negro Success. Alipiga muziki na bendi hiyo hadi pale kiongozi wao Bavon Marie-Marie Siongo alipofariki kwa ajali ya gari.
Bavon alikuwa mdogo wake Franco Makiadi, alifariki dunia Agosti 05, 1970, baada ya gari alilokuwa akiliendesha kupata ajali.
Ajali hiyo ilitokana na wivu wa kimapenzi baada ya kutokea mzozo kati yake na kaka yake Franco Luambo Makiadi, akimtuhumu kwamba alikuwa anafanya mapenzi na rafiki yake wa kike aliyejulikana kwa jina la Lucy.
Mwan’dido aliingia mkataba na kampuni ya kurekodi ya Editions Veve, iliyokuwa ikimilikiwa na Kiamuangana Mateta Wazelambongo ‘Verckys’.
Verckys alikuwa mahiri kwa kurekodi muziki wa soukous, producer, mfadhili, mtunzi, mpulizaji wa saxophoni pia alikuwa kiongozi wa bendi yake ya Orchestra Veve katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Zaire wakati huo)
Mwaka 1975 Nyboma Mwan’dido aliteuliwa kuwa kiongozi wa bendi ya Orchestra Kamale, iliyokuwa chini ya Editions Veve record label.
Kamale iliundwa na Verckys akiwatumia baadhi ya wanachama wa bendi ya Orchestra Lipua Lipua na Orchestra Kiam ambazo zilikuwa miongoni mwa bendi zilizoasisiwa chini ya lebo ya Veve, ya Verckys.
Bendi ya Kamale ilikuwa na watunzi na waimbaji mahiri akiwemo yaye Nyboma na Tshimanga Kalala Assosa, ambaye yupo nchini Tanzania, tangu miaka ya 1980, alipokuja na bendi ya Orchestra Fuka Fuka.
Hivi sasa Asossa ni kiongozi wa bendi ya Orchestra Bana Maquis ya jijini Dar es Salaam.
Wakati huo bendi ya Orchestra Kamale, walitoka na nyimbo kali zilizowakuna wapenzi na mashabiki wa muziki wa soukuos. Miongoni mwa nyimbo hizo ni Ngali, Masua, Andoya, Abisina, Bitota na nyingine nyingi.
Orchestra Kamale ilisambataika mwaka 1978, baada ya Tshimanga Kalala Assosa na Mulembu, walipoondoka kwenda kuunda bendi yao ya Fuka Fuka.
Baadhi ya wanamuziki wa bendi ya Orchestra Kamale waliobakia, wakabadili majina ya bendi ikaitwa Les Kamale, ikiiongozwa na Nyboma Mwanan’dido.
Miaka ya 1970, Les Kamale, ilikuwa maarufu kwa nyimbo kali za "Salanga" na "Afida na ngai."
Mwaka 1979 Nyboma alikwenda kufanya kazi ya muziki katika kundi ka African All-Stars nchini Togo, baada ya mwanzilishi wa kundi hilo Sam Mangwana kuondoka.
Ilipotimu mwaka 1981, Nyboma alirekodi albam moja kali ya ‘Double Double’, akiwa katika bendi yake mpya ya Les Kamale Dynamiques Du Zaire.
Aidha mwaka 1983 hadi 1984, alirekodi albam nyingine tatu chini ya jina la Les Kamale Dynamiques Du Zaire.
Nyboma aliwahi kufanya kazi za muziki na wanamuziki wakubwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akina Pepe Kalle akiwa na bendi yake ya Empire Bakuba, Koffi Olomide akiwa na wanamuziki wake wa Les Quatre Latin, Etoiles, Bopol, Syran na Wuta Mayi.
Albam nyingi za Nyiboma Man’dido aliwashirikisha wanamuziki nguli wakiwemo akina Pepe Kalle, Madilu Systeme, Kamale, Lokassa Ya Mbongo na wengine wengi.
Aidha Pepe Kalle alimshirikisha Nyiboma Man’dido katika wimbo albamu ya Moyibi 1988.
Aidha aliimba nyimbo za Lipwa Lipwa De Nyimboma na Stop Feu Rouge.
Baadhi ya albam alizotunga ama kushiriki kuimba alipokuwa katika bendi ni kama ya L’Orchestre Kamale iliyotoka mwaka 1977, Innovation vol. 6 na 7 alimshirikisha Bovi mwaka 1980.
Zingine ni Dede ambapo Nyboma, alimuita Lesale wakashirikiana kutengeneza wimbo. Mwaka 1982, akimshirikisha tena Pepe Kalle katika nyimbo za Lesale ya 1983 na Coeur a Coeur.
Nyimboma alishirikiana vyema na Pepe Kalle kwenye albam za Moyibi mwaka 1988, Anicet ya mwaka 1994 na Bandona.
Nyiboma Man’dido bado anendelea na shughuli za muziki akiwa nchini Uingereza ambako ndiko ameweka makazi yake.
Muandaaji wa makala hii anapatikana kwa namba: 0713331200, 0784331200, 0736331200 na 0767331200.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...