Serikali ya Tanzania na ya Namibia zajidhatiti kukuza na kuendeleza kiwango cha biashara na uchumi
kwa kutumia rasilimali zinazopatikana kati ya mataifa hayo.
Makubaliano hayo yamefikiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof.
Palamagamba John Kabudi (Mb) pamoja na Naibu Waziri Mkuu na Waziri Wizara ya Uhusiano na
Ushirikiano wa Kimataifa ya Namibia, Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwah wakati wa kuhitimisha Mkutano wa
pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Namibia jijini Dar es
Salaam.
Prof. Kabudi amesema kuwa kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Namibia bado ni kidogo
kikilinganishwa na fursa zilizopo, licha ya kiwango hicho kukuwa kutoka shilingi milioni 2,562.81 kwa
mwaka 2010 hadi shilingi milioni 21,830.3 kwa mwaka 2018.
Kutokana na takwimu hizo, Prof. Kabudi amesema ni dhahiri kwamba mamlaka husika zinatakiwa
kufanya jitihada za kutosha kwa kuhamasisha na kukuza uwekezaji baina ya nchi hizo. Aidha, pamoja na
mambo mengine, Prof. Kabudi ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka Namibia kuja
kuwekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo, sekta ya mafuta na gesi, kilimo na biashara,
viwanda vya dawa, ujenzi na utalii pamoja na uvuvi.
" Serikali ya Tanzania inafanya jitihada mbalimbali za kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini ili
kuhakikisha kuwa wawekezaji wanawekeza mahali salama. Jitihada hizo ni pamoja na utekelezaji wa
blue print ambao unasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu - Uwekezaji" amesema Prof. Kabudi
Ameongeza kuwa kutokana na jitihada hizo, ripoti ya Benki ya Rand Merchant ya Afrika Kusini
imeonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya saba (7) bora kwa uwekezaji kati ya nchi 52 za Afrika.
Aidha, ripoti ya The African Index (AII) 2018 imeonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 13 kati ya
nchi 54 kwa kuwa na masoko na vivutio vya utalii.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa Namibia,
Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwah amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na kwamba ushirikiano wa Namibia
na Tanzania ni wa kindugu,kidiplomasia,kiuchumi na ni wa kudumu.
"Napenda kutumia fursa hii kuwasihi sana wafanya biashara kutoka nchini Namibia na Tanzania
kushirkiana na kuona namna ya kukuza sekta ya biashara, utalii, kilimo, viwanda vya dawa, ujenzi
pamoja na uvuvi kwani kupitia uwekezaji huo tutaweza kukuza kiwango cha mapato kati ya mataifa
yetu," amesema Nandi-Ndaitwah.
katika mkutano huo, nchi hizo zimekubaliana kuendeleza ushirikiano katika Utamaduni, Sanaa na
Michezo; Ushirikiano katika sekta ya Utalii pamoja na ushirikiano kwenye maendeleo ya vijana. Katika
maeneo mengine, majadiliano yanaendelea na pande hizo mbili zimekubaliana hadi kufikia mwezi Machi
2020, Hati za Makubaliano ziwe zimesainiwa katika maeneo hayo.
Mkutano huo wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Namibia ulianza
katika ngazi ya maafisa waandamizi wa Serikali na kufuatiwa na ngazi ya Makatibu Wakuu na
kuhitimishwa na Mawaziri wa Mambo ya nje jana jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb),
akibadilishana hati ya makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na biashara na Naibu Waziri
Mkuu na Waziri Wizara ya Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa ya Namibia, Mhe. Netumbo Nandi-
Ndaitwah wakisaini leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb),
pamoja na Naibu Waziri Mkuu na Waziri Wizara ya Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa ya Namibia,
Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwah wakionesha hati za makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi
na biashara mara baada ya kusaini hati hizo leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwasilisha hotuba yake wakati wa kuhitimisha Mkutano wa pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Namibia leo jijini Dar es Salaam. Wengine kulia ni Balozi wa Namibia nchini Tanzania Mhe. Theresia Samaria, Naibu Waziri Mkuu na Waziri Wizara ya Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa ya Namibia, Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwah, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb), Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko, (Mb) pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa, (Mb).
Baadhi ya Makatibu wakuu, maofisa waandamizi, maofisa wa serikali pamoja na waandishi wa habari wakifuatilia ufunguzi wa mkutano wa JPC leo jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...