Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima akipata maelezo kutoka kwa Mhandisi Henry Mbaga kuhusu shughuli za ujenzi wa dampo la kisasa katika Jiji la Mwanza eneo la Buhongwa. Jiji la Mwanza linatelekeleza mradi mkubwa wa Kimkakati wa ujenzi wa dampo ambalo lina ukubwa wa hekta 34 na linatarajia kukamilika 9/12/2019 kwa gharama ya shilingi Bilioni 16.6
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt. Philis Nyimbi na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Bw. Kiomoni Kibamba kwa pamoja wakikagua maendeleo ya ujenzi wa dampo la kimkakati. Naibu Waziri Sima ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa dampo hilo la kisasa ambalo limezingatia hifadhi ya mazingira.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt. Philis Nyimbi katika kikao na wafanyabiashara wa vyuma chakavu Kanda ya Ziwa (hawapo pichani). Naibu Waziri Sima yuko katika ziara ya kikazi Mikoa ya Kanda ya ziwa yenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zinazohusu sekta ya Mazingira nchini.

…………………………

Na Lulu Mussa,Mwanza

Serikali imezitaka halmashauri zote nchini, kutenga maeneo maalumu mbali na makazi ya watu yatakayotumika kujenga madampo ya kisasa ili kuzingatia hifadhi ya mazingira.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima mara baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa dampo la kisasa linalojengwa eneo la Buhongwa Jijini Mwanza.

Alisema ujenzi wa huo wa dampo la kisasa utasaidia juhudi za Serikali za kutotumia fedha nyingi kwenye ununuzi wa vifaa tiba kwa kuwa taka zitakazolishwa katika Jiji la Mwanza zitapelekwa dampo kwa wakati na kunusuru magonjwa ya mlipuko.

“Huwezi kutenganisha afya na mazingira, mradi huu ni mkubwa sana na kwa namna utakavyotekelezwa hatutaraji kuona taka mjini zinazagaa.Tunatarajia kuona taka zote zinakuja hapa,” alisema Sima.

“Natoa rai kwa halmashuri zingine ambazo zinatekeleza miradi ya kimkakati kutoa kipaumbele kwa ujenzi wa madampo ya kisasa”.

Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Kiomoni Kibamba alisema dampo hilo lina ukubwa wa hekta 34 na linatarajia kukamilika desemba mwaka huu na kwa sasa ujenzi upo asilimia 78 ukigharimu Sh bilioni 16.6, ukienda sambamba na ujenzi wa barabara.

“Dampo hilo litakuwa na chemba sita za kuhifadhi taka na mabwawa ya kuhifadhi maji taka, barabara za kisasa zenye urefu wa kilomita 1.9, taa za nishati ya jua na maabara maalumu ya kupima maji taka” Kibamba alisema 

Kukamilika kwa dampo hilo la kisasa litakuwa na uwezo wa kuteketeza taka mara baada ya kufikishwa kwenye eneo hilo na,litaongeza mapato katika jiji hilo.Kwa mujibu wa Kibamba, tani 33 hadi 36 zinatarajia kupelekwa katika dampo hilo mara baada ya ujenzi kukamilika na linatarajia kudumu kwa zaidi ya miaka 15

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...