Na Woinde Shizza Michuzi Tv,Arusha

MKURUGENZI wa Hoteli ya Kitalii Impala na Naura za jijini Arusha Randy Mrema na msaidizi wake wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha kwa kosa kuwanyanyasa na kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi wake wapatao 180 katika kipindi cha miezi mitatu mfululizo.

Mrema na msaidizi wake Joram Lemanya walikamatwa mchana wa leo baada ya kuitwa na maofisa wa idara ya kazi ofisini na baadae kukamatwa na kufikishwa katika kituo cha Polisi jijini hapa wanakoshikiliwa hadi sasa.

Kabla ya kutiwa nguvuni kwa Mkurugenzi huyo maofisa wa Idara ya kazi pamoja na maofisa wa Uhamiaji walivamia hotel ya Impala na kuwaweka chini ya ulinzi wafanyakazi wawili ambao ni raia wa Kenya wanaodaiwa kufanyakazi kinyume na taratibu za nchi katika hotel ya Naura na Impala.

Akizungumzia tukio hilo Ofisa Idara ya Kazi mkoani hapa Wilfred Mdumi alithibitisha kushikiliwa kwa Mkurugenzi huyo kwa madai ya kukiuka makubaliano ya kulipa mishahara ya wafanyakazi wake katika kipindi cha miezi mitatu, Mei Juni na Julai kiasi kinachofikia zaidi ya Sh.milioni 120.

Amesema Mkurugenzi huyo amekuwa akiahidi kupitia vikao mbalimbali kuhusiana na madai hayo kikiwemo kikao na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Gabriel Daqqar lakini wameshindwa kutekeleza ahadi wanazozitoa huku wafanyakazi wakiendelea kuteseka kwa kukosa mshahara.

Ameongeza amelazimika kuchukua hatua hiyo ya kisheria ili wafanyakazi hao waweze kupata haki yao na wanatarajia kumfikisha mahakamani baada ya jalada kurejea kutoka kwa mwanasheria wa Serikali.

Kwa mujibu wa Mdumi Mkurugenzi huyo anadai changamoto za kibiashara zinazotokana na mgogoro wa kifamilia zinapelekea kuhujumiana kibiashara jambo linalosababisha kukosa wateja katika hoteli ya Impala na Naura na kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi.

Baadhi ya wafanyakazi hao wamedai kunyanyaswa na kudharauliwa na Mkurugenzi huyo na wala hataki mawasiliano yoyote juu yao jambo lililowalazimu kuandika barua za malalamiko kwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha na ofisi ya idara ya kazi kutaka kujua hatima ya madai ya mishahara yao ya miezi mitatu.

Wafanyakazi hao wameenda mbali zaidi kwa kudai Mkurugenzi wao amekuwa na matumizi mabaya ya fedha ambapo amekuwa akiendekeza kununua viwanja ,nyumba na kufungua hoteli yake binafsi na kushindwa kuwajali wafanyakazi wake wanaomwingizia kipato.

Wafanyakazi hao wamemwomba Waziri mwenye dhamana kuwasaidia ili kuweza kulipwa madai yao ya mishahara kwani kwa muda mrefu wanateseka na kushindwa kutunza familia zao na wengine kufukuzwa kwenye nyumba walizopanga.

Kabla ya tukio hilo Randy na Joram hivi karibuni walikamatwa na askari wa kikosi maalumu cha kuzuia dawa za kulevya wakihusishwa na biashara haramu ya dawa za kulevya na kusafirishwa kwenda jijini Dar es salaam chini ya ulinzi mkali walikoshikiliwa kwa wiki moja kabla ya kuachiwa kwa dhamana.

Hotel hiyo ya Impala ,Naura na Ngurdoto ni Mali ya baba yao Marehemu Bilionea,Melau Mrema aliyefariki mwaka 2017 nchini Afrika Kusini alikokuwa amelazwa ,ambapo marehemu aliacha wosia kuwa mali zote zisimamiwe na mtoto wake mkubwa Joan Mrema.

Marehemu Mrema aliyekuwa na wake zaidi ya wanne ,Mama yake na Randy aliungana na dada yake na marehemu Mrema(Shangazi) na kuamua kukimbilia mahakamani kumpinga Joani na kufanikiwa kumpindua .

Hata hivyo uamuzi wa Mahakama ulimpa mamlaka Randy kuwa msimamizi na Mkurugenzi mpya wa hotel ya Impala na Naura huku Joan akiachiwa hotel ya Ngurdoto na baadhi ya miradi mingine yakiwemo magari ya kusafirisha watalii.

Hata hivyo Joan ameonesha uwezo mkubwa wa kusimamia mali za marehemu baba yake na kufanikisha kuwalipa mishahara wafanyakazi wa Ngurdoto kwa wakati huku akifungua miradi mingine ikiwemo kuanzisha ofisi mpya ya utalii.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...