Na Veronica Simba – Dar es Salaam
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, amekutana na wazalishaji binafsi wa umeme nchini na kujadiliana masuala mbalimbali ya kuboresha zaidi sekta hiyo, ikiwa ni mwendelezo wa kutekeleza kwa vitendo azma ya serikali kutambua mchango wao na kuwawezesha.
Mkutano huo ulifanyika Septemba 19 jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa pia na Naibu Waziri Subira Mgalu, Katibu Mkuu Dkt Hamisi Mwinyimvua, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mhandisi Leonard Masanja, viongozi pamoja na wataalamu wengine mbalimbali kutoka wizarani na taasisi zilizo chini yake.
Akifungua mkutano huo, Waziri Kalemani alisema serikali itaendelea kutambua na kuthamini mchango wa wazalishaji hao wa umeme na itaendelea kuwajengea mazingira wezeshi ili wakue na kuzalisha zaidi kusudi lengo la kufikia uchumi wa kati na wa viwanda liweze kufikiwa.
“Nishati ndiyo injini ya uchumi wa viwanda. Pasipo umeme wa uhakika na wa kutosha, hakuna viwanda. Hivyo basi, pamoja na serikali kuanzisha na kutekeleza miradi mikubwa ya umeme, tungali tunahitaji mchango wenu pia ili tuzalishe umeme wa kutosha kwa ajili ya viwanda na matumizi mengine nchini.”
Aidha, akifunga mkutano husika, Waziri alitaja mambo kadhaa muhimu yatakayozinufaisha pande zote mbili, serikali na wawekezaji kwa kuzingatia manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Aliwataka wadau wa sekta hiyo kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC) na wengineo, kupitia upya masharti ya utoaji leseni na kuyaboresha ili kuwajengea wawekezaji mazingira rafiki zaidi ya uwekezaji lakini pasipo kukiuka sheria.
Vilevile, Waziri alielekeza kuwa taasisi zinazohusika na utoaji vibali, ziache tabia ya urasimu wa kutumia muda mrefu katika kushughulikia barua za mapendekezo kutoka kwa wawekezaji. Alitaka uwepo utaratibu wa kujibu barua hizo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja lakini kwa kuzingatia sheria.
Aidha, alitoa maelekezo kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kutangaza utaratibu wa upatikanaji ruzuku inayotolewa na serikali kwa wawekezaji hao na kuwashindanisha waombaji kwa uwazi kulingana na sifa zao ili kuepusha upendeleo.
Waziri pia alielekeza kwamba maeneo yote mahsusi ya uwekezaji katika sekta ya umeme jadidifu yabainishwe na kuwekwa wazi, ili watu wayajue na kwenda kuwekeza.
Kuhusu suala la gharama za umeme, Waziri alielekeza kuwa inapaswa bei zinazotolewa na wawekezaji binafsi ziwiane na za serikali ili kuwawezesha wananchi wote kunufaika na huduma hiyo pasipo malalamiko kuwa wengine wanapendelewa. “Mathalani, gharama iliyowekwa na serikali kuunganisha umeme kwa wananchi vijijini ni shilingi 27,000 tu; nanyi inabidi mjipange ili mtoze bei inayowiana na hiyo,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mgalu aliunga mkono yale yote yaliyoelekezwa na Waziri na akatilia mkazo kuwa taasisi za REA na TANESCO zihakikishe zinaweka utaratibu wa kufanya mapitio ya miradi mbalimbali ya umeme jadidifu inayotekelezwa nchini, hususan katika maeneo ambayo hayafikiwi na gridi ya taifa, ili kujiridhisha na maendeleo yake.
Naye Juma Shamte ambaye ni Mwakilishi wa wanachama wa Umoja wa Wazalishaji Binafsi wa Umeme Tanzania (Tanzania Independent Power Producers Association – TIPPA), alimshukuru Waziri Kalemani na serikali kwa ujumla kwa jitihada ambazo zimekuwa zikifanyika katika kutambua mchango wao na kuendelea kuwajengea mazingira wezeshi ya uwekezaji.
Awali, ilielezwa kuwa hadi sasa, idadi ya wanachama hai waliojiandikisha na kutambulika rasmi na serikali kama wazalishaji binafsi wa umeme nchini, inafikia 110 na kwamba kiasi cha umeme wanachozalisha kinafikia megawati 18 ambapo huingizwa kwenye gridi ya taifa na kiasi kingine hutumika kuhudumia wateja moja kwa moja.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akiongoza kikao baina yake na wazalishaji binafsi wa umeme nchini, jana Septemba 19, 2019 jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu na kulia kwake ni Katibu Mkuu Dkt Hamisi Mwinyimvua.
Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, akizungumza wakati wa mkutano wa Waziri wa Nishati na wawekezaji binafsi wa umeme (hawapo pichani), uliofanyika Dar es Salaam, Septemba 19, 2019.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Dkt Hamisi Miwnyimvua akizungumza wakati wa mkutano wa Waziri wa Nishati (kulia) na wawekezaji binafsi wa umeme (hawapo pichani), uliofanyika Dar es Salaam, Septemba 19, 2019.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akiongoza kikao baina yake na wazalishaji binafsi wa umeme, kilichofanyika Septemba 19, 2019 jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi wa wanachama wa Umoja wa Wazalishaji Binafsi wa Umeme Tanzania (Tanzania Independent Power Producers Association – TIPPA), Juma Shamte akizungumza wakati wa mkutano wa Waziri wa Nishati na wawekezaji binafsi wa umeme (hawapo pichani), uliofanyika Dar es Salaam, Septemba 19, 2019.
Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Leonard Masanja akizungumza wakati wa mkutano wa Waziri wa Nishati na wawekezaji binafsi wa umeme uliofanyika Dar es Salaam, Septemba 19, 2019.
Kutoka kushoto ni Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mhandisi Leonard Masanja, Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu Edward Ishengoma na Kamishna Msaidizi wa Umeme Mhandisi Innocent Luoga, wakifuatilia mkutano wa Waziri wa Nishati na wawekezaji binafsi wa umeme uliofanyika Dar es Salaam, Septemba 19, 2019.
Sehemu ya wataalamu kutoka wizarani wakifuatilia mkutano wa Waziri wa Nishati na wawekezaji binafsi wa umeme uliofanyika Dar es Salaam, Septemba 19, 2019.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Dkt Hamisi Mwinyimvua (kushoto), wakifuatilia hoja zilizokuwa zikiwasilishwa na wawekezaji binafsi wa umeme (hawapo pichani) wakati wa kikao baina yao (wawekezaji) na Waziri kilichofanyika Septemba 19, 2019 jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...