* Wadau waguswa wachanga shilingi milioni 23 kusaidia upasuaji wa moyo kwa watoto hao

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

KATIKA kutimiza ahadi aliyoitoa mwezi Juni mwaka huu kwa kuchangia gharama  za upasuaji kwa  watoto 60 waliotoka kwenye familia duni  Mkuu  wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda leo Juni 25  amepokea zaidi ya Shilingi Milioni 23 kutoka kwa wadau ambao wameguswa na kampeni aliyoanzisha ya ufadhili wa matibabu ya upasuaji moyo kwa watoto 60 kutoka familia zenye hali duni.

Miongoni mwa Wadau waliomuunga Mkono  Makonda ni Mbunge wa Kibaha Mjini Sylvester Koka ambaye amekabidhi hundi ya Shilingi milioni 10 kwaajili ya matibabu ya watoto 5 huku Mkurugenzi wa Dorka Catering Dorothy Kansolele akichangia milioni 6 na  Mkurugenzi wa kampuni ya Abe Professional Sound  Abraham Ngomko akichangia Milioni 6 kwaajili ya matibabu ya watoto 3.

Baada ya kupokea fedha hizo RC Makonda amezikabidhi kwa uongozi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na kueleza kuwa zitasaidia kugharamia zaidi ya Watoto10 kwenye upasuaji wa awamu ya pili.

Makonda amewashukuru wadau wote wanaondelea kumuunga mkono kwenye kampeni hiyo inayolenga kuokoa maisha ya watoto ambao wangeweza kupoteza maisha kutokana na wazazi wao kushindwa kumudu gharama za matibabu.

Wadau waliokabidhi fedha hizo wameeleza kuwa wataendelea kuunga mkono zoezi hilo kwa kuongeza fedha nyingine kwakuwa wanaamini kampeni aliyoanzisha  Mkuu wa Mkoa ni njema na inapaswa kuungwa mkono na wadau mbalimbali ili kuokoa maisha ya watoto.

Ikumbukwe kuwa mapema mwezi Juni mwaka huu  RC Makonda aliahadi kufadhili matibabu ya upasuaji wa moyo kwa watoto 60 kwa muda wa miezi sita ambapo kila mwezi watatibiwa watoto10 na hadi sasa tayari amefanikisha matibabu ya watoto 30 kati ya 60.

Awali akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete Profesa Mohamed Janabi amemshukuru RC Makonda kwa kuwaangalia kwa jicho la pekee watoto hao waliokuwa wanahitaji kufanyiwa upasuaji lakini serikali ilielemewa na gharama

Janabi amesema kuwa takribani watoto 512 wanatakiwa kufanyiwa upasuaji na amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza ili kuwasaidia na kuokoa maisha ya watoto hao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...