Na Said Mwishehe, Michuzi TV

MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania(TanTrade) imeeleza kwa kina mafanikio ambayo wamepata katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano onayoongoozwa na Rais Dk.John Magufuli.

Mbali ya kuzungumzia mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka minne, TanTrade imesema niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Mamlaka hiyo wanampongeza  Rais wa Dk.John Magufuli kwa kutimiza miaka minne madarakani na kwa kuongoza nchi yetu kwa umahari ili kufikia katika uchumi wa kati na wa viwanda. 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Movemba 27,mwaka 2019 Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Latifa Khamis amesema kuna mafanikio makubwa yaliyopatikana ambayo Watanzania wana kila sababu ya kufahamu ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza TanTrade ni Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania  ambayo ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 4 ya mwaka 2009 na kuanza shughuli zake rasmi Septemba, 2010 na moja ya jukumu lake ni kukuza na kuendeleza biashara ya ndani na nje ya nchi ili kuimarisha biashara yenye tija katika maendeleo ya kiuchumi.

Wakati majukumu ya msingi ya Mamlaka hiyo ni pamoja na kutafuta masoko ya mazao ya kilimo, madini, vivutio vya asili, bidhaa zinazozalishwa viwandani na huduma mbalimbali zinazotolewa kibiashara. Kwa upande wa Sekta ya Kilimo, baadhi ya mazao hayo (agricultural produces or commodities) ni mahindi, kahawa, korosho, pamba, pareto, mchele, kokoa, na mazao mengine ya kimkakati. 
Amesema kwa upande wa sekta ya viwanda, ni bidhaa yoyote ya kiwandani (manufactured products) ambayo ina mahitaji ya soko la ndani na lile la nje ya nchi.  Kwa upande wa sekta ya huduma (trade in services) ni huduma zote zinazotolewa kibiashara- jukumu letu ni kutangaza huduma hizo katika masoko ya ndani na nje nchi. 

"TanTrade pia imekuwa ikiratibu utafutaji wa masoko ya mazao mengine (Nontraditional Products) yakiwemo ya asali, bidhaa za viungo (spices), mafuta ya kula na mihogo.Jukumu kubwa ambalo limekuwa likitekelezwa ni kusimamia mnyororo mzima wa thamani kuanzia kwenye hatua ,"amesema Latifa Khamis.

Kuhusu mafanikio ya TanTrade...amesema ni pamoja na taarifa za upatakinaji wa masoko ndani na nje ya nchi ambapo ameeleza mamlaka imekuwa na jukumu la utoaji taarifa za upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi, mathalan kuanzia mwaka 2017 hadi 2019 jumla ya Kampuni 31,891 zilipatiwa taarifa mbalimbali za kibiashara kuhusu bei na masoko ya bidhaa ndani na nje ya nchi. 
Amesema kati yao wafanyabiashara 405 waliweza kuunganishwa na masoko na kuuza tani 102,000 za mahindi, tani 2,000 za karanga, tani 5,000 za soya, tani 50 za ufuta, tani 7 za majani ya papai, kilogramu 200 za unga wa ubuyu, tani 2 za iliki, tani 5,000 za muhogo na tani 3.2 za tangawizi ya unga.

"Miongoni mwa bidhaa zilizoonesha uhitaji mkubwa katika masoko ya nje ni pamoja na matunda, samaki na mazao ya bahari (mwani), jamii ya mikunde, asali, kahawa, chai, korosho, viungo na vyakula.  Maulizo hayo yalitoka katika nchi za India, Nchi za ukanda wa SADC, China, Japan, nchi jirani za Afrika Mashariki (EAC), Falme za Kiarabu, Misri, Marekani, Vietnam na Ulaya.

