Mkuu wa mkoa wa Geita Bwn. Robert Gabriel akizungumza na Waandishi wa Habari
Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Na Lydia Churi- Chato, Geita
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kesho
anatarajiwa kuzindua jengo jipya la Mahakama ya wilaya ya Chato ambapo wilaya
hiyo pamoja na baadhi ya wilaya na Mikoa nchini hivi sasa ina majengo ya kisasa
yanayorahisisha utoaji wa huduma za Mahakama.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari leo mkoani Geita, Mkuu wa Mkoa wa Geita Bw. Robert
Gabriel amesema majengo mengine mawili mapya ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita
na Mahakama ya wilaya ya Bukombe yatazinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma Alhamis Desemba 19 mwaka huu.
Kuzinduliwa
kwa jengo la Mahakama ya wilaya ya Chato kutaongeza idadi ya Wilaya na Mikoa
yenye majengo mapya na ya kisasa ya Mahakama. Wilaya zenye majengo mapya ni
pamoja na Ruangwa, Mkuranga, Kigamboni, Ilala, Bagamoyo, Kondoa, Longido, Kilwa
na Bukombe. Baadhi ya mikoa yenye majengo mapya ni Pwani, Simiyu, na Geita.
Mahakama ya Tanzania inaendelea na ujenzi wa majengo yake katika maeneo
mbalimbali nchini.
Mkuu
wa Mkoa wa Geita amesema, sambamba na uzinduzi wa majengo ya Mahakama, Rais
Magufuli pia ataweka jiwe la msingi ujenzi wa jengo la ofisi ya Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji wilayani Chato.
Aidha,
Rais Magufuli pia ataweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Msikiti wa kisasa
(Al-Huda) pamoja na kuzindua miradi ya visima vya maji katika maeneo ya shule
ya msingi Chato pamoja na kuzungumza na wananchi wa mkoa wa Geita na Taifa kwa
ujumla.
Mkuu
huyo wa Mkoa pia alitoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri kuwawahisha
wananchi kwenye matukio haya muhimu kwa maendeleo ya taifa pamoja na wananchi
kwa ujumla.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...