Na Zaynab Nyamka, Globu ya Jamii
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Celestine Mwesigwa ameanza kujitetea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo amedai aliyekuwa rais wa TFF, Jamal Malinzi alikuwa akiikopesha TFF na kwamba hakuhusika kwenye mchakato wa kumtoa aliyekuwa Mkurugenzi mpya wa Fedha na Mipango.

Mwesigwa amekiri kwamba mara ya mwisho Malinzi aliikopesha TFF Sh milioni 15 ili kulipia matangazo ya moja kwa moja ya  mechi ya Serengeti Boys iliyokuwa ikichezwa hapa  nchini kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Mwesigwa amedai hayo leo Septemba 20,2019  mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde wakati akijitetea mahakamani hapo.

Akiongozwa na Wakili wake, Richard Rweyongeza, Mwesigwa amedai mkataba wa udhamini ulionesha kuwa michezo inapochezwa ndani ya Tanzania mechi zioneshwe moja kwa moja kwenye chaneli ambazo wananchi wanaweza kuangalia bila kulipia.

Amedai walikuwa hawalipi chochote endapo Azam Pay TV ikionesha mechi hizo lakini wananchi walipaswa kulipia hivyo, walilazimika kuonesha kupitia TBC

Ameendelea kudai kuwa TBC walituomba kuonesha mechi hivyo tuliomba masafa kwa Azam ili kuwapa TBC kurusha matangazo ya moja kwa moja ambao walitukubalia lakini ndani ya saa 24, TBC walituambia hawarushi matangazo bila kulipwa Sh milioni 15," alidai Mwesigwa.

"Wakati wanatuambia tuwalipe akaunti yetu haikuwa na fedha tuliandaa hundi lakini hatukuweza kuwapa TBC kwani haikuwa na fedha. Tulimpigia rais na kutuambia kuwa atatupa fedha ili kuondoa aibu ya taifa."

Amedai walichukua fedha hizo na kupeleka benki ya DTB ndipo mechi hiyo ilirushwa moja kwa moja na kwamba Malinzi ni miongoni mwa wafadhili waliokuwa wakiisaidia TFF kwenye shughuli mbalimbali za timu za taifa.
Amedai Malinzi na wafadhili wengine walikuwa wakilipwa baada ya kupata fedha kwenye mashindano, fedha kutoka kwa wafadhili ambao ni CAF na Shirikisho la Mpira duniani (FIFA) na endapo hali ya kifedha inapokuwa nafuu.

Mwesigwa alidai vyanzo vya mapato vya TFF ni mashindano, ufadhili na udhamini na kwamba CAF na FIFA wanatoa fedha baada ya kupeleka ripoti ya ukaguzi wa fedha ya msimu uliopita.

"Malinzi alikuwa akitupa fedha endapi tutashindwa  kumlipa mkaguzi wa hesabu wa TFF ambaye anachaguliwa na FIFA," alidai.

Mwesigwa amedai aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Mipango, Edger Masoud ajira yake ilikoma baada ya kushindwa kufanya kazi vizuri hivyo, walivunja mkataba na TFF kwa kushirikiana na FIFA walifanya mchakato wa kumpata Mkurugenzi mpya hivyo, walitoa matangazo na kupata majina ya watu watatu.

Alidai majina hayo yalipelekwa kamati ya ajira chini ya Mwenyekiti wake Warace Karia wakati huo, ambapo walichambua majina hayo na kumpata Aziza Mwanja.

Mwesigwa pia alidai hawakuhusika katika matumizi mabaya ya madaraka na badala yake walifuata taratibu zilizowekwa na shirikisho hilo.

Mbali na Malinzi na Mwesigwa  washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga na Karani Flora Rauya.

Katika kesi  hiyo ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 20 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa Dola za Marekani 173,335

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...