"Mbali na kusambaza taarifa za uhitaji wa bidhaa mbalimbali TanTrade kwa kushirikiana na Wanunuzi kutoka nchi mbalimbali iliratibu semina za kutangaza fursa za biashara katika nchi zao ikiwa ni muendelezo wa kimkakati wa kupenya katika masoko yao. Semina mbalimbali ziliratibiwa ambapo wafanyabiashara na wadau 425 walishiriki ili kutambua fursa za masoko ya nje na taratibu za kuyafikia masoko katika nchi za Uswidi, Ufaransa, Ukraine, China na Rwanda,"amesema Khamis.


Ameongeza kuwa kuwa kuhusu ukuzaji na Uendelezaji wa Masoko ya Nje ya Nchi TanTrade imeendelea kukuza na kuendeleza bidhaa za kutafuta masoko kupitia Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF). TanTrade imeendelea kuratibu Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) kwa lengo la kutoa fursa za kutangaza bidhaa zilizoongezwa thamani na upatikanaji wa teknolojia ili kupanua wigo wa masoko ya nje ya nchi.

Pia upatikanaji wa teknolojia husaidia kutatua changamoto za uzalishaji hafifu wa bidhaa za kilimo, uchenjuaji wa madini n.k. Kila mwaka wastani wa kampuni 3,000 kutoka nchini na kampuni zaidi ya 500 kutoka zaidi ya nchi 35 hushiriki Maonesho hayo. Ambapo amesema mwenendo wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwa miaka minne ni kama ifuatavyo  mwaka 2016 jumla ya washiriki 2,573,    Mwaka 2017 jumla ya washiriki 2,610, Mwaka 2018 jumla ya washiriki 3,605 na mwaka 2019 jumla ya washiriki 3,860 .

Amesema maonesho haya yamekuwa na matokeo chanya, mathlani kwa mwaka 2019 mafanikio yaliyopatikana kutokana na uratibu huo ni  kwamba Kampuni 437 zilipata oda ya kufanya biashara (Business deals) zenye thamani ya Sh. 7.93 bilioni. Mauzo ya papo kwa papo yenye thamani ya wastani wa Sh. 209,450,000. Ajira za muda mfupi zipatazo 14,912 zilipatikana katika kazi mbalimbali za Maonesho kama vile ujenzi, ulinzi na usalama. Kuvutia watembeleaji wapatao 260,037 kutoka ndani na nje ya nchi.

Pia upatikanaji wa mapato ya Serikali kutokana na Kodi mbalimbali ikiwemo VAT, Ushuru wa Forodha na Kodi ya uingizaji bidhaa (Import Duty), fursa za kibiashara kwa watoa huduma mbalimbali hasa wajasiliamali wadogo wadogo  na kuongeza kila mwaka TanTrade inaratibu ushiriki wa kampuni za Tanzania katika Maonesho nje nchi hususan zile tulizo na utengamano nazo kama vile EAC, SADC ambapo wastani wa kampuni 200 hushiriki.

"Lengo la ushiriki wa makampuni ya Kitanzania kuhamasishwa kushiriki ni fursa ya kutambulisha bidhaa zao kwenye nchi hizo na kuingia mikataba ya kibiashara ili kupata masoko endelevu,"amesema.

Akizungumzia  Ukuzaji na Uendelezaji wa Masoko ya Ndani amesema TanTrade katika kutekeleza adhima ya Tanzania ya Viwanda ilianzisha Maonesho ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania yanayofanyika kila mwaka Mwezi Desemba yaliyoanza mwaka 2007 katika uwanja wa Mwl J.K.Nyerere   Barabara ya Kilwa Dar es Salaam.

Amefafanua wastani wa makampuni 497 hushiriki kila mwaka ili kuunga mkono kauli mbiu hiyo. Mafanikio kwa wazalishaji wa bidhaa nchini wanapata fursa ya kutambulisha bidhaa zao pamoja na kuhamasisha matumizi ya bidhaa za Tanzania kwa Watanzania. Kupitia Maonesho hayo wazalishaji mbalimbali wa mazao ya kilimo wameunganishwa na wenye viwanda kwa lengo la kuuza malighafi na hivyo kuwezesha kuwa na soko lenye uhakika.

