Na Veronica Simba – Tabora
Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imekagua mradi wa umeme jua unaotekelezwa katika kijiji cha Tura, kilichopo Uyui, Mkoa wa Tabora; ikiwa ni sehemu ya ziara ya kamati hiyo katika mikoa mbalimbali nchini, kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.

Akizungumza Oktoba Mosi, 2019 baada ya kukagua mitambo miwili ya umeme jua iliyofungwa kijijini hapo, Mwenyekiti wa Kamati husika, Mhandisi Styden Rwebangira, alisema mradi huo uliofadhiliwa na serikali kupitia mkopo wa gharama nafuu kutoka serikali ya Austria, ni njia mojawapo ya kuwafikia wananchi walio mbali na gridi ya Taifa.

“Kijiji hiki ni mojawapo ya wanufaika; kimepata umeme huu wakati kikisubiri umeme wa REA, maana kimeainishwa kupatiwa umeme huo katika Awamu ya Tatu ya mradi husika, Mzunguko wa Pili,” amefafanua.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu, alisema Wakala huo umeshakamilisha upimaji, ambapo takwimu zinaonesha kuwa, kutoka kwenye njia iliyo na umeme mpaka kijiji husika ni takribani kilomita 98.8 za umeme wa msongo wa kati.

“Mpango wetu ni kusambaza umeme huo kwa umbali wa kilomita 10 ili kuwafikia wateja wote zaidi ya 400 waliopo katika kijiji hiki,” alisema Olotu.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kata ya Tura, Nelson Mungwila, alitoa shukrani kwa serikali kwa kubuni mradi huo ambao alisema umekuwa wa manufaa makubwa kwa wananchi husika hususan katika kuboresha hali zao kiuchumi kupitia miradi mbalimbali wanayojishughulisha nayo.

Aliiomba serikali iwasaidie kuchangia gharama za kununua betri mpya za kuendeshea mitambo hiyo ya umeme jua ili wananchi waendelee kunufaika na mradi huo, kwani zilizopo zimeharibika.

Katika ziara hiyo, Kamati husika itatembelea mikoa mbalimbali kwa takribani wiki moja, kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini kwa lengo la kutatua changamoto zinazochelewesha utekelezwaji na ukamilishwaji wake.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Styden Rwebangira (kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu (kushoto), wakikagua moja ya mitambo ya umeme jua iliyopo katika kijiji cha Tura, wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora, Oktoba 1, 2019.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Styden Rwebangira (katikati) na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu (kushoto), wakijadiliana jambo na Afisa Mtendaji wa Kata ya Tura, Nelson Mungwila (kulia), walipowasili kwenye kata hiyo kukagua mradi wa umeme jua, Oktoba 1, 2019.
 Shule ya Msingi iliyopo katika kijiji cha Tura, wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora. Shule hii ni miongoni mwa taasisi za umma zinazonufaika na mradi wa umeme jua unaotekelezwa kijijini hapo kwa ufadhili wa serikali.
 Mashine ya kusaga nafaka iliyopo kijiji cha Tura, wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora. Mashine hii ni miongoni mwa miradi ya kijamii inayotekelezwa kijijini hapo kwa kutumia umeme unaotokana na mradi wa umeme jua, ambao umefadhiliwa na serikali.
 Taa maalum iliyowekwa kumulika moja ya mitaa ya kijiji cha Tura, wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora (kushoto) kwa ajili ya kuimarisha usalama. Taa hiyo inatumia nishati inayotokana na mradi wa umeme jua unaotekelezwa kijijini hapo kwa ufadhili wa serikali.
 Nguzo za umeme katika moja ya mitaa ya kijiji cha Tura, wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora. Nguzo hizo zinatumika kuunganisha umeme katika makazi ya watu, miradi ya kijamii na taasisi za umma na dini kupitia mradi wa umeme jua unaotekelezwa kijijini hapo kwa ufadhili wa serikali.
Matukio mbalimbali wakati Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ilipofanya ziara kukagua mradi wa umeme jua unaotekelezwa katika kijiji cha Tura, kilichopo Uyui, Mkoa wa Tabora, Oktoba 1, 2019.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...