Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 27 Novemba, 2019 amepiga marufuku halmashauri zote za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya hapa nchini kukopa fedha za kutekeleza miradi kutoka benki, na badala yake ameagiza miradi hiyo itekelezwe kwa kutumia fedha za bajeti na mapato ya ndani ya halmashauri hizo.


Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo wakati akiwasalimu wananchi wa Ushirombo katika Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita akiwa safarini kutoka Dodoma kwenda Chato Mkoani Geita.

Kabla ya kuwasalimu wananchi hao, Mhe. Rais Magufuli amesalimiana na wananchi wa Kahama Mkoani Shinyanga ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji huo Bw. Anderson David Msumba amemueleza kuwa halmashauri hiyo imekopa shilingi Bilioni 8 kwa ajili ya kujenga kituo cha mabasi.

Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mkurugenzi huyo kuachana na mkopo huo na amepiga marufuku halmashauri zote nchini kwenda kukopa benki fedha za kutekeleza miradi, na kwa ambazo zimeshakopa kurejesha fedha hizo vinginevyo Wakurugenzi wa halmashauri hizo wataondolewa katika nyadhifa hizo.

Amefafanua kuwa mamlaka ya kukopa fedha za miradi ya Serikali yapo mikononi mwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na sio kila halmashauri kukopa inavyotaka tena kwa riba kubwa kwa kuwa mwishowe Watanzania wote ndio watakaowajibika kuilipa kupitia hazina.

Akiwa katika safari hiyo Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Igunga, Nzega, Tabora pamoja na maeneo yote yaliyopangwa kupitiwa na mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kuwa matatizo ya maji yanayowakabili wananchi hao yatakwisha baada ya mradi huo kukamilika.

Mhe. Rais Magufuli amesema mradi huo ambao utagharimu shilingi Bilioni 620 hadi kukamilika upo katika hatua za ujenzi na mara maji yatakapofikishwa katika maeneo hayo Serikali itahakikisha yanasambazwa kwa wananchi.

Kabla ya kufika Igunga, Nzega na Tabora, Mhe. Rais Magufuli amesalimiana na wananchi wa Shelui Mkoani Singida ambapo amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo kutoa shilingi Milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha Shelui ifikapo Januari 2020, baada ya wananchi hao kuomba wasaidiwe kujengewa Kituo cha Afya kama walivyoahidiwa miaka ya nyuma.

Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa maeneo hayo pamoja na maeneo mengine ya Isaka, Kahama, Masumbwe, Uyovu Runzewe na Bwanga kwa mabadiliko makubwa ya kimaendeleo na amewahimiza kuendelea kuchapa kazi za uzalishaji mali hasa wakati huu ambapo mvua zinanyesha ili kujihakikishia chakula na kipato zaidi kutokana na kilimo.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano imechukua hatua mbalimbali za kupigania maslahi ya Watanzania ikiwemo sekta ya madini ambapo pamoja na kuwatetea wachimbaji wadogo imetunga sheria ya kuhakikisha nchi inanufaika na rasilimali hiyo, na katika hilo ameipongeza kampuni ya dhahabu ya Barrick kwa kukubaliana na Serikali kuunda kampuni ya pamoja iitwayo Twiga ambapo Serikali itakuwa inapata faida kwa asilimia 50 na kampuni ya Barrick itapata asilimia 50.

Akiwa Kahama, Mhe. Rais Magufuli amewasikiliza akina Mama watatu waliokuwa wakidai kudhurumiwa haki zao ambapo ameagiza Askari Polisi (Koplo Pascal Edward) anayedaiwa kusababisha kifo cha Mme wa Evanis Raymond Mzare baada ya kumgonga na gari, kusimamishwa kazi mara moja na hatua za kijeshi kuchukuliwa dhidi yake kutokana na kudaiwa kufanya njama za kuharibu kesi inayomkabili.

Pia amemuagiza Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga ACP - Sofia Jongo kumkamata mtu aitwaye Daudi anayedaiwa kumpiga hadi kumvunja mkono Mama aitwaye Maria Mavita wakati akifanya kazi zake za kuponda kokoto na amemuagiza Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama Bw. Clement Mkusa kufuatilia kesi ya Mama aitwaye Joyce Lenard anayedai hati ya nyumba yake imeghushiwa na kuna njama zinafanyika kumpora nyumba hiyo.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
27 Novemba, 2019

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...