Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV
BAADA ya miaka ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Yusuph Makamba na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Shinyanga Khamisi Mgeja kuishi wakiwa maadui hatimaye wamekutana na kusameehana na kuondoa tofauti zao kwa kusoma dua maalum.
Makada hao wa CCM wamekutana nyumbani kwa Makamba maeneo ya Kisanga Tegeta jijini Dar es Salaam na hivyo kutumia nafasi hiyo kuzungumza mambo mengi na kubwa ni kuombana msamaha na kusameehana.Baada ya dua wakacheka pamoja na kukumbatiana.
Akizungumza Mgeja kwa upande wake amesema kilichowasukuma kuondoa tofauti zao ni maadili na misingi ya dini na kwa maslahi mapana ya dini na utu tu si vinginevyo dini imesisitiza kusameheana."Sisi siasa ilitufikisha pabaya sana na mzee wangu huyu".
Kwa upande wake mzee Makamba amempongeza Mgeja kwa kueleza miaka ya nyuma Makamba akiwa Katibu mkuu wa CCM na Mgeja akiwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga walikuwa marafiki sana lakini shetani aliingilia kati na kumkumbusha umuhimu wa kusameheana na kutoa maelekezo yaliomo ndani ya dini.
Makamba ameitaka jamii izidishe upendo na kujenga utamaduni wa kusameheana kama alivyofanya yeye na Mgeja. "Tumeondoa tofauti na huko mbinguni, hizi siasa tutaaziacha hapa hapa duniani huko kila mmoja na amali zake, tujitahidi kufanya mema hapa duniani na kuzidisha upendo baina yetu,"amesema.
Baada ya kuondoa tofauti hizo wote pamoja kuangalia mifugo ya mzee na hasa ng'ombe wa maziwa, kuku, bata na sungura.
Mgeja baada ya kutembezwa na kujionea ufugaji wa kisasa amempongeza mzee Makamba kwa ufugaji wa kisasa wa kitaalamu na wenye tija kiasi ambacho amepata somo zuri na ujuzi huo atauchukua kuupeleka nyumbani kahama shinyanga.
"Hakika ugeni wangu huu pamoja na suluhu lakini nimepata elimu nzuri sana zitanisaidia katika shughuli zangu za ufugaji na kilimo ambazo ndizo niliko jielekeza hivi sasa huko nyumbani kijiji cha Nyanhembe kata ya Kilago halmashauri ya mji wa Kahama Shinyanga" amesema Mgeja
Mgeja ametoa mwito kwa watanzania wajielekeze katika shughuli za kilimo na ufugaji wenye tija kwani kuna fursa kubwa sana na hasa vijana kutoa ajira na ukuaji wa uchumi kuliko kubaki kijiweni na kubaki kuwa walalamikaji tu.
Pia ameshauri Watanzania kichangamkia soko jipya la sungura ambalo linakuwa kwa kasi ndani ya nchi na nje ya nchi hasa majirani zetu nchi za Kenya na kwamba Tanzania bila umasikini inawezekana.
Mgeja amesema ni vema kila mmoja wetu akatambua maendeleo na tukitaka kuondokana na umasikini ni lazima kufahamu maendeleo hayana njia ya mkato lazima afanye kazi kwa juhudi na maarifa na ndio siri ya mafanikio.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)Yusuph Makamba (aliyevaa kanzu) akiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Shinyanga wakiwa wamekaa pamoja baada ya kukutana na kuomba msamaha kutokana na tofauti walizokuwa nazo kwasababu ya mambo ya kisiasa
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...