Dkt John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania amemualika Mhe Yoweri Kaguta Museveni Rais wa Jamhuri ya Uganda kuzindua kongamano la kwanza la biashara kati ya Tanzania na Uganda linalotarajiwa kufanyika tarehe 6-7 Septemba, 2019 katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam. 

Hayo yamesemwa na Mhe Innocent Bashungwa, Waziri wa Viwanda na Biashara wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuwaeleza kuwa Mhe Yoweri Kaguta Museveni Rais wa Jamhuri ya Uganda ataambatana na wafanayabiashara kutoka nchini kwake ili kukutana na wafanyabaishara wa Tanzania. 

Mhe Bashungwa ameeleza kuwa lengo la kongamano hilo ni kutangaza fursa na kuhamasisha biashara na uwekezaji zilizoko Tanzania na Uganda. Pia Serikali itapata fursa ya kuongea na wafanyabiashara hao ili kuangalia changamoto za kufanya biashara katika nchi hizo mbili. Vilevile Serikali zetu zitashirikiana kuzitatua, kuangalia fursa zilizopo, kuongeza biashara katika nchi hizo mbili na kuhamasisha uwekezaji. 

“Sisi Tanzania tumekuwa tunawauzia chakula na vifaa vya viwandani, kwakuwa tunajenga uchumi wa viwanda ni fursa kwa watanzania kushiriki kwenye kongamano hilo ambalo litakuwa na tija kubwa kwetu kama nchi. Rais wetu analeta wakuu wa nchi mbalimbali ikiwemo Uganda ili kuwaonesha fursa tulizonazo pamoja na kujenga mtandao mpana wa biashara”, amesema Mhe Bashungwa 

Mhe Bashungwa ameeleza kuwa kutakuwa na Maonesho ya bidhaa za Tanzania ambapo Watanzania watapata fursa ya kuonesha bidhaa za kilimo na za viwandani, taasisi za umma na sekta binafsi zinazosaidia katika mnyororo wa thamani za biashara. Ujio wa Rais wa Jamhuri ya Uganda pamoja na wafanyabiashara toka nchini humo itakuwa ni fursa ya kuunganisha wafanyabiashara wetu na wafanyabiashara wa Uganda kukuza wigo wa biashara, kupata masoko mapya pamoja na kutatua changamoto na kujenga mazingira mazuri zaidi ya kufanya biashara. Amewahamasisha wazalishaji wa bidhaa za kilimo, wafanyabaishara na wamiliki wa viwanda kutoka Mikoa yote ya nchini kujitokeza kushiriki. 

“Wafanyabaishara waelewe kuwa ni mwanzo mzuri wa kupenya katika soko la Sudani ya Kusini kwasababu wapo wafanyabiashara wa Uganda wanafanya biashara nchini Sudani ya Kusini” amesema Mhe Bashungwa. 

Ameendelea kusema kuwa mwelekeo wa Serikali ya Tanzania ni kujenga uchumi wa viwanda hivyo ni fursa kwa Watanzania kutumia kongamano hili kwasababu Serikali inazidi kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara nchini, kujenga viwanda na kufuatilia masoko mbalimbali lengo ni kutaka uuzaji wa bidhaa nchini Uganda uongezeke. 

Imetolewa na: 
Theresa Chilambo 

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano-TanTrade

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...