Mkurugenzi wa Shirika la Karibu Tanzania Organization (KTO) Bw. Maggid Mjengwa akieleza jinsi Shirika lake linavyoshirikiana na Serikali katika kuhakikisha elimu ya mafunzo ya Malezi, maendeleo na makuzi wakati wa hitimisho la mafunzo ya Malezi, maendeleo na makuzi kwa wakufunzi wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akiwa katika picha ya pamoja na wakuu wa vyuo na wakufunzi mara baada ya kuhitimisha mafunzo ya Malezi, maendeleo na makuzi kwa wakufunzi hao jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akitoa cheti cha kuhitimu kwa Mkufunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Masasi Bi. Felister Nanguka mara baada ya kuhitimishwa kwa mafunzo ya Malezi, maendeleo na makuzi kwa mkufunzi kutoka Chuo cha Maendeleo ya Wananchi kwa wakufunzi hao jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wakuu wa vyuo na wakufunzi kutoka vyuo kumi vya Maendeleo ya Wananchi wakifuatilia mafunzo ya malezi, maendeleo na makuzi wakati wa Siku ya Mwisho ya Mafunzo hayo jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akizungumza na wakuu wa vyuo na wakufunzi kutoka Vyuo kumi vya Maendeleo ya Wananchi wakati akihitimisha mafunzo ya Malezi, maendeleo na makuzi kwa wakufunzi hao jijini Dar es Salaam. Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW



Serikali imeanza mpango wa kuwa na vituo vya malezi kwa watoto nchini nzima ili kuhakikisha wanajamii wanayapa kipaumbele malezi na makuzi kwa watoto ili kuhakikisha kunakuwa na taifa madhubuti.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha Semina ya Mafunzo ya Elimu ya Malezi, maendeleo na makuzi kwa wakufunzi kutoka vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.

Dkt. Jingu amesema kuwa vituo hivyo vitaratibiwa na Serikali ila vitaendeshwa na kusimamiwa na wananchi katika maeneo yao na mpaka sasa kuna zaidi ya vituo 1500 nchi nzima na vingine vinaendelea kuanzishwa.

Ameongeza kuwa malezi ni msingi mkubwa katika kuhakikisha tunapata kizazi chenye maadili, uwajibikaji na uzalendo katika kizazi itakayosaidia kujenga taifa bora. “Mafunzo haya ni muhimu na mmeamua suala sahihi, watoto wanahitaji malezi ya karibu na sio malezi tu bali wapate malezi sahihi” alisema Dkt. Jingu

Dkt. Jingu pia amewataka washiriki wanatumia stadi hiyo kuisaidia jamii na nchi kuweza kuwa na muelekeo mzuri kwa kuwa na vijana wazalendo wawajibikaji kwa maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo ya Ufundi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Noel Mbonde amesema kuwa Wizara ya Elimu itahakikisha inashirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha Elimu ya Malezi, maendeleo na makuzi kwa watoto inatekelezwa.

Ameongeza kuwa Wizara ya Elimu imehakikisha kila Chuo cha Maendeleo ya wananchi kinakuwa na kituo cha kulea watoto ili kuhakikisha inawasaidia watoto.

Naye Mwakilishi wa washiriki ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mbinga Bw. Lotty Mwang’onda amesema kuwa mafunzo waliyoyapata yatawasaidia kuleta mabadiliko hasa katika jamii inayowazunguka katika vyuo vyao ili kuhakikisha malezi, maendeleo na makuzi yanazingatiwa katika ukuaji wa mtoto.

Ameongeza kuwa wao kama washiriki wameshukuru kwa uzoefu na kama wataalam wa wanaofanya kazi na jamii watashirikiana na jamii kuhakikisha elimu walioyoipata inawafikia jamii inayowazunguka.

Aidha Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Karibu Tanzania KTO Bw. Aidan Mchawa ameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa ushirikiano wao na asasi za kiraia katika kuhakikisha wanatoa huduma kwa wananchi na kuhakikisha program ya Malezi, maendeleo na makuzi ya awali ya mtoto inarudisha misingi ya malezi ya mtoto hasa wa kitanzania.

Naye mshiriki Bi. Felister Nanguka ameishukuru Serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa elimu ya mafunzo ya Malezi, maendeleo na makuzi katika jamii hasa vijijini na kuahidi kufanya kazi hiyo kwa nguvu zao kwa kukaza msuli ili kuhakikisha watoto wanapata malezi stahili.

Shirika la Karibu Tanzania KOT limeandaa mafunzo kwa wakufunzi kutoka vyuo kumi vya Maendeleo ya Wananchi nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu malezi, maendeleo na makuzi ya awali ili wakaitoe elimu hiyo kwa jamii inayowazunguka.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...