Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la SMCCT, Evalyen Lyimo, akitoa mafunzo kuhusu lishe na chakula kwenye mkutano wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya mtoto na mama katika Kata sita zilizopo Wilaya ya Ikungi mkoani Singida. Mafunzo hayo yalikuwa na lengo ya kuzijengea uwezo kamati za ulinzi wa mama na mtoto ngazi ya wilaya hiyo.
Wadau na wanafunzi wakiwa kwenye mkutano huo wa kuunda kamati hizo
Wajumbe wa kamati za ulinzi wa mama na mtoto ngazi ya kata kutoka kata sita za wilaya ya Ikungi za Ihanja,Iseke,Iglanson,Minyughe na Muhintiri wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuundwa kwa kamati hiyo.
Mgeni rasmi wa mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akisalimiana na mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo.
Mgeni rasmi wa mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, akisalimiana na wanafunzi walioshiriki mkutano huo.
Mgeni rasmi wa mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akizungumza kwenye mkutano huo.
Wajumbe wa kamati za ulinzi wa mama na mtoto kutoka ngazi ya Wilaya ya Ikungi wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya hiyo, Edward Mpogolo (katikati aliyevaa miwani).



Na Dotto Mwaibale, Singida

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Save the Mother and the Children of Central Tanzania (SMCCT), limeunda kamati za ulinzi wa mama na mtoto katika kata sita na vijiji 18 katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida. 

Imeelezwa kwamba majukumu ya kamati hizo ni kumlinda mama na mtoto dhidi ya vitendo vya ukeketaji na ukatili wa kijinsia. Hayo yalisemwa na mwezeshaji wa mradi wa utetezi dhidi ya mila potofu, Japhet Kalegeya wilaya ni hapa juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mradi huo uliofadhiliwa na Shirika la Foundation for Civil Society ambalo limetoa shilingi milioni 40 kwa mradi utakaofanyika kuanzia mwezi Julai hadi Machi 2020. 

Alisema wamefikia uamuzi wa kuanzisha kamati hizo ili ziweze kuharakisha kutokomeza kabisa vitendo hivyo ambavyo vipo kinyume na haki za binadamu kama vile ukatili dhidi ya wanawake na watoto, mimba za utotoni, ndoa za utotoni ,ubakaji ,ulawiti,ukeketaji na udhalilishaji wa kijinsia katika wilaya hiyo. 

“Mradi huu wa utetezi dhidi ya mila potofu ikiwemo ukeketaji na ukatili wa kijinsia,unalenga kuwafikia wanawake na wasichana wapatao 7,200 katika wilaya ya Ikungi ambapo hali ya unyanyasaji wa kijinsia ni mbaya”,alisema Kalegeya.

Akitolea mfano wa hali hiyo alisema kuanzia Januari hadi oktoba 2018 jumla ya wanafunzi 37 waliokuwa kati ya kidato cha kwanza na nne walipachikwa mimba.

Naye mwanafunzi wa kidato cha tatu wa Sekondari ya Masinda, Rosemary Seith, amelishukru na kulipongeza shirika la SMCCT kwa kushirikisha baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuwapa elimu juu ya madhara ya ukeketaji na ukatili wa kijinsia. 

“Sisi tuliohudhuria mafunzo haya yametusaidia kujua kwa mapana madhara ya vitendo hivyo vya ukeketaji na ukatili wa kijinsia sasa tunaenda kuwaelimisha na wenzetu ambao hawakubahatika kupata mafunzo haya hapa leo”, alisema. 

Wakati huo huo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la SMCCT, Evalyen Lyimo, ametaja baadhi ya malengo ya mradi huo kuwa ni kuongezeka kwa uelewa kwa jamii kuhusu kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukeketaji na kuimarisha mfumo wa utoaji wa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia katika jamii hadi ifikapo Machi mwaka 2021.

Kata zilizounda kamati hizo ni Ihanja, Iglansoni,Iseke, Minyughe na Muhintiri.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...