Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) Kanda ya Mashariki umewashukuru wakazi wa jiji la Dar es Salaam na maeneo ya jirani kwa namna walivyojitokeza kuchangiaji damu kwa ajili kuwasaidia wagonjwa wenye uhitaji ikiwemo majeruhi wa ajali ya moto iliyosababishwa na lori la mafuta lililopinduka na kulipuka eneo la Msamvu Mkoani Morogoro ambapo watu zaidi ya 90 wameripotiwa kufariki dunia na wengine kujeruhiwa.

Sambamba na shukrani hizo Mpango huo umeendelea kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kuchangia damu huku ukiwahimiza kuendelea kuchangia damu zaidi ili kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji wa damu waliopo kwenye vituo mbalimbali vya afya hapa nchini.

Akizungumza wakati wa hitimisho la zoezi la uchangiaji damu lililofanyika kwa siku tatu mfululizo kwenye viunga vya stendi ya mabasi ya Mbagala jijini Dar es Salaam ili kusaidia majeruhi hao, Muhamasishaji Jamii kutoka NBTS, Bi Mariamu Juma alisema shukrani hizo zinafuatia mafanikio makubwa yaliyopatikana wakati wa zoezi hilo muhimu lililoandaliwa na NBTS kwa kushirikiana na benki ya Exim Tanzania.

“Kwa kweli muitikio ulikuwa wa kuridhisha na tumefanikiwa kukusanya chupa takribani 155 kulingana na malengo yetu hivyo tunawashukuru sana wakazi wa Mbagala na vile vile tunawashukuru sana Benki ya Exim Tanzania ambao ni washirika wetu wakubwa kwa kujitoa kwao kwa hali na mali hadi kufanikisha zoezi hili pamoja na wakazi wa Dar es Salaam kwa ujumla wanaoendelea kuchangia damu kwenye vituo vingine ikiwemo ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili.’’ Alisema.

Tangu kutokea kwa ajali hiyo ya moto mkoani Morogoro imeshuhudiwa idadi kubwa ya wakazi wa Dar es Salaam na kwinginepo nchini wakiguswa na kuitikia wito wa kuchangia damu kwa majeruhi hao ambapo imearifiwa kuwa bado kuna uhitaji wa damu huku jamii ikiendelea kuhamasishwa kujitolea zaidi ili kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji.

“Watanzania wasisubiri kuuguliwa na ndugu ndio wakumbuke kuchangia damu na mazao ya damu wanatakiwa kuwa na tabia ya kuchangia damu mara kwa mara ili itumike kuwatibu wagonjwa na si tu majeruhi wa ajali bali pia kuna makundi mengine yenye uhitaji mkubwa wa damu ambayo ni pamoja na wagonjwa wa saratani, watoto, kina mama wajawazito na wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji’’ alisema.
Baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam waliojitokeza kwenye viunga vya Stendi ya mabasi ya Mbagala jijini Dar es Salaam wakifuata taratibu ili kuchangia damu kwa ajili ya majeruhi wa ajali ya moto iliyosababishwa na lori la mafuta lililopinduka na kulipuka eneo la Msamvu Mkoani Morogoro ambapo watu zaidi ya 70 walifariki dunia na wengine kujeruhiwa. Zoezi hilo la siku tatu lilikamilika mwishoni mwa wiki, kwa uratibu wa benki ya Exim Tanzania kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...