Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv.
MMOJA wa watuhumiwa wa uhujumu uchumi wa vitambulisho vya Taifa (NIDA) Astery Ndege, amehukumiwa kulipa fidia ya Sh 293,446,400.23 kama hasara aliyosababisha kwa Mamlaka hiyo kufuatia kukiri kosa lake hilo
Ndege ambaye ni mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, ameachiwa huru peke yake huku washitakiwa wengine katika kesi hiyo ambao ni aliyekuwa mkurugenzi wa NIDA, Dickson Maimu, Meneja Biashara wa NIDA, Avelin Momburi, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo wakiendelea kubaki rumande.
Hatua hiyo imekuja baada ya Ndege kuandika barua ya kuomba msamaha kwa DPP, kukiri makosa ya kuisababisha NIDA hasara ya zaidi ya Sh bilioni 1.1 yalipopelekea kuingia kwa makubaliano.
Akisoma hukumu hiyo, hakimu Mkazi Mwandamizi, Salum Ally amesema mshitakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh milioni nne kwa mashitaka mawili aliyokiri ya kuongoza genge la uhalifu na kusababisha hasara hiyo na kuongeza kuwa amezingatia kitendo cha mshitakiwa kukiri kosa lake na sheria inayoelekeza mshitakiwa kulipa faini.
Mapema kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladislaus Komanya aliwasomea washitakiwa wote mashitaka 50 badala ya mashtaka 100 yaliyokuwa yakiwakabili awali ambapo amedai washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 50, yakiwemo ya kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri, kughushi, kutoa nyaraka za uongo, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Sh 1,175,785,600.93 kwa NiDA.
Hata hivyo, ni mshtakiwa ndege pekee ndiye amekiri kutenda makosa ya kujihusisha na genge la uhalifu na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni moja, huku wenzake wakikana mashtaka hayo.
Kufuatia kukiri mwenyewe, mahakama ilimtia hatiani.
Wakili Komanya aliiomba mahakama kutoa adhabu kwa mshitakiwa kulingana na makubaliano waliyoingia. Pia amedai mshitakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na kwamba kitendo cha kaomba msamaha kitasaidia kupunguza msongamano wa watu gerezani.
Kwa upande wake wakili wa utetezi, Godwin Nyaisa amedai mshitakiwa hajaisumbua mahakama kwa kuwa amekiri na anajutia kosa lake na tayari amekubali kurejesha sehemu ya hasara kama ilivyoainishwa kwenye makubaliano yao.
Amedai mpaka sasa mshitakiwa amekaa gerezani miezi 10 hivyo, anaomba apatiwe adhabu ya faini.
Katika mashitaka kusababisha hasara inadaiwa Maimu,Ndege na Ntalima wanadaiwa kati ya Julai 19, 2011 na Agosti 31 mwaka 2015 katika maeneo tofauti ya Dar es Salaam kwa udanganyifu walisababisha hasara jumla ya Sh 1,175,785,600.93 kwa NIDA.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...