Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu
(kulia) akimkabidhi Mwenyekiti wa bodi wadhamini wa Taasisi ya MOI Prof.
Charles Mkony sheria pamoja mpango mkakati wa Taasisi hiyo kwa ajili
utekelezaji.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisisitiza jambo
wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya wadhamini wa Taasisi ya MOI mapema
leo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya MOI Dkt.
Respicious Boniface akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya
wadhamini iliyozinduliwa rasmi mapema leo na Waziri wa Afya Ummy
Mwalimu.
Mwenyekiti mpya wa Bodi ya
Wadhamini wa Taasisi ya MOI Prof. Charles Mkony akiongea jambo wakati wa
uzinduzi wa bodi ya mpya ya wadhamini ya Taasisi hiyo ambayo
imezinduliwa rasmi leo na Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiwa katika picha ya
pamoja na Bodi mpya ya wadhamini wa Taasisi ya MOI aliyoizindua mapema
leo.
……………………
Na WAJMW-DSM
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Mhe. Ummy Mwalimu Leo amezindua bodi mpya ya wadhamini ya taasisi ya
mifupa (MOI ) na kuitaka bodi hiyo kusimamia vizuri utekelezaji wa
majukumu ya kila siku ya Taasisi hiyo ili kuiwezesha kuendelea kutoa
huduma bora kwa viwango vya juu.
Waziri Ummy amesema mchakato wa upatikanaji wa wajumbe wa
bodi mpya ya MOI ulikua mgumu kwani majina yalikua mengi lakini lengo
ikiwa ni kupata wajumbe makini watakaoisimamia vyema Taasisi hiyo.
“Ndugu Mwenyekiti, Prof. Mkony pamoja na wajumbe, ni ukweli
kwamba wajumbe wa bodi hii wamechelewa kupatikana kutokana na mchujo
uliokua unafanyika miongoni mwa majina yaliyokua yamependekezwa, nitumie
fursa hii kuwapongeza mliokidhi vigezo na ni matarajio yangu
mtaisimamia vyema Taasisi hii ambayo ni tegemeo kubwa hapa nchini”.
Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na
Rais Dkt. John Pombe Magufuli imefanya uwekezaji mkubwa katika Taasisi
ya MOI jambo ambalo limepelekea huduma za afya kuimarika na kupunguza
kwa kiasi kikubwa rufaa za kupeleka wagonjwa nje ya nchi.
“Uboreshwaji wa miundombinu umepelekea kuongezekaa idadi ya
wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji hapa MOI, mwaka 2015 idadi ya wagonjwa
waliokua wanafanyiwa upasuaji hapa MOI kwa mwezi ilikua kati ya 400
mpaka 500 lakini sasa hivi imeongezeka na kufikia 700 mpaka 900 kwa
mwezi.” Waziri Ummy.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface
amesema kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya awamu
ya Tano katika Taasisi ya MOI, huduma nyingi mpya zimeanzishwa na
katika kipindi cha miaka 4 Taasisi imewafanyia upasuaji zaidi ya
wagonjwa 43,200.
“Mh. Waziri katika kipindi cha Miaka 4 ya Serikali ya awamu
ya Tano, kupitia usimamizi wa Wizara yako tumeweza kuanzisha huduma za
upasuaji wa magoti na mabega kwa njia ya matundu, upasuaji wa kunyoosha
vibiongo kwa watoto, upasuaji wa kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu
kwenye ubongo, upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo kupitia puani,
upasuaji wa mgongo kwa kufungua eneo dogo, hii ni hatua kubwa sana
kwetu.” Amesema Dkt. Boniface.
Akitoa neno la shukrani Mwenyekiti mpya wa Bodi mpya ya
Wadhamini MOI Prof. Charles Mkony ameshukuru kwa kupewa dhamana ya
kusimamia Taasisi hiyo muhimu na kuahidi kendelea kuisimamia MOI ili
iendelee kutoa huduma bora na za viwango vya juu kwa wananchi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...