*Asema waafrika tulichelewa sana, sasa tunatakiwa kukimbia wakati wenzetu wakitembea.

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

RAIS Dkt.John Joseph Magufuli leo Agosti 5 amezindua rasmi wiki ya maonesho ya viwanda ikiwa ni katika kuelekea mkutano mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo wa nchi za Kusini mwa Afrika unaotarajiwa kufanyika nchini na kuwakutanisha wakuu wa nchi 16 ambao watakaa kwa siku mbili na kujadili masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii yanayolenga kuimarisha jumuiya iyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam Rais Magufuli amezipongeza nchi wanachama kwa hatua wanazoendelea kuchukua katika kutekeleza mkakati wa Maendeleo wa 2015/2063 na kuwahimiza wanachama kuwa na umoja na kushirikiana na sekta binafsi ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangia katika maendeleo.

Ujumbe mkubwa alioutoa Rais Magufuli kwa nchi wanachama ni pamoja na kukuza na kuendelea ubunifu kwa bunifu mbalimbali katika nchi zao na sio kukimbilia wataalamu kutoka nje pekee na hiyo ni  pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya kibiashara kwa kuhakikisha kuna umeme wa uhakika na wa bei nafuu huku akitolea mfano Tanzania ambayo kwa sasa inatekeleza mradi mkubwa ya umeme kutoka bonde la mto Rufiji utakaozalisha zaidi ya megawati 2000 pamoja na ujenzi wa reli itakayounganisha Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Magharibi mwa Tanzania na nchi jirani za  Rwanda na Burundi.

Mbali ya hilo ushauri mwingine alioutoa Rais Magufuli kwa nchi wanachama wa SADC ni kuweka vipaumbele kwa viwanda vya ndani ya jumuiya kwa kuuziana bidhaa na malighafi ili kuweza kuendelea zaidi na kukua kiuchumi kwa nchi zote za SADC.

Vilevile Rais Magufuli amezishauri nchi wanachama wa SADC kutoa vikwazo vinavyokwamisha kufikia maendeleo kwa urahisi zaidi na hiyo ni pamoja na utitiri za kodi, kuwepo kwa taasisi nyingi za usimamizi na sheria kali za udhibiti wa mipaka zinazowakwamisha wafanyabiashara kusafirisha bidhaa zao kutoka nchi moja hadi nyingine.

Magufuli amesema kuwa lazima nchi za jumuiya ya SADC zibadilike kwa kujenga viwanda vyetu wenyewe na kutumia malighafi zinazozalishwa katika  nchi zetu;

" Kuna upotevu mkubwa sana wa fedha za kigeni unaotokana na kuagiza bidhaa kutoka nje, bora tutumie fedha hizo katika kutekeleza miradi ya kimaendeleo. Tanzania tumeweka mkakati wa kujenga viwanda na kutumia malighafi tunazozalisha na kwa miaka mitatu ya uongozi wa serikali ya awamu wa tano zaidi ya viwanda vipya  4000 vimeanzishwa ni vyema nchi wanachama tukajizatiti katika hilo ili tufikie maendeleo" ameeleza Rais Magufuli.

Rais Magufuli amewashauri wanajumuiya iyo kuitumia wiki ya viwanda kwa kubadilishana uzoefu ili kuweza kufikia malengo na kuhimiza majadiliano yatakayofanyika katika wiki hiyo yafanyike wazi bila kuficha na yalete mapinduzi ya kimaendeleo na amewaalika wageni kutembelea vivutio vingi vinavyopatikana nchini zikiwemo mbuga za wanyama, mlima Kilimanjaro na kutalii katika visiwa vya Zanzibar.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...