Baadhi ya meli zinazotoa huduma ya usafiri katika bandari ya Ziwa Victoria jijini Mwanza Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli(MSCL) Eric Hamissi akizungumza leo Desemba 7,2019 kuhusu meli zao zote nne zinavyojiendesha kwa faida baada ya kuweka mfumo mzuri wa kusimamia mapato yatokanayo na utoaji huduma ya usafiri wa meli.
 
Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii-Mwanza

OFISA Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli(MSCL) Eric Hamissi amesema kuwa kampuni hiyo kwa sasa meli zake zote nne ambazo zinaendelea kutoa huduma kati ya meli 14 walizonazo zinajiendesha kwa faida.

Na kwamba moja ya mkakati walionao ni kuhakikisha wanajipambanua kama kampuni ambayo itakuwa inatoa huduma zake kibiashara na huko mbele ya safari matarajio yao ni kutoa gawio kwa Serikali.

Ameyasema hayo leo Desemba 7,mwaka 2019 akiwa ofisini kwake jijini Mwanza wakati akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari nchini waliopo kwenye ziara ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari(TPA) katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano.

"Meli zetu zote nne ambazo ni Mv.Wimbi, Mv. Sangara, Mv. Umoja na Mv. Clarias zote zinajiendesha kwa faida, hakuna hata meli moja ambayo inaendeshwa kwa hasara.Tumeweka mkakati madhubuti wa kuhakikisha hatupati hasara na kwa kweli hili limewezekana.

"Ni mtarajio yetu kwa muelekeo huu nasi tutakuja kutoa gawio hata kama la Sh.milioni 20 lakini tuonyeshe kutambua kazi nzuri ambayo inafanywa na Rais wetu mpendwa katika kuimarisha usafiri wa majini,"amesema Hamissi.

Amesema kuwa chini ya Serikali ya Awamu ya Tano Kampuni hiyo mbali ya meli zake kutojiendesha kwa hasara imefanikiwa pia kuimarisha ukusanyaji mapato kwa kutumia mfumo wa ulipaji kwa njia ya kieletroniki sambamba na kudhibiti mianya yote iliyokuwa inasababisha fedha za kampuni kupotea.

Amesisitiza kuwa tayari wameshafunga mafumo wa kukusanya mapato wa kielekroniki katika Bandari za Mwanza na Nansio Ukerewe ambapo sasa yamepanda kwa asilimia 50. "Si hilo tu kwa kushirikiana na TPA sasa kazi yetu imekuwa na ufanisi mkubwa, tumeongeza mapato. Pia tumeshafunga mfumo wa kielekroniki sambamba na utoaji elimu kwa watumiaji wetu".

Amesema kila shilingi inayoingia wanaiona katika mtandao na hakuna kificho tena kwani wameweka uwazi na hivyo kila kinachoingia kinaonekana.

Ameongeza kutokana na mafanikio ambayo wanayo wanafikiria kuwa na meli mpya ya Tanzania katika Bahari ya Hindi ambayo itatoa huduma ya kusafirisha mizigo kati ya Tanzania na nchi za Mashariki ya mbali pamoja na nchi ya Comoro.

Wakati huo huo amesema kuwa usafiri wa meli unapokuwa imara maana yake ni kuimarisha uchumi wa nchi, hivyo mikakati inayoendelea hivi sasa nchini kutasaidia kujenga uchumi imara kutokana na kuendelea kuboreshwa kwa miundombinu ya meli nchini.

"Kutokana na umuhimu na urahisi wa usafiri wa meli pia Serikali ya Rais Magufuli, imetenga Shilingi bilioni 16 kwa ajili ya kujenga chelezo kubwa ambayo itabeba meli kubwa yenye uwezo wa tani 4,000,"amesema Hamissi

Amesema kwa muda mrefu ukarabati wa meli haujafanyika ambapo kwa mara ya mwisho ulifanyika mwaka 1960 kwa meli ya Mv. Victoria.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...