Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv
HAKIMU Mkazi wa Mahakama ya Ukonga, Faudhia Hamza ametoa wito kwa wananchi wenye dukuduku, malalamiko ama vinyongo mioyoni mwao juu ya mambo yote ya kimahakama kujitokeza katika Mahakama inayotembea kutoa shida zao.
Wito huo umetolewa leo Septemba 12,2019 wakati akiendesha kesi katika mahakama inayotembea eneo la Chanika jijini Dar Salaam na kuongeza kuwa, Mahakama hiyo itakuwa ikitoa huduma kila alhamisi katika eneo la ofisi ya serikali ya mtaa ya chanika.
"Ninawaomba wananchi wote nchini mnapoiona hii gari ya mahakama inayotembea msiikimbie wala kufikiri kuwa sasa mtafungwa hapana, huu ni ukombozi wenu jitokezeni ili kutatua matatizo hasa yanayohusiana na madai, mirathi na ndoa" Amesema Hakimu Hamza.
Ameongeza kuwa katika jamii watu wamekuwa wakikaa na vitu katika mioyoni ambavyo vinawapelekea kuchukua maamuzi magumu ikiwamo kujinyonga kutokana na kukosa ushauri ama elimu ila mahakama hii inayotembea ipo kwa ajili ya wananchi, inapokea kesi, vinyongo, madukuduku na malalamiko waliyonayo wananchi na kuwashauri kwa mujibu wa sheria na taratibu zake.
Kwa upande wa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala,Martha Mpaze amesema mahakama hii inayotembea imejikita kusikiliza kesi za madai, talaka na Mirathi kwa kutoa usuluhishi zaidi na kwamba utakuwa akitoa maamuzi ndani ya siku 30.
Amesema wamesogeza huduma hizo karibu na Mwananchi ili kuhakikisha haki inatendeka kwa usawa, urahisi na kwa wakati na kwamba awali huduma hizo zilikuwa zikitolewa katika Mahakama ya Mwanzo ya Ukonga lakini kutokana na umbali na nguzo ya tatu ya mahakama ya kuwa karibu na Mwananchi.
Huduma hii ya mahakama inayotembea iliyoanzishwa mwaka huu 'mahakama mtaani kwako' kwa sasa inafanyakazi katika Mkoa wa Dar es Salaam na Mwanza.
Kwa upande mkazi mmoja wa Chanika ambaye ni Katibu wa CCM, Yahaya Rajabu aliishukuru mahakama kwa kusogeza mahakama mtaani kwani itasaidi wananchi kupata uelewa wa sheria kwa kuwa wengi wanakabiliwa na changamoto nyingi hasa migogoro ya talaka na wana kuwa njia panda hawajui nini cha kufanya lakini ushauri na elimu inayotolewa na mahakama hiyo itawapa dira jinsi ya kukabiliana nazo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...