Na Said Mwishehe, Globu ya Jamii.

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro ametoa maagizo kwa makamanda wa Polisi wa Mikoa na vikosi vya Polisi kujiepusha na vitendo vya rushwa na kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu pamoja na kushiriki kikamilifu kuunga mkono jitihada za Serikali kufanisha Tanzania ya viwanda.

Akizungumza leo Septemba 24,mwaka 2019 jijini Dar es Salaam wakati  wa kufungua mkutano wa siku tatu wa  kutathimini utendaji kazi wa Jeshi hilo IGP Sirro  ametumia nafasi hiyo kueleza mambo kadhaa ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria huku pia akikemea tabia ya vitendo vinavyofanywa na baadhi yao kiasi cha kuchafua sifa ya jeshi hilo.

IGP Sirro amesema jeshi la Polisi lazima liendelee kulinda usalama wa raia na mali zao na hatarajii kuona jeshi hilo linakuwa chanzo cha migogoro kati yake na wananchi.

Katika mkutano huo IGP Sirro amesema kuwa amezungumzia umuhimu wa Jeshi la Polisi kuhakikisha katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Novemba mwaka huu linafanya kazi zake kwa umakini zaidi ikiwa pamoja na kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama na amani iliyopo inaendelea kudumu.

"Haturajii jeshi letu la polisi kuwa chanzo cha kuvuruga amani, tunakwenda kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na mwakani uchaguzi mkuu, ni lazima tuwe makini kwa kuhakikisha tunafanya kazi kwa weledi,"amesema.

Kuhusu rushwa, IGP Sirro amesema bado kuna baadhi ya askari polisi wamekuwa wakitengeneza mazigira ya kupata rushwa ambapo ametumia nafasi hiyo kutoa onyo kwa wenye kujihusisha na rushwa ndani ya jeshi hilo.

"Kuna baadhi ya askari polisi bado wanaendeleza vitendo vinavyoashiria kuomba rushwa kwa wenye kutenda makosa na hasa barabarani.Jeshi la Polisi halitaki kuona rushwa kwa watumishi wake na hivyo wenye tabia ya kujihusisha na rushwa kuacha mara moja,"amesema IGP Sirro.

Amewataka makamanda na makamishina wote nchini kuhakikisha wanasimama kidete kukomesha rushwa na kuwataka kila mmoja kwa nafasi yake kukemea vitendo vya rushwa."Bado kuna askari polisi wanachukua rushwa hadharani wanaposimamisha mabasi."

Pamoja na mambo mengine IGP Sirro ametumia nafasi hiyo kuonesha kusikitishwa na baadhi ya makamanda wa mikoa kutokamilisha kwa wakati ujenzi wa nyumba za watumishi katika mikoa yao ambapo amewaagiza kuharakisha ujenzi wa nyumba hizo.

Kuhusu jeshi la polisi kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.John Magufuli amesema ili maendeleo ya nchi hii yaweze kupatikana yanahitaji nchi kuendelea kuwa salama na hivyo jeshi hilo litaendelea kutimiza majukumu yake kikamilifu. "Jeshi la Polisi tutaendelea kusimama imara kulinda usalama wa nchi yetu."

Wakati huo huo IGP Sirro amewataka makamishna wa mikoa kuwaanda askari vijana ambao watashika nafasi zao ili wao kurejea makao makuu kwa ajili ya utungaji wa sheria na ushauri  kwani ni vyema kuwa na damu changa itakayoweza kufanya kazi kwa nguvu zaidi kuliko kung'ang'ania nafasi hizo za ukamishna.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...