MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema
ufuatiliaji pamoja na usimamizi makini wa Watendaji wa Ofisi yake
katika kuratibu matumizi sahihi ya fedha zinazotekeleza Miradi ya
Kijamii ndio uliopelekea kufanikisha vyema kwa Miradi ya Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF}.
Amesema Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambayo ndio
inayoratibu shughuli zote za Tasaf kwa upande wa Zanzibar imelazimika
kuchukuwa hatua hiyo ili kulinda Heshima itakayotoa ushawishi kwa
Wafadhili wa Mpango huo kuendelea kuunga mkono katika utoaji wa Mikopo
zaidi.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati wa Mazungumzo yake ya
Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 yanayounda Taifa la Nigeria
waliowasili Zanzibar kwa ziara ya Siku mbili kuja kujifunza kutokana
na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika mpango wa kuhudumia Kaya
Maskini Nchini Tanzania.
Ameeleza kwa vile Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} unatoa
huduma katika pande zote mbili za Tanzania, Serikali zote mbili ile
ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar zinalazimika kufuatilia mwenendo mzima wa fedha
zinavyotumika katika Miradi ya Tasaf ili kufikia lengo.
“ Serikali ililazimika kufanya uchambuzi yakinifu na kujiridhisha
katika mwenendo wa wa matumizi ya Miradi ya Tasaf ili kuepuka upotevu
ambao ungegharimu machungu kwa wasimamizi wa Miradi hiyo”. Alisisitiza
Balozi Seif.
Amesema ipo Miradi mingi ya Kijamii katika maeneo mbali mbali ya
Visiwa vya Unguja na Pemba Mjini na Vijijini iliyoleta ukombozi kwa
Wananchi walio wengi baada ya kupata msukumo uliotokana na uanzishwaji
wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania katika Awamu tofauti
uliojikita kuhudumia moja kwa moja miradi hiyo.
Balozi Seif amesema ipo haja kwa Wafadhili wa Miradi ya Kijamii
akatolea Mfano Benki ya Dunia pamoja na Taasisi nyengine za Kimataifa
za misaada ya Maendeleo kuendelea kuongeza ufadhili wao kwa vile lengo
la uanzishwaji wa Miradi ya Kijamii limefanikiwa vyema.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema hatua hiyo ya
Wafadhili ni muhimu kwa vile inaweza kusaidia kuondoa mkwamo kwa
baadhi ya Changamoto zinazotokana na Miradi inayoanzishwa hasa katika
Sekta za uzalishaji kupitia Vikundi vya ujasiri amali.
Balozi Seif ameishauri Timu hiyo ya Waratibu Wakuu wa Majimbo ya
Nigeria kwamba katika kuimarisha Miradi na huduma za Kijamii ipo haja
ya Mataifa ya Afrika kuzidi kushirikiana katika kubuni mbinu na njia
za pamoja katika kuendeleza Miradi hiyo itakayoleta ustawi na Maisha
bora kwa Waafrika walio wengi.
Amesema mfano ulioonyeshwa na Timu hiyo ya Waratibu Wakuu wa Majimbo
36 ya Taifa la Nigeria wa kufika Tanzania kujifunza mwenendo wa
uendeshaji wa Miradi ya Kijamii ni mwanzo wa kuigwa kwa Mataifa
mengine yanayotekeleza Miradi kama hiyo Barani Afrika.
Mapema Mratibu wa Washirika wa Sekta za Kijamii kutoka Ofisi ya Makamu
wa Rais wa Nchini Nigeria Bwana Gyangyang Limave ameishukuru na
kuipongeza Tanzania kwa umakini wake iliyonao wa kuhakikisha Bara la
Afrika linaendelea kuimarika Kiuchumi na Ustawi.
Byangyang amesema msimamo wa Tanzania katika kustawisha maisha
ya Wananchi wake ni mfano wa kuigwa na Mataifa mengine Duniani
yaliyoanza mpango wa kuimarisha Taasisi za Kijamii.
Amesema Serikali ya Nigeria katika muelekeo wake wa kustawisha Maisha
ya Wananchi wake tayari imeshaanzisha Taasisi inayoratibu na kusimamia
kasuala ya Kijamii mnamo Mwaka 2016.
Gyangyang Limave amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
kwamba zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 1.3 zimetolewa na Serikali
Kuu katika kuimarishaji wa Kaya Maskini Nchini humo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kushoto akisalimiana na Mratibu wa Washirika wa Sekta za Kijamii kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wa Nchini Nigeria Bwana Gyangyang Limave wakati akijiandaa kuzungumza na Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 ya Taifa la Nigeria waliofika Zanzibar kujifunza Mpango Maalum wa uendeleshaji wa Miradi ya Tasaf.
Balozi Seif Kulia akizungumza na Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 ya Taifa la Nigeria waliofika Zanzibar kujifunza Mpango Maalum wa uendeleshaji wa Miradi ya Tasaf.
Balozi Seif katikati waliokaa vitini akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 ya Taifa la Nigeria pamoja na Watendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} Bara na Zanzibar.
Balozi Seif akibadilishana mawazo na Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 ya Taifa la Nigeria mara baada ya kupiga picha za ukumbusho wa uwepo wao Visiwani Zanzibar.
Balozi Seif akiagana na Kiongozi wa Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 yanayounda Taifa la Nigeria Naibu Mkurugenzi wa Taasisi inayosimamia masuala ya Ustawi wa Jamii Bwana Ortutu baada ya mazungumzo yao. Picha na – OMPR – ZNZ.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...