Moureen Rogath, Michuzi TV, Buhigwe.
Wadau mbalimbali wa elimu nchini wametakiwa kujitokeza kuwekeza kwenye elimu kwa mtoto wa kike kwa lengo la kuinua na kuongeza ufaulu wa wasichana ukilinganisha na ufaulu wa mtoto wa kiume ambao umekuwa mkubwa.
Hayo yamebainishwa na mratibu wa Equip wilaya ya Buhigwe Bi. Noel Kasaya, wakati alipotembelea katika shule ya msingi Nyarugano iliyopo kata ya Kibwiga, kukagua miradi iliyotekelezwa na Mpango wa Kuinua Elimu ya Msingi(Equip).
Bi. Kasaya alisema wanafunzi wa kike wana haki sawa ya kupata elimu bora kama mtoto wa kiume.
Alisema wadau wanamchango mkubwa katika kuinua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi ambapo kwa sasa wanafunzi wamekuwa na ufaulu mdogo kuliko watoto wa kiume hasa katika mkoa wa Kigoma.
Mwalimu mkuu wa shule ya Nyarugano Bw. Elias Boaz, alisema walipokea fedha kutoka Equip kiasi cha sh 550,000 kwa awamu mbili na kuanzisha mradi wa shamba la kulima ndizi pamoja na kununua sola ya kusomea wanafunzi hasa nyakati za jioni.
“Lengo la fedha hizi ni kuiwezesha shule kujitegemea kwa mahitaji yake na si kila kitu kutegemea kutoka serikalini. Hapa shuleni kwetu hatuna umeme tukaamua kununua sola kwa ajili ya kusomea wanafunzi wa maeneo ya karibu na shule nyakati za jioni,” alisema,
Awali kabla ya kununua sola na kuweka taa kwaajili ya wanafunzi kujisomea hali ya ufaulu ilikuwa kwa asilimia 39 kwa darasa la saba lakini kwasasa baada ya wanafunzi kuanza kujisomea ufaulu umepanda kwa asilimia zaidi ya 55 huku watoto wa kike wakiwa wanashika namba moja.
Bw. Sosthenes Katunzi mwalimu wa shule hiyo ambaye alipewa mafunzo ya mbinu za kufundishia na Equip kwa ajili ya kwenda kufundisha waalimu wenzake wa madarasa ya awali pamoja na madarasa ya juu alisema kwamba mafunzo aliyoyapata ni kwa ajili ya mbinu za kufundishia wanafunzi wa madarasa ya awali, na kwa kuwa hawawezi kuchukua waalimu wote mimi ni mwakilishi wao ambapo nakuja kufundisha waalimu wenzangu,”alisema Katunzi.
Mwanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo Leonia Samwel, alisema wamekuwa na klabu ya juu kwaajili ya kufundishwa usawa wa kijinsia, ambapo umeweza kumsaidia kwa kujua haki zake kama mtoto wa kike awapo darasani.
“Katika klabu yetu nimejifunza usawa wa kijinsia kati yangu na mwanafunzi wa kiume zamani nilikuwa siwezi kumfata na kumuuliza swali lakini kwasasa naweza kukaa naye na kusoma naye bila kuogopa tofauti na awali,”alisema Samweli.
Waalimu pamoja na wazazi wakiwa katika shamba la shule la migomba ya ndizi ambalo lengo lake ni kusaidia wanafunzi wa shule ya msingi Nyarugano iliyopo kata ya Kibwiga wilayani Buhigwe mkoani hapa,na kujitegemea ambapo walipokea kiasi cha Sh. 550 , 000 Kwa Mpango wa Kuinua Elimu ya Msingi (Equip).
Sehemu ya shamba la shule la migomba ya ndizi la kusaidia wanafunzi wa shule ya msingi Nyarugano iliyopo kata ya Kibwiga wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...