Songea: MKOA wa Ruvuma una ziada ya  chakula tani  zipatazo 269,000  zilizo zalishwa katika msimu wa kilimo  2019 katika maghala yake, huku  pato la mwananchi katika mkoa huo likipanda kutoka shilingi ml 2.1  mwaka 2015 hadi kufikia ml 2,240,000. mwaka 2019 kwa mwaka.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wik,i wakati akiongea na waandishi wa Habari alipotembelea kituo cha ununuzi wa mahindi cha  wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula NFRA Kanda ya Songea kilichopo eneo la Ruhuwiko mjini Songea.

Alisema, mafanikio hayo yametokana na juhudi kubwa za uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara unaofanywa na wakulima wa mkoa huo ambao wamekuwa wanatumia fursa za kuwepo kwa Ardhi nzuri na mvua zinazo nyesha kwa wingi kuzalisha mazao mashambani.

Aidha Mkuu wa Mkoa, ametangaza rasmi bei mpya ya mahindi kutoka shilingi 430 hadi 600 kwa kilo na kuwataka wakulima kupeleka mahindi yao kwa NFRA ili kupata bei nzuri, badala ya kuuza kwa wafanya biashara wengine ambao wananunua kwa bei isiolingana na gharama halisi ya uzalishaji.

Mndeme, amemshukuru Rais Dkt John Magufuri na Serikali yake kwa uamuzi wa kuongeza bei ya mahindi kwa wakulima wa mkoa huo kutokana na kutambua thamani ya  kazi zao na pia  itaongeza hamasa ya uzalishaji wa  mazao ya chakula na biashara.
Pia Mndeme alieleza kuwa,Serikali imeongeza mgao wa mahindi Wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula kutoka tani 13,000 mwaka 2018 hadi kufikia tani 25,000  katika msimu 2019  na  uamuzi huo unatokana na serikali kutambua na kuthamini kazi zinazo fanywa na wakulima wa mkoa huo.

Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa alisema, Serikali imeanza  kujenga vihenge na maghala mapya ambayo yatatumika kuhifadhi na kuongeza thamani ya mazao nakutoa wito kwa watu wenye uhitaji wa chakula kwenda Ruvuma kununua mahindi.

Pia alisema, jumla ya watu 600 wamepata vibarua  vya muda na kudumu katika kituo cha wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula wanaofanya kazi mbalimbali, hivyo NFRA imesaidia sana kupunguza tatizo la ajira kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma.

Amewataka wananchi waliobahatika kupata nafasi hizo,kufanya kazi kwa  kujituma na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuharibu mchakato  wa ununuzi wa mahindi, kwani uwepo wa kituo cha kununulia mahindi cha NFRA umesaidia kupunguza ukali wa maisha kwa jamii ya watu wa Ruvuma.

Kwa upande wake,kaimu meneja wa wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula NFRA kanda ya Songea Eva Michael alisema, hadi sasa NFRA imenunua tani 12,000 za mahindi na wanaendelea kupokea mahindi kutoka sehemu mbalimbali ndani ya Mkoa wa Ruvuma.

Alisema, zoezi la ununuzi wa mahindi linafanyika kwa ubora wa hali ya juu ili kupata mahindi safi ambayo yatakidhi vigezo na kuwataka wakulima kupeleka mahindi kwa wingi  kwa NFRA ambao ndiyo wakombozi wa mkulima katika mkoa huo.

Baadhi ya wakulima waliokutwa wakiuza mahindi yao katika kituo hicho,wameishukuru Serikali kwa uamuzi wa kuongeza bei ya mahindi,hata hivyo wameiomba  kudhibiti uuzaji holela wa pembejeo hasa mbolea ambazo zinauzwa kwa bei kubwa.

Rose Mbonde alisema,wakulima wamekuwa wakitekeleza maagizo mbalimbali yanayotolewa na Serikali yao, hata hivyo wengine wanashindwa kulima kutokana na changamoto kubwa ya kupanda kwa pembejeo ambazo zinauzwa kwa bei  ya juu  jambo linalo wakatisha tamaa baadhi ya wakulima.

Michela Hyera, ameiomba Serikali kituo cha Ruhuwiko kiwe cha kwanza  cha kuuzia mahindi kwani kunamazingira mazuri ya wakulima kuleta mahindi yao ikilinganisha na vijijini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...