Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

MAJERUHI 32 kati ya 47 wa ajali ya moto iliyotokea Agosti 10 mwaka huu Mkoani Morogoro wamefariki dunia hadi kufikia asubuhi ya leo, huku wagonjwa waliobaki hospitalini hapo ni 15 ambapo wagonjwa13 wapo chumba cha wagonjwa mahututi na wawili ambao ni wanawake wapo wodi ya kawaida (Sewahaji.)

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkuu wa kitengo Cha mawasiliano ya umma wa hospitali ya taifa Muhimbili Aminiel Aligaesha amesema kuwa kumekuwa na maswali mengi katika mitandao ya kijamii kuhusiana na hali za wagonjwa hao hasa kutokana na namna wanavyopoteza maisha licha ya kupelekwa katika hospitali hiyo.

"Janga hili limegusa jamii na taarifa tunatoa kila asubuhi ili jamii isiseme tunaficha, na tunapenda kuwataarifu watanzania kuwa serikali kwa kushirikiana na hospitali ya taifa Muhimbili imetumia fedha, utaalamu, ujuzi na rasilimali katika kuokoa maisha ya wenzetu 32 waliopoteza maisha, na hatuangalii mtu ameungua kiasi gani huduma zote zitatolewa bila kuangalia ni kiasi gani ameungua" ameeleza Aligaesha.

Daktari bingwa wa upasuaji kutoka hospitali ya taifa Muhimbili Dkt. Edwin Mrema amesema kuwa katika ajali ya moto kitu cha kwanza kinachoangaliwa ni kuzuia moto usitokee na kuleta madhara zaidi.

"Lazima jamii ifahamu kuhusiana na kuungua moto, katika janga hili wengi wameathirika katika mfumo wa upumuaji, figo na kupata vidonda katika asilimia kubwa ya mwili hali inayopelekea kuathirika kwa urahisi vijidudu kutokana na ngozi yao kuwa wazi, na wagonjwa wetu waliungua katika mazingira ya wazi hivyo wakaanza kuathirika palepale na walipoteza maji kwa kiasi kikubwa na chembembe nyingine za protein na chumvi" ameeleza. 

Amesema kuwa majeruhi hao wameungua kwa asilimia kubwa na wana uhitaji mkubwa wa tiba zaidi."Majeruhi waliungua moto katika eneo la wazi na kuathirika kwa kuunguza ngozi na kibaya zaidi kuvuta moshi wa kemikali iliyowafanya kuwa katika hali hatarishi" ameongeza.

Pia daktari bingwa wa magonjwa ya upasuaji Laurean Rwanyuma amesema kuwa wagonjwa wengi walioletwa katika hospitalini hapo walikuja wakiwa wameungua kati ya asilimia 70 hadi 100 na kuathirika sana katika mfumo wa upumuaji kutokana na moshi waliovuta.

Amesema kuwa wanajitahidi kupambana kuokoa maisha ya wagonjwa hao kwa kuhakikisha hawapati baridi, wanapata dripu za maji pamoja na dawa za kupunguza maumivu."Wagonjwa wengi wameathirika kwenye mapafu na wapo kwenye mashine ya oksijeni kwa kuwa hata ubongo unahitaji pia" ameeleza Rwenyuma.

Amesema kuwa serikali kwa kushirikiana na wafanyakazi wanapambana kuokoa maisha ya wagonjwa hao hasa kuwakinga wasishambuliwe na wadudu na wanaendelea kupambana kuokoa maisha yao.

"Kuna wengine wameungua kwa asilimia 80 bado tunapambana Ila kuna wengine waliungua chini ya asilimia 50 pia wapo hospitalini hapo na wanaendelea kupata tiba.

Kuhusiana na tetesi za uhaba na kuwepo wa uhaba wa wataalamu na vifaa tiba hospitalini hapo hali inayopelekea wagonjwa wengi kupoteza maisha Daktari Rwanyuma amesema kuwa wataalamu na vifaa vipo lakini tatizo kubwa lililojitokeza ni wagonjwa kuungua kwa asilimia kubwa na wengine kuungua kwa asilimia 100.
Daktari bingwa wa upasuaji  katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,Laurean Rwanyuma (katikati) akizungumza na waandishi wa habari   leo kuhusu vifo na hali za majeruhi wa janga la moto lilitokea Agosti 10 Mkoani Morogoro, baada ya Lori la mafuta kulipuka,ambapo amesema majeruhi 32 kati ya 47 wa ajali hiyo wamefariki Dunia hadi kufikia asubuhi ya leo Agosti 21,2019. Majeruhi wengine 15 wanaendelea kupatiwa matibabu na kati ya hao 13 wamelazwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU). Kulia ni daktari bingwa wa upasuaji Edwin Mrema na kushoto ni Ofisa uhusiano na mawasiliano kwa umma wa hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...