Wizara ya Fedha na Mipango
inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa iliyoandikwa kwenye gazeti la
Mtanzania toleo la tarehe 18/12/2019 yenye kichwa cha habari “Wastaafu
EAC waibuka na mafao yao” ambapo taarifa hiyo ilieleza kuwa wastaafu wa
iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki hawajalipwa mafao yao kwa miaka 40
iliyopita.
Wizara ya Fedha na Mipango
inapenda kuufahamisha Umma kuwa imekwishawalipa wastaafu wa iliyokuwa
Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mujibu wa “Hati ya Makubaliano” (Deed of Settlement)
iliyosajiliwa Mahakama Kuu tarehe 21/09/2005, kati ya Serikali na
watumishi wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hati ya Makubaliano
ilibainisha wazi mambo yafuatayo:-
- Wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walikubali kufuta madai yao yote yaliyokuwa katika Kesi Na. 95 ya mwaka 2003, waliyoifungua Mahakama Kuu ya Tanzania;
- Serikali ilikubali kuwalipa wadai wote waliokuwa wamefungua kesi mahakamani na wengine wote waliofanya kazi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kabla ya Juni 30, 1977, na baada ya malipo hayo kufanyika, Serikali isingedaiwa tena;
- Serikali ilikubali kuwalipa wastaafu 31,831 jumla ya shilingi 117.0 bilioni kwa misingi ya stahili ya kila mmoja kulingana na taarifa ya kila mmoja wao kwenye jalada au nyaraka nyingine zilizothibitishwa. Aidha, Serikali ilikubali kuchukua gharama za mawakili wa wadai ili malipo wanayolipwa wastaafu hao yasikatwe chochote.
Zoezi la ulipaji mafao kwa ujumla
lilikamilishwa mwaka 2009/2010 na serikali iliiagiza Wizara ya Fedha na
Mipango kuendelea kushughulikia madai halali yatakayojitokeza, hususan
yale yanayohusu mirathi kwa wahusika katika zoezi hili (case by case basis) kwa
kutumia Sheria na taratibu zilizotumika katika zoezi husika. Hadi
Desemba 2013 jumla ya wastaafu 31,788 kati ya 31,831, walikwishalipwa
kiasi cha Shs 116,880,813,918.39 ikiwa ni sawa na asilimia 99.9 ya fedha
zote zilizokubalika kulipwa.
Kwa maelezo haya Serikali kwa
mara nyingine tena inarejea kusisitiza kuwa wastaafu wa iliyokuwa
Jumuiya ya Afrika Mashariki wamelipwa haki zao zote kwa mujibu wa sheria
na inatoa wito kwa wastaafu wote wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika
Mashariki kukubali kuwa malipo yaliyolipwa baada ya uhakiki ni halali
kwa mujibu wa sheria.
Kwa kuwa Serikali inatoa
kipaumbele kwa maslahi ya watanzania wote hususan wanyonge, hata mara
baada ya kuwa imelipa mafao hayo, bado imefungua mlango wa kupokea na
kuendelea kusikiliza madai ya mtu mmoja mmoja na kulipa baada ya
kujiridhisha na uhalali wa madai husika.
Aidha, Serikali inawasihi sana
wazee wetu hawa kujiepusha na upotoshaji na udanganyifu kutoka kwa
wajanja wachache wanaotaka kujinufaisha kupitia migongo yao kwa
kuendelea kujidai kwamba wao wana uwezo wa kusimamia madai yao ambayo
hayapo.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
DODOMA
20 DISEMBA, 2019
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...