Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii
WANANCHI wa Kijiji cha Diguzi waliopo Kata ya Matuli wilayani Morogoro ambao wanajihusisha na Mradi wa kuleta mageuzi kwenye sekta ya mkaa nchini Tanzania(TTCS), maarufu 'Mkaa Endelevu'wamesema kwa sasa maisha yao yamenoga na wanajimudu kiuchumi ukilinganisha na hapo kabla ya kuwepo kwa mradi huo.
Wamesema mradi wa mkaa endelevu umesababisha wananchi wa kijiji hicho kuwa na uhakika wa maisha kichumi wao pamoja na kijiji chao na kwamba uwezo walionao hivi sasa wanachohitaji sio fedha za Serikali bali wanahitaji kuhakikishiwa usalama wa mradi huo ambao umeleta maendeleo makubwa.
Wakizungumza katika mahojiano maalumu na Michuzi Globu ya jamii, wananchi hao wamesema uwepo wa mradi huo umewafanya waondokane na utegemezi kwa asilimia kubwa, kwani hivi sasa mambo mengi wanafanya kwa kutumia fedha za mradi huo.
Mtendaji wa Kijiji cha Diguzi Redemter Matola amesema kwa maendeleo ambayo wameyapata kupitia mradi huo wanaelekea kusaidia vijiji vingine huku akifafanua kabla ya mradi wa mkaa endelevu haujafika kijijini hapo hawakuwa na mapato ya aina yoyote.
Amesema baada ya kuingia kwa mradi huo ndani ya mwaka mmoja wa utekelezaji wa mradi 2018/2019 walifanikiwa kuingiza Sh.milioni 63. "Kutokana na kuingiza kiasi hicho cha fedha, hakika tumefanya mambo mengi ya maendeleo."
Pia amesema kutokana na mradi huo kuonesha matokeo chanya wananchi wa kijiji hicho wanaiomba Serikali kuundeleza pale wafadhili watakapofikia kikomo kwani una tija kwa kijiji na nchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi kupitia mradi wa mkaa endelevu Chilunda Iman amesema kwa maendeleo waliyoyapata kwa mwaka mmoja imewafanya wajiamini na hawana muda wa kusubiri Sh.milioni 50 za kila kijiji kwani wenyewe kupitia mradi huo wanao uwezo wa kupata zaidi ya fedha hizo kupitia mradi huo.
Amesema kabla ya mradi huo maisha yalikuwa magumu, lakini baadae ndio wamegundua kumbe walikuwa wamekalia rasilimali muhimu katika kijiji chao.
"Tuwe wakweli hapa katika kijiji chetu wala hatuna haja ya kusubiri wala kuhitaji Sh. Milioni 50 za Rais kwa kila kijiji.Katika milioni 63 ambazo tumezipata, tumetumia Sh.milioni 48 kufanya maendeleo na tunaendelea.
"Tumejenga choo cha kijiji Sh.milioni tatu, tuweka umeme jua kwenye Zahanati kwa gharama ya Sh.milioni moja, tumefanya ukarabati wa tanki la maji kwa Sh.milioni moja na tunajenga nyumba ya mwalimu kwa Sh.milioni 13.8.
"Pia kuna fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya kutumika kulipa gharama za ulinzi wa msitu wetu wa kijiji ambao ndio tunautegemea kwa ajili ya mradi wetu wa mkaa endelevu,"amesema.
Akizungumza kuhusu mradi huo wa mkaa endelevu, Ofisa Kujemgea Uwezo kutoka Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania(TFCG), Simon Lugazo ameeleza kwamba vijiji 30 ikiwemo cha Diguzi wilayani Morogoro, Kilosa na Mvomero vimenufaika na mradi huo kwa kujengewa uwezo wa kutumia rasilimali ya misitu kwa njia endelevu.
Amesema kilichosemwa na wananchi wa Diguzi ndicho hicho hicho kinachosemwa na vijiji vingine ambavyo mradi huo upo." Lengo letu sisi kama TFCG, Mjumita na TaTEDO kupitia TTCS chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswis (SDC) kumtoa mwananchi wa kijijini kwenye umaskini," amesema.
Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili ya Kijiji Jonathan Biko amesema pamoja na mafanikio kuna baadhi ya changamoto ambazo nazo zimekuwa sehemu ya kuwafanya kuongeza jitihada kuhakikisha mradi wao unakuwa salama na endelevu.
Ametaja baadhi ya changamoto ni uelewa finyu kuhusu utunzaji misitu kwa maendeleo endelevu, uhaba wa vifaa duni vya ulinzi na wafugaji kuingiza mifugo kwenye misitu hali inayoibua migogoro zaidi.
" Unaenda kukamata muhalifu kwa kutumia vyombo vya asili huku yeye ana silaha ya moto hii ni changamoto kubwa,"amesema. Aidha, Biko amesema pamoja na changamoto hiyo wameendelea kulabiliana nazo kwa kufuata taratibu za kisheria.
Amesema katika msimu wa 2019/2020 wanatarajia kuKusanya mapato zaidi ya Shilingi Milioni 60 ambazo zitatekeleza miradi mipya na kumalizia ya zamani.
Sehemu ya msitu wa hifadhi ya kijiji cha Diguzi ambao umetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mkaa endelevu unavyoonekana.
Mweka Hazina wa Kamati ya Maliasili ya Kijiji, Angelina Mugasa kizungumza kuhusu namna ambavyo kijiji chao kimepiga hatua kimaendeleo kutokana na utekelezaji wa mkaa endelevu kijijini hapo
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Diguzi wilayani Morogoro wakiwa kwenye kikao cha kuelezea mafanikio yaliyopatikana kupitia mradi wa mkaa endelevu.
Mweka Hazina wa Kamati ya Maliasili ya Kijiji, Angelina Mugasa kizungumza kuhusu namna ambavyo kijiji chao kimepiga hatua kimaendeleo kutokana na utekelezaji wa mkaa endelevu kijijini hapo
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Diguzi wilayani Morogoro wakiwa kwenye kikao cha kuelezea mafanikio yaliyopatikana kupitia mradi wa mkaa endelevu.
Mtendaji
wa Kijiji hicho cha Diguzi wilayani Morogoro Redemter Matola
akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wananchi wa kijiji
cha Diguzi kuhusu maendeleo yaliyopatikana kupitia mradi wa kuleta mageuzi
kwenye sekta ya mkaa nchini Tanzania(TTCS).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...