Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu kesho Desema 4,2019 inatarajia kutoa uamuzi wa kama ipokee kielelezo cha CD iliyohifadhi video iliyorekodiwa wakati wa mkutano wa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe au la.

Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa utetezi katika kesi hiyo ya uchochezi dhidi ya Zitto inayounguruma mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kupinga kupokelewa kwa kielelezo hicho kwa madai kuwa  shahidi anayepataka kutoa kielelezo hicho mahakamani hajaeleza ni namna gani video hiyo ilirekodiwa.

Akiwasilisha hoja zake za kupinga, wakili wa utetezi, Jebra Kambole amedai kuwa nyaraka inayotakiwa kutolewa na Sajent James ambaue ni shahidi wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo ni ya kielektroniki hivyo inatakiwa kufuata maelekezo ya sheria yanayohusu utoaji wa kielelezo cha kielektroniki.

Amedai CD ambayo inatakiwa kupokelewa mahakamani haijarekodiwa na shahidi huyo hivyo ameshindwa kukithi matakwa ya kifungu cha 18 (2) (a) cha sheria hiyo ya kielektroniki na kwamba shahidi huyo ameshindwa kuonesha mashine iliyotumika kurekodi na kama ilikuwa inafanya kazi vizuri hivyo ameiomba mahakamani isipokee kielelezo hicho.

Akipinga hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga amekiri kuwa kielelezo ambacho shahidi wao anataka kipokelewe na kitumike kama ushahidi mahakamani ni cha kielektroniki.

Amedai kitu ambacho shahidi amekuja kukielezea mahakamani hapo ni kuhusu uchunguzi walioufanya katika video kama ni halisi au la na kwamba hakuna kifungu ambacho upande wa utetezi wamekielezea  kwamba aliyerekodi video ndio anayepaswa kutoa kielelezo hicho.

Kufuatia mabishano hayo, Hakimu Shaidi amesema atatoa uamuzi kesho kama kielelezo hicho kipokelewe au la.

Mapema,  shahidi wa 14 ambaye ni Mtaalamu wa Uchunguzi wa Kisayansi kutoka Makao Makuu ya Polisi, Sajent James (52) alidai alipata barua iliyoambatanishwa na CD  kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni ikielekeza kufanya uchunguzi wa picha iliyomo kwenye kielelezo hicho.

Alidai barua hiyo ilipewa namba OB/IR/8291/2018 ya Oktoba 10,2018 ililetwa na Koplo Faraji na baada ya kuipokea,  mkuu wake wa kazi, SP Tumaini alimpa jukumu la kufanya uchunguzi ambapo baada ya uchunguzi aligundua kuwa video iliyohifadhiwa kwenye CD ni halisi hivyo aliandaa hati kwa mujibu wa kifungu cha 202 (1) cha Sheria ya Mwendendo wa Makosa ya Jinai (CPA) na katika ripoti ya uchunguzi wa kielelezo hicho aliandika Desemba 6, 2018 na kuiomba mahakamani ikipokee kielelezo hicho na kioneshwe kilichomo ndani ya CD.

Katika kesi hiyo, Zitto anadaiwa Oktoba 28, 2018 akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, uliyofanyika katika Makao Mkuu ya ofisi ya Chama cha ACT Wazalendo alitoa maneno ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.

Inadaiwa alisema " Watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya Nguruka, Polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua".

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...