Pia TanTrade kwa kushirikiana na taasisi inayosimamia wadau wa Mbogamboga na matunda (TAHA) kwa kushirikiana na Shirika la Biashara la Kimataifa (ITC) iliandaa mradi wenye lengo la kuboresha masoko ili kuongeza mauzo ya nje (MARKUP) kwa wazalishaji wa parachichi nchini. Mradi huo ulilenga kuwasaidia wazalishaji wa parachichi ili kufaidika na fursa ya upatikanaji wa mitaji ya biashara, mafunzo ya namna ya kufikia soko la nje pamoja na kuwa sehemu ya ushiriki wa maonesho mbalimbali yatakayoenda sambamba na mikutano ya kibiashara (B2B).

"TanTrade ilifanikiwa kutatua changamoto ya ukosefu wa soko la vitunguu maji ambapo, iliratibu mkutano wa umoja wa wafanyabiashara wa vitunguu maji soko la Mwanakwerekwe Zanzibar ili kuwaunganisha na wazalishaji hao na masoko yenye tija.TanTrade imefanikiwa kuratibu uanzishwaji wa vyama vya wazalishaji wa bidhaa mbalimbali nchini. Lengo la kuanzisha vyama hivyo ni kuwatambua ili kuweza kwa pamoja kuongeza nguvu ya kupenya kimasoko na pia kuwasaidia katika kutatua changamoto za kimasoko. Vyama hivyo vilivyoratibiwa uanzishwaji ni Wazalishaji wa bidhaa za ngozi (TALEPA), Wazalishaji wa Viungo vya Chakula (TASPA) na Wazalishaji wa bidhaa za mihogo (TACCAPA) ,"ameongeza.

Ametaja mambo mengine yaliyofanyika kwa mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka minne ni utoaji wa mafunzo kwa wazalishaji wa bidhaa za kilimo.TanTrade ilitoa mafunzo kwa wazalishaji wa bidhaa mbalimbali nchi ikiwa ni malengo ya kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vinavyokidhi mahitaji ya masoko, kutambua na kushauri mbinu bora za kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo ya kibiashara katika mnyororo wa thamani. 

Amesema mafunzo hayo huwa shirikishi na taasisi zingine za kimkakati. Mafunzo yametolewa ni kwa wazalishaji wa bidhaa za Mafuta katika zao la Alizeti kwa mkoa wa Lindi, Zao la Mwani, Kahawa kwa Zanzibar, Zao la Muhogo. 

Kuhusu kuimarisha biashara za mipakani amesema TanTrade kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara inatekeleza mipango mbalimbali yenye lengo la kuwasaidia wafanyabiashara kukidhi vigezo vya kibiashara, kujenga mazingira rafiki ya biashara na kurahisisha bidhaa kuvuka mipaka kupelekwa nchi jirani. 

Utekelezaji huo ni pamoja na uimarishwaji wa Kamati za Pamoja Mipakani (JBC) na kutoa mafunzo juu ya sheria na taratibu za kufanya biashara mipakani. Jumla ya kamati saba za pamoja (Joint Border Committees) zimeundwa katika mipaka ya Tunduma, Kasumuru, Mutukula, Rusumo, Kabanga, Sirari na Namanga. 

"TanTrade inaendelea kuzisimamia kamati hizo ili kuhakikisha zinafanya kazi na kufikia malengo tarajiwa ikiwa ni pamoja na kuratibu uondoaji wa vikwazo vya biashara visivyokuwa vya kiushuru.  TanTrade inaendelea kushirikiana na kamati hizo ili kuweza kuwa na taarifa sahihi za upatikanaji wa biashara katika mipaka ya nchini. Taarifa hizo ni kigezo muhimu katika kuhamasisha biashara za mipakani na kutoa ushauri mahususi wa kisera,"amesema Khamis.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Latifa Khamis akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 27,2019 kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi madhubuti wa Rais Dk.John Magufuli.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...