Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyasosi wilayani Bariadi
kabla ya kuwasha umeme katika eneo hilo.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani ( mwenye shati la bluu) akisalimiana na watumishi mbalimbali wa
Mkoa wa Simiyu mara baada ya kufika katika uzinduzi wa Kituo cha
Kupokea na Kutawanya Njia kuu za Umeme kilichopo eneo la Ng’ami wilayani
Bariadi mkoani humo.

Eneo la Kituo cha Kupokea na Kutawanya Njia kuu za Umeme kilichopo katika eneo la Ng’ami wilayani Bariadi mkoani Simiyu.

***********************************
Hafsa Omar – Simiyu
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani, amezindua Kituo cha Kupokea na Kutawanya Njia Kuu za Umeme
(Switching Station) kilichopo katika kijiji cha Ng’ami, eneo la
Viwandani, wilayani Bariadi, Mkoa wa Simiyu.
Uzinduzi huo umefanyika Desemba
15, 2019 ambapo Kituo hicho kinachukua umeme kutoka Kituo Kikuu cha
Mabuki kilichopo Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza umbali wa kilomita
87.2, kupitia Njia ya kusafiri umeme ya Msongo wa kV 33.
Akizungumza na waandishi wa habari
kabla ya uzinduzi huo, Dkt Kalemani, alisema kituo hicho kimezinduliwa
rasmi kwa lengo la kuimarisha hali ya upatikanaji umeme katika Mkoa wa
Simiyu ambao umejikita katika uwekezaji wa Viwanda , na hivyo unahitaji
umeme wa uhakika.
Kutokana na uwepo wa Kituo hicho,
Dkt. Kalemani alisema “natoa agizo kwa Meneja wa Mkoa, mtafute eneo la
kiwanja hapa, mjenge eneo la makazi kwa ajili ya mtumishi
atakayekiangalia kituo hiki kwa masaa 24, kwa sababu ikitokea dharura
haitowezekana mtu kutembea kilomita 10 kuja hapa hivyo ni lazima mtu
akae hapa.”
Aidha, Dkt Kalemani alitoa wito
kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, kuwahamasisha wananchi wa
eneo hilo kutunza miundombinu ya kituo husika ili wananchi wasifanye
uharibu wa aina yoyote katika eneo hilo, ambalo ni muhimu kwenye
maendeleo ya shughuli mbali mbali za kiuchumi.
Vile vile, alisema ifikapo mwezi
Machi mwakani Kituo Kikuu cha Kupoza umeme cha Imalilo kilichopo wilaya
ya Bariadi, mkoani humo nacho kitakuwa kimekamilika ambapo kitawezesha
wananchi wa Mkoa huo na maeneo ya jirani kupata umeme wa uhakika na
wakutosha kwa ajili ya matumiza ya kawaida na Viwanda vilivyopo mkoani
humo.
Aidha, alisema kuwa, Serikali
imetoa zaidi ya shilingi bilioni 4 kwa Mkoa huo ambazo zinatumika kwa
ajili ya kufanya ukarabati wa miundombinu ya umeme iliyoharibika na
kusambazia umeme katika maeneo ambayo bado hayajapata umeme.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Anthony Mtaka aliishukuru Serikali kwa kazi kubwa inayofanya ili
kuhakikisha umeme unapatikana nchi nzima.
Alisema, Mkoa huo unaenda kwenye
Mapinduzi ya Viwanda kwa haraka na ujio wa kituo hicho utaharakisha
maendeleo ya Viwanda mkoani humo.
Aliongeza kuwa, wawekezaji
waliofika mkoani Simiyu walitaka wajenge viwanda karibu na eneo ambalo
lipo karibu na kituo hicho cha umeme na Serikali imeridhia ombi hilo.
Katika ziara yake mkoani humo,
Waziri wa Nishati, alitembelea eneo kutakapojengwa Kituo cha Kupoza
Umeme, Imalilo wilayani Bariadi na kuwasha umeme katika kijiji cha
Nyasosi kilichopo wilayani humo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...