NA MWANDISHI MAALUM - ORCI
Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), imepanga kuwachunguza virusi vya homa ya ini watu wapatao 1,000 ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani.
ORCI imetenga siku tano kuanzia Julai 27 (jana) hadi kufikia Julai 31, mwaka huu ambapo uchunguzi utafanyika bila malipo.
Hayo yameelezwa leo hospitalini hapo na Mkurugenzi wa Idara ya Kinga na Huduma za Saratani ORCI, Crispin Kahesa alipozungumza na waandishi wa habari.
"Kwa siku ambazo si za maadhimisho huwa tunatoza kiasi cha Sh. 10,000 kuchunguza, tumefanya bila malipo ili kuenda sambamba na na kauli mbiu ya mwaka huu isemayo 'Finding the Missing millions' (Wekeza kwenye mapambano dhidi ya homa ya ini," amesema.
Dk. Kahesa amesema kwa siku ya jana na leo tayari watu zaidi ya 150 wamejitokeza kuchunguzwa iwapo wana maambukizi ya virusi hivyo au la!
"Kwa upande wa watu wazima umekuwa mkubwa kwa kundi la wanawake kuliko wanaume na kwa kundi la vijana uwiano umekuwa sawa huku ikielezwa kwamba wengi waliojitokeza ni wale waliozaliwa kuanzia 1990 na kuendelea," amesema.
Dk. Kahesa ambaye pia ni bingwa wa Kinga ya magonjwa ya saratani ORCI amesema kati ya watu hao zaidi ya 150 waliojitokeza sita walikutwa wana maambukizi.
Dr. Kahesa amesema sambamba na utoaji hudumu ya uchunguzi na chanjo ya Homa ya ini unaoendelea kutolewa katika taasisi ya Ocean road huduma hii pia inatolewa Kwa watumishi katika maeneo yao ya kazi ikiratibiwa Na ORCI kwa maombi maalumu.
Amesema kwa namna ambavyo jamii imepata mwamko kuhusu umuhimu wa kuchunguzwa iwapo wana maambukizi ya ugonjwa, wapo baadhi ya wazazi ambao waliambatana na watoto wao ili nao wachunguzwe.
"Wamekuja na watoto wa umri wa mwaka mmoja, miwili wakiomba nao wachunguzwe, hawakuwa na uelewa kwamba watoto waliozaliwa kuanzia 2002 hadi sasa tayari walishapatiwa chanjo dhidi ya ugonjwa huu.
"Hivyo, pamoja na kufanya uchunguzi tumetoa pia elimu, kwamba wanaostahili kuchunguzwa ni wale ambao walizaliwa kuanzia 2002 kurudi miaka ya nyuma," amesema.
Amewasihi watanzania kuzitumia vema siku zilizobakia kwa kuhakikisha wanajitokeza kuchunguzwa afya zao.
"Hadi kufikia Julai 31, mwaka huu tunakusudia kuwachunguza watu 1,000, ikiwa mtu anakutwa hana maambukizi atahitajika kupata chanjo tatu kukingwa.
"Kupata chanjo atachangia gharama kiasi cha Sh. 10,000, chanjo ya pili atarudi baada ya mwezi mmoja na ya tatu ni baada ya miezi sita," amesema.
Mkurugenzi wa Idara ya Kinga na Huduma za Saratani ORCI, Crispin Kahesa
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...