Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii.
SERIKALI imesema itashirikiana na mtoto Anna Zambi bega kwa bega kuhakikisha anatimiza ndoto zake alizozipanga kabla hajafikwa na msiba mkubwa wa kuondokewa na wazazi wake wote wawili pamoja na wadogo zake watatu kwa mpigo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, nyumbani kwa kina Anna, Goba jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na watoto, Dkt. John Jingu amesema inafahamika kuwa mtoto Anna anamahitaji mengi yakiwemo ya kisaikolojia.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu tayari Serikali kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii wameshaanza kumpatia tiba ya kisaikolojia tokea alipofika Dar es Salaam jana akitokea Shuleni mkoani Tanga.
Dkt. Jingu amesema wamepata taarifa kuwa mtoto Anna ataendelea kulelewa na Mama yake Mdogo huko Arusha lakini Serikali itaendelea kufuatilia hatua kwa hatua maisha yake ili kuhakikisha anapata stahiki zake ikiwemo Elimu.
"Mtoto Anna anahitaji kusoma, hatutamuacha peke yake tutabeba hilo jukumu, ingawa Mama Mdogo amekubali kuishi nae, hatutamuachia mwenyewe tutaendelea kuwa naye mpaka pale tutaona anauwezo wa kujitegemea, kuwa mtu mzima.
Aidha Mkoa wa Dar es Salaam unapanga kufanya kitu kwa ajili ya kumsaidia mtoto Anna ambapo mpaka sasa kuna Kamati za Ulinzi wa Mtoto kila mahali ambazo zimeelekezwa kuhakikisha haki za Anna hazipotei. Maendeleo na Ustawi wa Anna vitaendelea kuwa jukumu letu.
Naye Msemaji wa Familia, Ibrahim Zambi ameishukuru Serikali kwa ujumla kwa ushirikiano katika kipindi chote cha Msiba, amesema wao kama Familia wamekaa tayari wamekubaliana Mtoto Anna ataishi na Mama yake Mdogo ambaye ni Isabella Raymond Lyimo.
Kwa upande wake Anna ameiomba serikali na jamii nzima kutomuacha peke yake. " Naombeni muwe na moyo wa kunisaidia mpaka pale ambapo nitatimiza ndoto zangu na ninawaahidi mkiniruhusu na mkinisaidia nitasoma kwa bidii ilo nije kiwasaidia wenzangu wengine ambao wako kwenye matatizo kama ya kwangu au wenye matatizo mengine," amesema Anna.
Naye Mama Mdogo wa Anna anayeenda kuishi na Mtoto huyo mkoani Arusha, Isabella Lyimo amesema, anamuomba mungu ampe nguvu za kumlea Anna, na amelipokea ombi hilo kwa moyo mmoja kwa kuwa Anna mwenyewe pia amemchagua yeye kuishi naye.
Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. John Jingu akizungumza walipomtembelea Mtoto aliyepoteza Wazazi wake wote kwa mpigo na Wadogo zake watatu, Anna Zambi nyumbani kwao Goba jijini Dar es Salaam Mtoto Anna Zambi akizungumza na vyombo vya habari leo nyumbani kwao Goba jijini Dar es Salaam

Mtoto Anna Zambi akifarijiwa na Watu mbalimbali waliomtembelea nyumbani kwao Goba jijini Dar es Salaam
Mama Mdogo, Isabella Raymond Lyimo akizungumza na Waandishi wa Habari, Goba jijini Dar es Salaam.
Msemaji wa Familia, Ibrahim Zambi akizungumza na Waandishi wa Habari, Goba jijini Dar es Salaam wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya alipofika nyumbani hapo.








Naikubali blog Hui ,kaka endelea na kazi nzuri
ReplyDelete