Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (katikati) akikagua ujenzi wa mradi wa maji wa Orukesment Wilayani Simanjiro wakati wa ziara yake kwenye mradi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (wa pili kushoto) akikagua ujenzi wa mradi wa maji wa Orukesment Wilayani Simanjiro wakati wa ziara yake kwenye mradi. Kushoto ni mwakilishi wa Kampuni ya Jandu Plumbers, Mhandisi Kotturu Ramnadh.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akitoa maelekezo kwa Mkandarasi Jandu Plumbers kuhusiana na uekelezaji wa mradi wa maji wa Orukesment Wilayani Simanjiro. Katikati ni mwakilishi wa Mkandarasi, Kotturu Ramnadh.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (katikati) akikagua ujenzi wa mradi wa maji wa Orukesment Wilayani Simanjiro wakati wa ziara yake ya kukagua hatua ya ujenzi wa mradi.

**************************
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony  Sanga amemtaka Mkandarasi Jandu Plumbers wa Arusha anayejenga mradi wa Maji wa Orukesment Wilayani Simanjiro kuukamilisha kwa muda uliyopangwa.
Ametoa maelekezo hayo Desemba 14, 2019 alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo Wilayani Simanjiro sambamba na kuzungumza na mkandarasi.

Akiwa katika ukaguzi wa utekezaji wa mradi, Mhandisi Sanga alibaini shughuli zinazoendelea kutekelezwa na Mkandarasi kuegemea zaidi maeneo ambayo hayapelekei wananchi kupata huduma ya maji mapema iwezekanavyo kama ilivyo dhamira ya Serikali. 

Alibainisha kwamba Mkandarasi anajenga maeneo ambayo siyo kipaumbele cha mradi na hivyo alimtaka kuhakikisha anaelekeza nguvu zaidi kwenye ujenzi wa maeneo yatakayowapatia wananchi maji ikiwemo ujenzi wa chanzo, kituo cha tiba ya maji na bomba kuu la kusafirishia maji. 

”Nilichokiona hapa kwenye mradi ni kwamba Mkandarasi amejikita zaidi katika kujenga majengo ya ofisi na nyumba za wafanyakazi ambayo hayapelekei wananchi waanze kupata maji badala ya kujielekeza kwenye maeneo yenye tija ya kuleta huduma ya maji kwa haraka ili wananchi waanze kunufaika,” alisema Mhandisi Sanga. 

Mhandisi Sanga alifafanua kwamba mradi wa maji katika Mji wa Orukesment unao umuhimu mkubwa kwa wananchi wa maeneo hayo hasa ikizingatiwa kuwa umekuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu. 
“Wananchi wameusubiri sana huu mradi, wamekuwa na shauku kubwa ya kuanza kupata huduma kutoka hapa, sijaridhishwa na huu utaratibu anaoendelea nao Mkandarasi, ningependa kuona matokeo ya haraka kutoka hapa,” alisisitiza Mhandisi Sanga. 

Awali akiwasilisha taarifa ya maendeleo  ya ujenzi wa  mradi  huo kwa Mhandisi Sanga, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Babati (BAWASA), Mhandisi Iddi  Msuya ambao ndio wasimamizi wa mradi  huo alieleza tayari wamemuagiza Mkandarasi kuhakikisha anaongeza nguvu kazi ili kutekeleza maeneo nyeti kwa haraka zaidi.
Alibainisha kuwa kukamilika kwa mradi kutanufaisha zaidi ya wakazi 52,000 na mifugo katika mji wa Orkesumet pamoja na vijiji vinavyozunguka mji huo.

Mhandisi Msuya alimuahidi Naibu Katibu Mkuu Sanga kuhakikisha anasimamia vyema maelekezo aliyotoa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma mapema iwezekanavyo. Kwa upande wake mwakilishi wa Kampuni ya Jandu Plumbers, Mhandisi Kotturu Ramnadh aliahidi kukamilisha ujenzi wa mradi huo katika kipindi kilichowekwa cha mwezi Aprili, 2020. 

Aidha aliahidi kuongeza nguvu katika ujenzi wa chanzo na kituo cha tiba ya maji sambama na bomba kuu la kusafirisha maji kama ilivyoelekezwa na Naibu Katibu Mkuu Sanga. 

Mradi wa maji Orukesment unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kiarabu kwa nchi za Afrika (BADEA) na Mfuko wa Maendeleo wa nchi zinazozalisha mafuta (OFID) kupitia mkopo wa masharti nafuu ambao umetengewa jumla ya Dola za Marekani Milioni 18.42

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...