Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
WATU watatu wakazi wa Jijini Dar es Salaam wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi likiwemo shtaka la kuiba madini  yenye thamani ya Sh 507,347,000.

Akisoma hati ya mashtaka, wakili wa Serikali, Jacqueline Nyantori amewataja washtakiwa hao kuwa ni, Donald Njonjo (30) Mkazi wa Kigamboni, Gamba Muyemba (51) Mkazi wa Tandika na Kashif Mohamed (41) Mkazi wa Upanga jijini Dar es Salaam.

 Mbele ya Hakimu Mwandamizi Mfawidhi, Kelvin Mhina imedaiwa kuwa kati ya Novemba 30, 2017 na Juni 29, mwaka huu katika Ofisi ya Tume ya Madini iliyopo Masaki wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam washtakiwa waliiba madini ya dhahabu yenye uzito wa Kilogramu 6.244 yenye thamani ya Sh 507,347,000 mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Imeendelea kudaiwa kuwa, Julai 8, mwaka huu katika Mtaa wa Indiragandhi wilayani Ilala jijini Dar es Salaam mshtakiwa Mohamed alikutwa na madini ya dhahabu yenye uzito wa gramu 2794.5 ya Dola za Marekani 121,155.45 sawa na Sh 278,714,478.06 mali ambayo imeibiwa kwenye Tume ya Madini.

Katika shtaka la tatu imedaiwa kati ya Julai Mosi, 2018 na Novemba 31, mwaka jana katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Ilala, washitakiwa kwa pamoja waliuza madini ya dhahabu yenye uzito wa Kilogramu 6.244 ya thamani ya Sh 507,347,000 bila kuwa na kibali.

Pia inadaiwa, kati ya Julai Mosi, 2018 na Novemba 31, 2018 katika maeneo mbalimbali washtakiwa hao walijihusisha moja kwa moja na muamala unaohusu madini hayo ya dhahabu wakati wakijua kuwa dhahabu hiyo imetokana  na kosa tangulizi la wizi.

Hata hivyo, washitakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakani hapo kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 29, mwaka huu kwa kutajwa na washitakiwa wamerudishwa rumande kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ama kuwapatia dhamana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...