Na Woinde shizza, Arusha 

WADAU wa sekta ya Mifugo katika Halmashauri ya Arusha wameitaka jamii  kuachana na dhana potofu ya kuthamini bidhaa za nje ya nchi ni bora kuliko zinazotengenezwa hapa nyumbani, badala yake kuanza kuthamini na kutumia bidhaa zinazotengenezwa na viwanda vya nyumbani, ili kuunga mkono jitihada za Serikali na utekelezaji wa uchumi wa viwanda, kuelekea uchumi wa kati.

Wakizungumza leo Oktoba 4,mwaka 2019 wadau hao wamewaambia waandishi wa habari changamoto kubwa inayokabili wawekezaji wa sekta ya mifugo, ni uelewa duni wa jamii,kuhusu mtumizi ya bidhaa zao za ndani na kuthamini zaidi bidhaa kutoka viwanda vya nje ya nchi. 

Wamefafanua wafugaji wengi wameanza kuamka na kuanza kufuga kibiashara kwa kutumia malighafi za mifugo, kuanzisha viwanda, ikiwemo viwanda vya kuchakata ngozi, kufungasha maziwa na nyama, teknolojia ya gasi itokanayo na kinyesi cha ng'ombe, na kuongeza kuwa changamoto kubwa ni ushindani mkubwa wa bidhaa za nje, unaotokana na dhana potofu ya jamii ya watanzania kutokununua bidha zinazotengenezwa nchini.

Msimamizi wa kiwanda cha Uchakataji Nyama, 'Maasai Exports Butchery', Frenk Mollel, amesema kuwa licha ya kuwa kiwanda hicho, huzalisha bidhaa za nyama zenye ubora wa kimataifa, lakini bado wananchi hawatumii bidhaa hizo kwa wingi, jambo linalosabisha soko la ndani kusuasua.

"Watu kutoka mataifa ya nje wananunua ng'ombe hapa nchini, wanasafirisha nje ya nchi, kule wanatumia mashine kama tunazo tumia sisi, lakini wakiingiza nchini bidhaa hizo, watanzania wananunua bidhaa hizo zaidi na kwa bei ya juu, wakidhani ni bora zaidi, ilihali kiwango cha ubora kinafanana na bidhaa ambazo tunazalisha hapa nchini," amesema Mollel.

Aidha, Mollel ameishauri Serikali na Taasisi zake, kuwa mfano kwa kutumia bidhaa za ndani, ikiwemo nyama inayozalishwa hapa nchini, kwa kufanya hivyo kutawapa hamasa wananchi kutumia bidhaa zinazotengenezwa ndani ya nchi.

Kwa upande wake  mfugaji Leah Sangawe amesema ng'ombe ni zaidi ya biashara, kwa kuwa  ana uwezo wa kutoa malighafi nyingi tofauti, zinazoweza kuzalisha bidhaa ikiwemo chakula, mavazi, dawa, pamoja na mapambo na kuwashauri wafugaji kutokukatishwa tamaa na changamoto za masoko na kuendelea kuzalisha bidhaaa zenye ubora wa kushindana kwenye soko la kimataifa.

"Ng'ombe hutoa kwato kwaajili ya gundi, mifupa kwa ajili ya mapambo, ngozi kwa ajili ya viatu, maziwa na nyama kwa ajili ya chakula, kinyesi kwa ajili ya nishati hivyo unapamuuza ng'ombe nje ya nchi unapoteza faida nyingi ambazo zingesaidia kukuza uchumi wa taifa" amesema mfugaji huyo.

Sambamba na hayo, Ofisa Mifugo Halmashauri ya Arusha, Charles Ngiloriti, amesema, halmashauri imejipanga kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili wafugaji, ikiwa ni pamoja na kuwatembelea maeneo yao ya kazi, kuwapatia elimu wafugaji ili kuongeza thamani ya bidhaa zitokanazo na mifugo.

"Tumekuwa tukiwashirikisha wadau mbalimbali wa mifugo kwenye maonesho, semina na mikutano pamoja na kuwatembelea ili kubaini changamoto pamoja na kuwapatia elimu juu ya ufugaji bora wenye tija katika jamii" amesema Ngiloriti.

Daktari wa mifugo Halmashauri ya Arusha, Dk. Yohana Kiwone amewaambia wadau hao kuwa, halmashauri ipo kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji wote, hivyo wanatakiwa kutumia fursa hiyo, kutatua changamoto zinazowakabili na kufanya uzalishaji bora unaokidhi viwango vya soko la kimataifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...