Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof.Ibrahim Hamis Juma akiingia katika viwanja vya Shule ya Sheria kwa vitendo (School of Law) kwa ajili ya kuwapokea na kuwakubali Mawakili wapya wapatao 558 ikiwa ni sherehe ya 61.

Na Magreth Kinabo, Innocent Kansha na Tawani,Salum.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewashauri Mawakili wapya kutumia elimu ya sheria kibiashara ili kuweza kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira katika sekta hiyo.

Kauli hiyo ameitoa leo Desemba 13, 2019  katika mahafali ya 61 ya kuwapokea na kuwakubali Mawakili wapya 558 yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sheria kwa Vitendo (School of Law)  jijini Dar es Salaam.

Ambapo alisema sekta hiyo, katika karne ya 21 inakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni shinikizo la kiuchumi, kijamii na mabadiliko ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Alisema uzoefu wa huko Marekani katika kukabiliana na changamoto ya  Mawakili kukosa ajira ni kuwapatia elimu maalum ya biashara, na mbinu za kufanya biashara.

“Mawakili lazima watambue Makampuni yao ya Uwakili (Law Firms) ni biashara kama zilivyo biashara zingine. Ujuzi wa biashara utamwezesha Wakili afahamu biashara ya Kampuni yake ya Uwakili. ujuzi wa biashara ni zana ya kuendeshea Kampuni yako ya Uwakili au biashara nyingine yoyote ile”, alisema Jaji Mkuu.

 Aidha, alisema kuwa ujuzi katika biashara utawaweka katika hali ya utayari wa kushidana katika soko la huduma ya uwakili katika dunia ambayo mipaka ya huduma hizo  na zinginezo zenye ushindani mkubwa.

Aliongeza kuwa changamoto ya Mawakili kukosa ajira za kudumu ipo katika  nchi nyingi kama  vile Australia, Marekani, na Kanada.

“Mawakili lazima mkubali ushindani kutoka nje ya Tanzania. Jengeni madaraja ya ushirikiano na Mawakili wenzenu vijana wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili mtafute biashara ndani na nje ya Tanzania”, alisisitiza.

Aliongeza kwamba mawakili hao, wanapaswa kujifunza lugha za kimataifa  kwa ufasaha mfano:- Kiingereza, Kifaransa na Kichina.

Naye Mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Onorius Njole amewashauri, kuwa kwenda kufanya kazi katika maeneo yaliyo mbali na miji mikubwa yakiwemo maeneo ya vijijini kwa kuwa yana uhitaji mkubwa wa huduma hizo.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Dkt. Rugemeleza Nshala aliwasii wafanye kazi za uwakili kwa bidii, weledi na kuzingatia maadili ili kuiwezesha Mahakama kutimiza jukumu la msingi la kutenda haki.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma hapa Tanzania inaonyesha kuwa ni idadi ndogo  ya wahitimu wa Sheria walioomba kujaza nafasi za kazi katika Utumishi wa Umma ndio walifanikiwa kupata ajira 2017/2018, ambapo  walioomba walikuwa 3,250 waliopata walikuwa 88 sawa na asilimia 2.7na mwaka  2018/22019 walioomba walikuwa 2,826 waliopata walikuwa 19 sawa na asilimia 0.6.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe.Sharmillah Sarwatt akitaja majina ya Mawakili wapya waliokubaliwa na kuapishwa leo katika katika viwanja vya Shule ya Sheria kwa vitendo (School of Law).
Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) pamoja na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt Eliezer Mbuki Feleshi (wa tatu kushoto) wakiwa na baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakifuatilia sherehe hiyo.
Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) pamoja na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt Eliezer Mbuki Feleshi (watatu kushoto)wakiwa na baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiinama kwa ajili ya kuwapokea na kuwakubali Mawakili hao.
Mawakili wapya waliokubaliwa na kuapishwa leo wakitoa heshima kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Wajumbe wa Baraza la Elimu ya Sheria kwa Vitendo wakifuatlia sherehe ya kuapishwa Mawakili hao.
Mawakili hao wakiwa katika picha ya pamoja

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...