Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
MKUU wa Kitengo cha Mauzo cha Ramada Hoteli, William Mgatta (36) wenzake wawili,   wamefikishwa katika  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka matatu likiwemo shtaka la kujifanya maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kushawishi rushwa ya Sh milioni 300.

Mbali na Mgatta washitakiwa wengine ni wafanyabiashara Mohammed Abdallah (25) na Daniel Ileme (35) ambao wote kwa pamoja  wamesomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Agustina Mmbando.

Hati ya mashtaka imesomwa na Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Aneth Mavika  imedai kati ya Mei Mosi na  Juni 10, mwaka huu, katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam na Arusha, mshitakiwa Abdallah na Ileme wakiwa wafanyabiashara na mshitakiwa Mgatta akiwa Mkuu wa Kitengo cha mauzo cha Ramada hoteli walishawishi rushwa ya Sh milioni 300.

Amedai kuwa, alishawishi rushwa hiyo kutoka kwa Francis Matunda kama kishawishi ili wasimchukulie hatua za kisheria kwa kukataa kuwalipa wafanyakazi wake kiasi cha Sh bilioni moja wanayomdai.

Imeendelea kudaiwa kuwa katika tarehe tofauti katika eneo lisilotambulika jijini Dar es Salaam na Arusha washitakiwa Abdallah, Ileme na Mgatta walikula njama ya kutenda kosa la kujifanya ni watumishi wa umma.

Wakili Mavika ameendelea kudai kuwa, katika shtaka la tatu, imedaiwa, Juni 10, mwaka huu katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam na Arusha washtakiwa kwa pamoja  walijifanya ni watumishi wa Takukuru kitu ambacho walijua kuwa si kweli.

Hata hivyo, upande wa mashtaka umedai kuwa, upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na hawana pingamizi la dhamana endapo washitakiwa watatimiza masharti.

Akiwasomea masharti ya dhamana, Hakimu Mmbando amemtaka kila mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika wenye barua halali na vitambulisho ambao pia wametakiwa kuwalisilisha mahakamani hapo fedha taslimu Sh milioni 50 au hati ya mali isiyohamishika  yenye thamani ya fedha hiyo na kusaini bodi ya Sh milioni 50.

Washitakiwa wameshindwa kutimiza masharti hayo na wamerudishwa rumande. kesi imeahirishwa hadi Julai 30, mwaka huu kwa kutajwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...